Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta akimwonyesha picha aliyekuwa Mbunge wa
Bunge la Katiba, Dk Fransis Michael wakati wa ibada ya shukrani
iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
Usharika wa Kinondoni jana. Kulia ni Mbunge wa Mtera, Livingston
Lusinde.
Waziri wa
Uchukuzi, Samuel Sitta amesema changamoto zote alizokutana nazo kabla na
wakati wa Bunge Maalumu la Katiba anamuachia Mungu. Sitta alitoa kauli hiyo jana kwa waandishi wa
habari baada ya kumalizika kwa Ibada ya kutoa shukrani katika Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kinondoni.
Alisema katika kipindi hicho alikutana na malalamiko na tuhuma mbalimbali. Pia alisema, Katiba Inayopendekezwa ni tumaini jipya la Watanzania Sitta alisema mchango wake ndani ya Serikali kuhusu Katiba utabakia kuwa alama kwa Watanzania.
Katika ibada hiyo, Sitta alikuwa ameongozana na
mkewe Magreth Sitta, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma,
Celina Kombani na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Wabunge waliohudhuria ni Victor Mwambalaswa wa
Lupa, Livingston Lusinde wa Mtera na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky
Kamata aliyeimba wimbo wa shukrani kanisani hapo. Sitta alisema kila anapoanguka bado atasimama na kusonga mbele huku akiamini Mungu pekee ndiye atakayempigania.
“Katika Katiba kuna watu walijisahau na kulazimisha wengine wafuate misimamo yao, hiyo haikuwa sahihi,” alisema na kuongeza: “Shukrani hii ni matokeo ya changamoto zote
zilizojitokeza, siyo kwenye Katiba tu hata mambo mengine Mungu
aliyonitendea, nimekuwa nikijiuliza mimi ni nani mbele yake,” alisema
Sitta.
Wakati huohuo, Kamata aliwashukuru wanasiasa wenzake kuwa pamoja naye katika kipindi chote cha kuugua kwake mwaka jana.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment