Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka akiwasilisha bungeni hotuba ya
bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2015/2016, mjini Dodoma jana.
Mjadala wa Kikao cha 12
cha Bunge la Bajeti jana ulitawaliwa na vilio vya kamati za Bunge na
wabunge kuhoji sababu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto
kupewa fedha kidogo ya maendeleo, huku Wizara ya Kazi na Ajira ikikosa
kabisa fungu kutoka Hazina.
Wamesema hali hiyo inasababisha wizara hizo
kutokuwa na jipya katika kuiendeleza nchi, ikiwa ni pamoja na kumaliza
tatizo la ajira nchini.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Maendeleo
ya Jamii kuhusu bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira, mjumbe wa kamati
hiyo Maua Daftali alisema katika bajeti ya mwaka 2014/15, wizara hiyo
haikupewa hata shilingi moja ya fedha za maendeleo. “Bajeti ya wizara
hii mwaka 2014/15 ni Sh17 bilioni, kati ya hizo Sh5.8bilioni zilikuwa
kwa ajili ya kulipa mishahara, Sh8.9 bilioni kwa ajili ya matumizi
mengine na Sh2.9bilioni kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
Alifafanua kuwa hadi Aprili mwaka huu, fedha za
mishahara zilizotoka ni Sh4.7bilioni, matumizi mengine zilitoka ni Sh2.6
bilioni na hakukuwa na fedha yoyote ya bajeti ya maendeleo iliyotolewa. “Kwa mantiki hii, inaonyesha hakuna kazi yoyote ya
maendeleo iliyofanywa na wizara hii. Kukosekana kwa bajeti ya maendeleo
maana yake ni kwamba wizara hii haina jipya katika kuindeleza nchi,”
alisema Dk Daftari.
Bajeti ya wizara hiyo mwaka 2015/16 ni Sh38.8bilioni, huku Sh20bilioni zikitengwa kwa ajili ya maendeleo.
Akiwasilisha taarifa ya kamati ya Bunge ya
Maendeleo ya Jamii kuhusu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto, mjumbe wa kamati hiyo, Agness Hokororo alisema wizara hiyo
katika bajeti ya 2014/15 ilitengewa Sh8.9bilioni za maendeleo.
“Hadi Machi mwaka huu, wizara ilikuwa imepokea Sh2
bilioni sawa na asilimia 22 ya bajeti ya maendeleo. Kamati imebaini
miradi ya maendeleo haikupewa kipaumbele na hii itaathiri ustawi wa
shughuli za kijamii zinazosimamiwa na wizara,” alisema Hokororo.
Akiwasilisha hotuba ya Wizara ya Kazi na Ajira,
waziri wake Gaudencia Kabaka alisema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi
sasa zimezalishwa ajira milioni 1.9 katika sekta ya kilimo, elimu, afya,
ujenzi wa miundombinu, nishati na miradi ya kijamii pamoja na ajira
milioni moja katika sekta binafsi.
Wabunge wanena
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Maulidah Komu
alisema Serikali imeshindwa kuwasaidia watoto yatima na wale wa mitaani,
badala yake imekuwa na mikakati ya muda mrefu ambayo haiwasaidii
walengwa.
“Watoto yatima na mitaani wanapata tabu sana na
wanaingiliwa kinyume na maumbile. Mfano kuna nyumba moja ya kuwalea
ilikuwa Morogoro walikuwa wanafanyiwa kitu kibaya na Serikali haichukui
hatua,” alisema.
Mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa ameitaka Serikali
kuanzisha utaratibu kutoa mikopo kwa vijana wanaomaliza darasa la saba
ili waweze kupata fursa ya kujiunga na vyuo vya ufundi.
Alisema vijana hao wakikosa nafasi ya kuendelea na masomo huishia vijiweni kwa sababu ya kukosa fedha ya kujiendeleza kielimu.
Kauli ya Mwaiposa iliungwa mkono na Mbunge wa Viti
Maalumu (CUF), Riziki Omari Juma ambaye pamoja na mambo mengine,
alitilia mkazo zaidi mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino),
kuitaka Serikali iweke utaratibu wa kuwalinda badala ya kuendelea
kufanya uchunguzi kusaka wauaji.
“Mbona Tembo wanalindwa sana na ikitokea ameuawa
mmoja tu wahalifu wanasakwa, lakini albino akiuawa hakuna hatua
zinazochukuliwa,” alihoji.
Mbunge wa Mafinga (CCM), Mendrad Kigola alisema
tatizo la ajira kwa vijana limeendelea kuwa kubwa na kuitaka Serikali
ianze kutoa mikopo ya pikipiki kwa sababu vijana wengi wanamaliza vyuo
vikuu na kukosa ajira.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment