Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), ametangaza nia
ya kugombea urais, akisema akifanikiwa kukamata dola atahakikisha
anasimamia vyema rasilimali za nchi zinatumika vyema.
Mpina akihutubia katika uwanja wa shule ya msingi Mwandoya, Meatu,
Simiyu, alisema ana uwezo wa kusimamaia na kuhakikisha rasilimali
hususani fedha zinatumika ipasavyo. Alisema nchi ina tatizo kubwa la rushwa linalokwamisha jitihada,
mikakati na mipango ya maendeleo na ustawi wa wananchi, hivyo
atahakikisha wote wanaotumia fedha za umma kwa kuhifadhi benki za nje,
wanachukuliwa hatua za kisheria.
“Nia kubwa ya kutaka niwe Rais, lengo ni kuipa kipaumbele serikali
na kuhakikisha inakuwa na fedha za kutosha ili kukabiliana na changamoto
za mapato,” alisema.
Kuhusu elimu, alisema atahakikisha anaboresha mambo muhimu
yaliyokuwa ndani ya sekta hiyo, huku akisisitiza serikali ya CCM
imefanikiwa kutekeleza mikakati yenye lengo la kukuza kiwango cha elimu,
hivyo jukumu la serikali yake kama akichaguliwa Rais ataondoa vizingiti
vinavyosababisha taaluma hiyo kuonekana havifai.
Kuhusu uchumi, Mpina alisema atahakikisha mikataba mibovu
inayosababisha mapato ya nchi kuyumba, inakaa vizuri na kulinufaisha
taifa, huku akitangaza kukabiliana na wale wanaotumia mabilioni ya pesa
za serikali na kushindwa kulizilipa.
Aidha, alisema atahakikisha sekta ya afya inaimarika na kutoa
huduma kwa jamii ipasavyo ikiwamo kuwaweka watumishi wa taaluma katika
kufanya kazi wakiwa ndani ya mazingira mazuri ili kusaidia jamii ipate
huduma ya afya. “Mambo haya nitayashughulikia muda mfupi nikiingia madarakani,” alisema.
“Zaidi ya asilimia mbili ya fedha zinatoroshwa kwenda nje ya nchi
na wanaohusika hawachukuliwi hatua ingawa wanafahamika, natuma salamu
kwa watu hao katika serikali yangu wajiandae kuzirejesha hizo fedha
walizochukua,” alisema Mpina.
Naye katibu wa CCM wilaya Maswa, Jonathan Mabiya, aliwataka
wananchi kufanya uamuzi sahihi kuchagua viongozi bora wakati wa uchaguzi
mkuu.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment