Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akiwakaribisha wanafunzi wa vyuo
mbalimbali nchini pamoja na waendesha bodaboda waliomtembelea nyumbani
kwake Dodoma hivi karibuni kumshawishi agombee urais.
Historia yake
Edward Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika
Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee
Ngoyai Lowassa (atafikisha miaka 62 Agosti mwaka huu). Alianza kusoma
katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967.
Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha
kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 - 1971, kabla ya
kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo
mkoani Tabora mwaka 1972–1973.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka
1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) na
baadaye Chuo Kikuu cha Bath Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi
katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya
kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na
baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.
Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano,
wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella,
Adda, Robert na Richard.
Mbio za ubunge
Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge wa Monduli mwaka
1990 na 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na
Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa
Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi
(mwaka 1995), Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3. Alikaa bila
uteuzi wowote kwa miaka miwili. Mwaka 1997–2000, Rais Benjamin Mkapa
alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na
Kuondoa Umasikini).
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena
ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu. Rais Mkapa akamteua kuwa
Waziri wa Maji na Mfugo hadi mwaka 2005. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na
kushinda kwa asilimia 95.6. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri
Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.
Uwaziri mkuu wa Lowassa ulikoma Februari 2008, alipojiuzulu
kutokana na kashfa ya Richmond. Kamati Maalumu ya Bunge ya watu watano
iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ilisisitiza kuwa wizara ya Nishati
na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu ndizo zinazopaswa kubeba lawama ya
uingiaji wa mkataba mbovu na Richmond, kampuni ambayo uchunguzi
ulionyesha kuwa ni ya mfukoni mwa watu huku Serikali ikilazimika kulipa
mabilioni ya fedha katika mkataba ambao una upungufu makubwa.
Wakati Lowassa analitaarifu Bunge kuwa
amemuandikia Rais barua ya kujiuzulu, alisisitiza kuwa “…anafanya hivyo
ili kulinda taswira ya chama chake na Serikali na kuwa shida ya wabaya
wake ni u-waziri mkuu na siyo kingine…”
Baada ya kujiuzulu, Lowassa aligombea ubunge kwa
mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na kupata asilimia 90.93 ya kura zote
na hadi sasa ndiye mbunge wa jimbo hili japokuwa amekwishaaga kwamba
hatagombea tena kiti hicho.
Mbio za urais
Lowassa ni miongoni mwa wana CCM 17 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 1995 lakini aliyepitishwa ni Mkapa. Mwaka 2005, hakugombea urais ila alikuwa na
mipango ya muda mrefu ya kumsaidia rafiki yake, Kikwete na inadaiwa kuwa
makubaliano ya Kikwete na Lowassa yalikuwa kwamba mwenzake akishaongoza
nchi kwa miaka 10 (yaani 2005 – 2015) atamtengenezea njia 2015 – 2025.
Kabla mipango hiyo haijatimia ndipo Lowassa
akapata kile ambacho Kikwete anakiita “ajali ya kisiasa”. Lakini hata
baada ya ajali ya kisiasa kutokea, nimeambiwa walikuwa na makubaliano
mengine kuwa “Kikwete angesaidia kumsafisha rafiki yake” ili mwaka huu
2015 ufikapo aweze kumuachia Ikulu ya Magogoni.
Tangu Lowassa aachie uwaziri mkuu na tangu agundue
kuwa Kikwete ‘amemkalia” kimya, alianza juhudi zake mwenyewe za
kujitengenezea njia ya kuelekea Ikulu na amefanya mambo mengi
yanayoashiria kuwa amedhamiria kuingia Magogoni.
Kama kuna mtu nchi hii ametoa michango mingi ya
rasilimali fedha katika kuchangia misikiti, makanisa, vijana, vikundi,
harambee na vinginevyo, hakuna kama Lowassa. Michango hiyo, wachambuzi
wengi wanaihusisha na mbio zake za urais.
Nguvu yake
Nguvu ya kwanza ya Lowassa ni umaarufu, yeye ni
maarufu kuliko wagombea wote wa CCM, ndani na nje ya chama hicho. Yeye
ndiye anatajwa kuliko wenzake wote na hili halina shaka.
Nguvu ya pili ya Lowassa iko kwenye uwezo wa
kirasilimali (watu na fedha). Lowassa na mtandao wake wana rasilimali za
kutosha kuendesha harakati hizi. Kwa siasa za CCM ya miaka hii
iliyowatupa mkono wakulima na wafanyakazi, rasilimali (fedha na watu) ni
kila kitu. Jambo hili linampa nguvu zaidi dhidi ya wagombea wenzake
ambao nao wanahaha huku na kule kuzisaka.
Udhaifu wake
Nini kinaweza kumfanya apitishwe
Jambo la tatu linalompa Lowassa nguvu ni kuwahi kuwa Waziri Mkuu
na kuijua kwa undani mifumo ya uendeshaji wa nchi na hata kuisimamia.
Ushawishi wake kwa mifumo hiyo umeendelea hadi sasa na nimeambiwa kuwa
kuna taasisi muhimu za kidola zimegawanyika kwa sababu ya kumuunga
mkono, watendaji serikalini nao wamegawanyika kwa ajili yake na kila
mmoja ana hofu kuwa asipofanya “booking” kwenye kambi ya Lowassa,
anaweza kukosa vyeo bwerere kwenye Serikali ijayo.
Alipokuwa Waziri Mkuu alionyesha misimamo ya
kiuongozi na kuthubutu kwingi kunakotakiwa kufanywa na mkuu wa nchi,
lakini misimamo yake na uthabiti wake unahusishwa pia na kujikuta mara
nyingi akifanya uamuzi wenye makosa mengi au wenye kuzua maswali mengi
ya kisheria.
Lakini jambo la nne ni kuzijua njia zilizompa
madaraka Kikwete mwaka 2005. Kati ya wagombea wote wa CCM kwa sasa,
huenda ni Lowassa peke yake ndiye anayezijua vizuri njia alizotumia
Kikwete kujenga mtandao mkubwa wa ushindi mwaka 2005, makanisani,
misikitini, vyuoni na kwingineko, hadi nyumba za ibada zikaimba “Kikwete
ni chaguo la Mungu”. Kwa hiyo anajua njia ipi apite kuwashinda wagombea
wengine.
Udhaifu wake
Udhaifu wa kwanza wa Lowassa ni kuwa karibu mno na
watu wenye majina yenye taswira zinazotia shaka. Kuna msemo mmoja wa
Kiingereza unaosema, “The bird with same feathers, flocks together”
(Ndege wenye mabawa yanayofanana, huruka pamoja). Marafiki wakubwa wa
Lowassa ni watu wenye pesa na matajiri, hilo linaweza kumkwamisha katika
harakati zake.
Ndiyo maana jamii imegawanyika mno juu yake,
wengine wakimuona kama mtu mwenye mipango mingi ya kifedha na
mfanyabiashara zaidi kuliko kiongozi wa nchi huku wengine wakimuona kama
kiongozi anayethubutu.
Ikiwa Lowassa hataweka wazi mgongano wa masilahi
ulioko kati yake na baadhi ya wafanyabiashara wenye tuhuma lukuki, jamii
itaendelea kumuona kama mtu asiyeweza kukemea maovu.
Kiongozi mmoja wa CCM ameniambia kuwa, hata mwaka
1995, moja ya mambo yaliyomfanya Mwalimu Julius Nyerere asimuone Lowassa
kama chaguo, ni suala la uhusiano wake na matajiri na watu wenye fedha
na ilifikia wakati mwalimu akahoji, “…kijana huyu anatoa wapi fedha zote
hizi?”
Udhaifu mwingine wa Lowassa uko katika eneo la
mapambano dhidi ya rushwa. Ikumbukwe kuwa Tanzania ilipofikia na uchumi
wake unavyozidi kuporomoka, moja ya kazi kubwa ya Serikali ijayo
itapaswa kuwa “mapambano dhidi ya rushwa” kwa maneno na vitendo
vinavyoonekana.
Alipokuwa Waziri Mkuu hakuonyesha makeke yake
kwenye mapambano dhidi ya rushwa na hakutaka kujihusisha wala
kujionyesha kuwa anawachukia wala rushwa. Pamoja na kuonyesha utendaji
mzuri akiwa Waziri Mkuu, kipengele hiki kilimuangusha na hadi leo hii
kokote kule anakokwenda hapendi kuzungumzia rushwa na wala rushwa. Huu
ni udhaifu wake mwingine mkubwa.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe
Lowassa ana uzoefu wa zaidi ya miaka 38 ya
kuitumikia CCM na Serikali, ameongoza wizara kadhaa hadi kufikia kuwa
Waziri Mkuu, bila shaka, uwezo wake wa kiuongozi, utendaji na usimamizi
vilidhihirika. CCM inaweza kuhitaji mtu wa aina yake, ambaye iliwahi
kupima utendaji wake na labda kuridhishwa nao.
Nini kinaweza kumwangusha?
Asipochaguliwa (Mpango B)
Jambo la pili ambalo linaweza kumvusha ni woga wa CCM
‘kuvunjika’. Kuna taarifa nyingi zinazoonyesha kuwa vikao vya CCM
visipolipitisha jina lake likafikishwa mkutano mkuu ili kura ndizo
ziamue, wajumbe wa mkutano huo wanaweza kutoshiriki na huenda anaweza
kukihama chama hicho na kundi kubwa la viongozi na wanachama. Ikiwa CCM
inazifahamu taarifa hizi, inaziamini na kuzithibitisha, huenda
ikampitisha na kukubali yaishe.
Jambo la tatu linaloweza kumfanya apitishwe ni
kuwa na mtandao mkubwa na ufuasi uliopitiliza kuliko mgombea mwingine
yeyote wa chama hicho. Ukimgusa Lowassa kwenye mtandao wa kijamii
utajibiwa haraka mno, ukimsema gazetini makala itajibiwa haraka na
ukimsema vibaya kijiweni kwa vijana utakodolewa macho. Amejipanga
vilivyo na CCM inaweza kuhitaji mgombea wa aina yake ambaye ana nguvu ya
kipekee ya kuweza kukisaidia chama hicho kupata ushindi.
Nini kinaweza kumwangusha?
Mambo matano yanaweza kumwangusha Lowassa. La
kwanza ni makundi. Kama nilivyoeleza, yeye ndiye mtu mwenye kundi kubwa
kuliko wagombea wote ndani ya CCM, ikiwa chama hicho kitaamua kumpata
mtu wa kati ‘neutral’ ili kukifanya chama kisitetereke, yeye ndiye
atakayekuwa wa kwanza kuenguliwa.
Lakini jambo la pili ni kashfa ya Richmond. Tangu
kashfa hiyo ilipotokea, Lowassa hakuwahi kuiongelea tena na hajawahi
kuwaeleza Watanzania alihusikaje na kama yeye hakuhusika ni kina nani
waliohusika kwa majina. Ukweli ni jambo muhimu kwa mtu anayehitaji
kuongoza nchi. Ukituhumiwa kwa kashfa kubwa kama ya Lowassa halafu
unasema tu hukuhusika bila kueleza nani walihusika huku wewe ndiye
ulikuwa Waziri Mkuu, inajenga taswira kuwa kuna jambo kubwa unalificha
na husemi ukweli kwa jamii yako. Hili linaweza kumhukumu. CCM inaweza
kumuondoa Lowassa ili kuondokana na mgombea mwenye madoa hata kama haina
uthibitisho na madoa hayo kwa asilimia 100.
Jambo la tatu linaloweza kumchuja Lowassa ni afya
yake. Pamoja na kuwa afya ni jambo binafsi na siri ya mtu lakini kwa
kiongozi, kila jambo lake ni mali ya umma. Rais Kikwete alipougua tezi
dume aliutangazia umma na hakuficha. Kwa kipindi kirefu Lowassa amekuwa
akionekana kama mgonjwa na si siri kuwa amekuwa akipata matibabu katika
hospitali za kimataifa nje ya nchi. Anapaswa awaeleze Watanzania nini
kinamsibu, la asipofanya hivyo wapinzani wake kisiasa wanaweza kuendelea
kulitumia jambo hili ipasavyo na chama chake kikaona lina mantiki na
kikalitumia kumsulubu kama “unfit person to lead the nation”. Kila chama
kinahitaji mgombea urais wake awe na afya bora, isiyofichwa na
inayoeleweka. Anapaswa kujitokeza na kufafanua hili haraka na hasa
ikizingatiwa muda umekwenda sana.
Michango ya kujitolea kila kukicha katika taasisi
mbalimbali, harambee, nyumba za ibada na maeneo mengine ni jambo jingine
linaloweza kumhukumu. Lowassa amejitolea mno katika eneo hili. Chama
chake kinaweza kujiuliza kwa nini mtu anayejiandaa kugombea urais
ajitolee kwa kiwango hiki kusaidia kuchangisha fedha na hata yeye
mwenyewe kuchangia kila panapotokea matukio makubwa?
Je, nia yake ni sahihi? Mwalimu Nyerere aliwahi
kusema kuwa “Ikulu hakuna biashara” na CCM inaweza kujitathmini ikiwa
mgombea wa namna hii akiingia Ikulu hataanza kutafuta mbinu ya
kujirudishia fedha alizokuwa akichangia. Eneo hili si salama kwa
Lowassa.
Jambo la tano ni madai kuwa kuna maelewano hafifu
na Rais Kikwete. Jambo hilo hakuna aliyethibitisha, lakini huwezi
kulidharau moja kwa moja. Katika siasa, ukishindana na walioshikilia
“mpini” unaweza kuanguka mahali usipotarajia. Pamoja na kuwa
“hawakukutana barabarani”, ukweli ni kuwa Lowassa na Kikwete wa sasa si
wale ‘ma-comrade’ wa 2008 kurudi nyuma. Hawa wa sasa ni watu tofauti na
duru za ndani ya Serikali zinaonyesha kuwa haziivi.
Kama hivyo ndivyo basi, karata za Lowassa zinaweza
kuingia shakani kwa sababu ya kutoimarisha uhusiano wake na Rais
anayeondoka madarakani, maana kwa siasa za kurithishana kwa kujuana
katika vyama tawala barani Afrika, lazima tukubali ukweli kuwa, Rais
aliyeko madarakani ana mchango na ushawishi mkubwa katika kutengeza rais
ajaye.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Namuona Lowassa akiwa na mipango mitatu ikiwa hatapitishwa kugombea urais: Mpango wa kwanza ni kuendelea kuihamasisha jamii kimaendeleo
katika taasisi za kidini, za kiraia, makundi ya vijana, wazee na
wanawake kwa mtindo huuhuu ambao amekuwa akiufanya kati ya 2008 –2015 na
hata kutoa michango yake na marafiki zake kwa jamii.
Hitimisho
Mpango wa pili ni kuishauri Serikali katika maeneo
mbalimbali ya kisera na kiusimamizi. Kwa sababu alipokuwa Waziri Mkuu
alionyesha usimamizi mzuri na ufuatiliaji imara katika ofisi za umma,
anaweza kuifanya kazi hiyo kiushauri.
Mwisho ni kurudi kwenye biashara. Lowassa ni
mfanyabiashara katika sehemu kubwa ya maisha yake. Ikiwa hatagombea
urais kwa tiketi ya CCM itakuwa muda muafaka kwake kurejea na kusimamia
biashara zake na kuachana na siasa za majitaka kama alivyowahi kutamka
mmoja wa marafiki zake.
Hitimisho
Nguvu ya Lowassa ndani ya CCM haimithiliki na hofu
ya chama hicho kuwa kumuacha nje ya ulingo kutakitetemesha haikwepeki.
Lakini ukweli ni kuwa ndani ya CCM “kuna minofu mingi” ambayo inawazuia
vigogo wakubwa wasiondoke na kuhamia vyama vingine hata kama
hawakupitishwa kugombea urais. “There is too much stake to eat in CCM
than going out”.
Ndiyo maana bado CCM ina nafasi ya kujichagulia
mgombea inayemtaka na vigogo wanaotajwa kuitikisa kama Lowassa wakiogopa
kuondoka kwa sababu wamekaa serikalini muda mrefu na sasa hawawezi
kumalizia maisha bila mfumo huo waliouzoea.
Kwa hiyo, nadhani Lowassa ataendelea kuwa
mwanachama mtiifu kwa CCM akiwa Rais au akiwa raia wa kawaida. Kama kuna
vyama vya upinzani vilikuwa “vinamtumbulia” macho kama fisi asubirivyo
mkono wa binadamu udondoke, ni vyema vikajipanga kupata wagombea wake
imara na vijijenge. Pamoja na yote haya namtakia kila la heri Mzee
Edward Lowassa katika safari yake ya kisiasa.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment