Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali
Siku moja baada ya Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kutoa tuhuma nzito dhidi ya
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuandikisha wapigakura wasio na sifa,
tume hiyo imeibuka na kukanusha vikali.
Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali alisema jana
kuwa hakuna majina ya marehemu yanayoendelea kutumika katika Daftari la
Kudumu la Wapigakura hivyo CUF iache kuipotosha jamii.
Alikuwa anajibu madai ya Maalim Seif kuwa ZEC
iliandikisha na kuruhusu wapigakura wenye umri chini ya miaka 18,
walioandikishwa mara mbili, wasiokuwa wakazi na waliotumia ama majina au
picha za watu wengine.
Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema
madai hayo yamebainika katika utafiti uliofanywa na chama hicho ili
kubaini hujuma zilizofanywa na SMZ na taasisi zake ambazo zinaweza
kufanyika pia katika uchaguzi ujao.
Katika majibu yake, Ali alisema sheria na taratibu
za uchaguzi kabla ya kupiga kura, yaani daftari huhakikiwa na majina
kubandikwa hadharani katika vituo vya kupigia kura zilifanyika, hivyo
kama kungekuwa na dosari, zilipaswa kuwekewa pingamizi.
Alisema sekretarieti ya ZEC inafanya kazi zake kwa
maelekezo ya makamishna wake wakiwamo wawili kutoka CUF ambao wanafanya
nao kazi kwa ushirikiano mkubwa na hayakuwahi kujitokeza malalamiko
hayo. Alisema kabla ya kuanza uandikishaji mwezi huu,
ZEC ilikutana na wadau vyama vya siasa na kuwaeleza mambo manne
yatakayofanyika ambayo ni uandikishwaji wa mwisho kwa wapiga kura,
kuhakiki daftari la wapigakura, ikiwamo kuondoa waliokufa, kubadilisha
taarifa na kuhamisha taarifa za wapigakura.
Alisema endapo kungekuwa na kasoro, makamishna hao
wa CUF ndiyo wangekuwa wa mwanzo kulalamika kwa vile wapo jikoni na
siyo viongozi wa chama wanaolalamika kwenye vyombo vya habari.
“Kama kweli ana ushahidi wa kile anachokizungumza,
kwa nini haleti malalamiko yake ZEC badala yake analalamika kwenye
vyombo vya habari?” alihoji.
Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya
Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame alisema viongozi wenye dhamana
wanapaswa kufanya utafiti na kupata ukweli kabla ya kutoa shutuma nzito
ili wananchi wapate taarifa sahihi.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mzanzibari Mkaazi,
mtu yeyote kabla ya kusajiliwa, anatakiwa awe na cheti cha kuzaliwa,
barua ya sheha na haiwezekani mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 kupewa
kitambulisho hicho.
Alisema kabla ya kuandikishwa kuwa mpiga kura,
lazima mtu awe na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na masharti ya
kukipata lazima awe na cheti cha kuzaliwa na sheha amtambue.
Kuhusu Shein
CHANZO: MWANANCHI
Mkurugenzi huyo alikanusha madai ya kuwepo kwa kambi ya jeshi
inayotumika kuandikisha na kuwapatia watu vitambulisho vya Mzanzibari
Mkaazi bila sifa, akisema idara yake haina uhusiano wowote na kikosi
wala jeshi lolote hapa nchini.
Alisema Maalim Seif ni Makamu wa Kwanza wa Rais,
hivyo ana uwezo wa kumwita ofisini kwake wakati wowote kumwelezea madai
yake, lakini hajawahi kufanya hivyo isipokuwa mara moja baada ya mtoto
wake wa kumlea kukwama kupata barua ya sheha ya kumwezesha kupata
kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi.
Alisema utafiti wa CUF una kasoro kubwa kwa vile
mamlaka inazozishutumu hazikupewa nafasi ya kujieleza dhidi ya
malalamiko hayo, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za utafiti.
Kuhusu madai kuwa baadhi ya wafuasi wa CUF
hawapatiwi vitambulisho vya ukaazi, alisema kuna zaidi ya vitambulisho
20,000 ambavyo havijachukuliwa na wahusika, wengi wao kutoka Pemba.
Kuhusu Shein
Akizungumzia madai kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein anatakiwa kuanza kujitayarisha kisaikolojia kuwa Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali
Vuai alisema Maalim Seif hana ubavu wa kuiangusha CCM visiwani hapa.
Alisema kama alishindwa akiwa kijana hawezi kufikia malengo hayo akiwa mzee.
Vuai alisema Dk Shein ana kila sababu za kushinda
kutokana na kutekeleza vyema ilani ya uchaguzi, kulinda misingi ya amani
na umoja wa kitaifa na ndiyo maana Serikali ya Umoja wa Kitaifa
imeendelea kuwapo na kuhudumia wananchi wake.
Vuai alisema endapo Maalim Seif haridhishwi na
utendaji wa ZEC alitakiwa kuzungumza ndani ya Baraza la Mapinduzi na si
kwenye vyombo vya habari, jambo ambalo linazorotesha malengo ya
maridhiano yaliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment