Profesa Mark Mwandosya
Profesa Mark Mwandosya alizaliwa Desemba 28, 1949 mkoani Mbeya (atafikisha miaka 68 Desemba mwaka huu). Alianza elimu yake katika Shule ya Msingi Majengo
iliyoko Mbeya Mjini (mwaka 1957 – 1958), kisha akahamia Shule ya Msingi
Chunya iliyokuwa inamilikiwa na “White Fathers” mwaka 1959 – 1960.
Aliendelea katika Shule ya Msingi Chunya “Middle School” kati ya mwaka
1961 – 1964.
Alipata elimu ya sekondari (kidato cha I – IV)
katika Shule ya Malangali kabla ya kujiunga na kidato cha V na VI katika
Shule ya Chuo Cha Ufundi, Dar es Salaam (DIT) mwaka 1969 – 1970.
Mwaka 1971, Profesa Mwandosya alikwenda Uingereza
kusomea Shahada ya Sayansi katika Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Aston
na kuhitimu kwa viwango vya juu mwaka 1974.
Mwaka huohuo 1974 aliunganisha masomo ya Shahada
ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza akibobea
katika uhandisi wa umeme na kuhitimu mwaka 1977.
Miaka miwili ya kwanza wakati anasomea shahada ya
uzamivu (1974 – 1976) alikuwa ni Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM) na alipomaliza “ubobezi” huo, alianza kufundisha chuo
hicho akiwa mhadhiri kamili mwaka 1970 – 1980.
Walimu wa UDSM waliomfahamu Mwandosya tangu
akianza kazi wamenijulisha kuwa alikuwa mtu wa kujibidiisha sana na
ndiyo maana alipanda harakaharaka katika kazi zake kitaaluma. Mwaka
1980-1983 alikuwa Mhadhiri Mwandamizi kabla ya kuwa Profesa Mshiriki
mwaka 1983 – 1987 na baadaye miaka iliyofuata akawa Profesa kamili.
Profesa Mwandosya alihamishiwa serikalini kuwa
kamishna katika Wizara ya Maji, Nishati na Madini mwaka 1985 – 1990,
akapandishwa na kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo mwaka 1990 – 1992,
akapelekwa Wizara ya Viwanda na Biashara kuwa Katibu Mkuu mwaka 1992 –
1993 kabla ya kurudi kufundisha UDSM akiwa Profesa kamili mwaka 1994 –
2000. Ndani ya chama chake CCM, Profesa Mwandosya amepitia safari ndefu tangu akiwa Shule ya Sekondari Malangali.
Amekuwa kiongozi wa vijana wa Tanu miaka ya 1967,
mwanachama mtiifu wa Tanu mwaka 1971-1977 na baadaye aliendelea kuwa
mwanachama wa CCM. Kuanzia mwaka 2000, alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa
ya wilaya yake na kuanzia mwaka 2002 ,aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu
ya chama hicho.
Profesa Mwandosya amemuoa Lucy na wana watoto na familia imara.
Mbio za ubunge
Mbio za urais
Mbio za ubunge
Profesa Mwandosya alipoamua kuingia katika siasa
za majukwaani katika ubunge, alikwenda jimboni kwake Rungwe Mashariki.
Hii ilikuwa mwaka 2000. Alipokea kijiti kutoka kwa mbunge wa CCM
aliyekuwa amemaliza muda wake na hakukutana na upinzani imara. Alishinda
kwa kipindi cha mwaka 2000 – 2005 na wakati wote wa ubunge wake,
alitumikia awamu ya pili ya urais wa Benjamin Mkapa akiwa Waziri wa
Mawasiliano na Uchukuzi.
Mwaka 2005 ulikuwa mwepesi zaidi kwa Profesa
Mwandosya, CCM ilimpitisha kwa mara ya pili jimboni hapo na kufumba na
kufumbua wapinzani “wakalala mbele”. Profesa Mwandosya akawa mbunge
anayesubiri tu kuapishwa baada ya kupita bila kupingwa.
Wakati awamu ya kwanza ya uongozi wa Rais Jakaya
Kikwete unaanza, Profesa Mwandosya aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Makamu wa Rais (Mazingira), 2006-2008 na baadaye akawa Waziri wa
Maji na Umwagiliaji 2008-2010.
Mwaka 2010, ulikuwa na matukio yaleyale ya 2005
katika jimbo la Rungwe Mashariki. Profesa Mwandosya alikosa mpinzani na
akapita bila kupingwa na kuapishwa kuwa mbunge kwa kipindi cha tatu.
(Vyama vya upinzani havikuweka wagombea).
Aliteuliwa kuwa Waziri wa Maji na baadaye Waziri Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu) hadi hivi leo.
Profesa Mwandosya amekutwa na misukosuko kadhaa ya
kiafya ikihusishwa na mazingira ya kuwekewa sumu na wapinzani wake wa
kisiasa “mapambano ya uongozi ndani ya CCM” au kupigwa vita kutokana na
misimamo yake ya kisiasa”.
Mbio za urais
Profesa Mwandosya alianza mbio za kusaka urais wa
Tanzania mwaka 2005 alipochukua fomu na kuomba ridhaa hiyo kabla ya
kushindwa katika hatua za upigaji kura na Kikwete ndiye aliyeshinda.
Hata hivyo, ameitumikia miaka 10 ya uongozi wa
Kikwete katika utulivu mkubwa akionyesha busara za kiuongozi kila mara
na wachambuzi wengi wanaichukulia hali hiyo kama maandalizi ya mara
nyingine ya kuomba ridhaa ya uongozi wa nchi kupitia kwenye chama chake.
Tayari Profesa Mwandosya ameshaeleza kuwa
hatagombea tena ubunge katika Jimbo la Rungwe Mashariki na kwamba ana
mipango mingine. Mipango hiyo inachukuliwa kuwa ni kuingia tena katika
mbio za urais.
Katika kuonyesha kwamba yuko makini na atashiriki
katika safari ya urais mwaka huu, amewahi kukaririwa na gazeti moja la
kila wiki akisisitiza kwamba “…kuteuliwa na chama kuwa mgombea urais ni
heshima kubwa na ni kilele cha utumishi ambao mwanachama anaweza kutoa
kwa chama na kwa Taifa. Itakuwa ni heshima iliyoje kwangu iwapo chama
kitaweza kunifikiria na hatimaye kuniteua kufika hapo.”
Nguvu yake
Udhaifu wake
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Nini kinaweza kumwangusha?
Profesa Mwandosya hajatangaza rasmi kuwa atawania urais kupitia
CCM, lakini maneno na vitendo vyake vinaonyesha kuwa anahitaji na
atakuwa mmoja wa wagombea.
Pia, ni mmoja wa wanachama wa CCM ambao wanatajwa
na kuonekana kama Watanzania ambao walau wanaweza kusimama na kuomba
ridhaa hiyo.
Nguvu yake
Profesa Mwandosya ni mwanataaluma aliyebobea, tena
katika elimu adhimu, uhandisi wa masuala ya umeme na ametumia taaluma
yake kuandika mambo mengi yanayohusu nishati na hata maendeleo
yatokanayo na nishati.
Amefanya tafiti mbalimbali na kuchapisha vitabu kadhaa ndani na nje ya nchi, kupitia taaluma yake, amezidi kuwa mweledi na anajua anachokisimamia. Hii ni sifa muhimu kwa kiongozi anayehitaji kuongoza dola.
Amefanya tafiti mbalimbali na kuchapisha vitabu kadhaa ndani na nje ya nchi, kupitia taaluma yake, amezidi kuwa mweledi na anajua anachokisimamia. Hii ni sifa muhimu kwa kiongozi anayehitaji kuongoza dola.
Walau kuwa na taaluma ya jambo fulani na ukaonekana umelisimamia na unalimudu.
Lakini kuna jambo la pili linalompa nguvu Profesa
Mwandosya. Mzee huyu amefanya kazi Tanzania kwa muda mrefu kushinda
wasomi wengine kama yeye wanaotafuta urais.
Tangu mwaka 1974 hadi sasa (miaka 40), amekuwa ama
akifundisha UDSM, akiongoza wizara katika wadhifa wa katibu mkuu, akiwa
mbunge na au waziri. Vyote hivyo amevifanya akiwa ndani ya nchi kwa
hiyo amekuwa karibu na wananchi na anayajua matatizo yao.
Jambo la tatu ni utulivu na busara. Profesa
Mwandosya si mtu wa kubeba mambo kwa pupa na kusimamia uamuzi wake huku
ukiwa hauna tija. Ni mtu anayehitaji kila kitu kifanywe kwa utaratibu na
kwa kuelewana.
Waziri mmoja alinijulisha kuwa, hata ndani ya
Baraza la Mawaziri la Kikwete, yeye ni mtu ambaye hutumiwa katika kamati
ndogo za mawaziri za kutatua mambo magumu yaliyowashinda vikaoni na
kwamba busara zake zimetumiwa mara nyingi kuifanya Serikali ya Rais
Kikwete iweze kuwa na utulivu.
Jambo la tatu ni kufahamika, jina la Profesa
Mwandosya si geni kwa Watanzania. Limesikika sana. Katika kufanikiwa
kuongoza nchi au kuvuka vinyang’anyiro vya ndani ya vyama, umaarufu
wenye tija ni jambo la msingi. Watanzania wanamfahamu Profesa Mwandosya kama waziri wa muda mrefu na mtu anayejiheshimu. Hii ni silaha ya kawaida kwake.
Mwisho, yeye ni miongoni mwa maprofesa wanaoishi maisha ya kawaida sana. Baadhi ya wasomi wa ngazi ya u - profesa na tena
wakifikia hizo za uwaziri na nyinginezo, huwa ni watu wa dharau,
majivuno na kujisikia. Profesa Mwandosya si miongoni mwao, labda aina ya
jamii aliyotoka ndiyo inayombeba na kumuondolea dharau na kiburi, lakini
jamii ilimkuza na kumuachia tangu zamani, nadhani yeye mwenyewe si
mpenda makuu.
Hataki kuishi maisha ya anasa, yasiyo na maana na
ambayo haoni faida yake. Watu wengi wa karibu wanamuona kama Mtanzania
wa kawaida. Hili ni jambo muhimu.
Udhaifu wake
Profesa Mwandosya ni mmoja wa wanasiasa wapole
sana. Utulivu na upole uliopitiliza ni vitu viwili tofauti. Utulivu ni
sifa kubwa ya kiongozi lakini upole uliopitiliza ni udhaifu mkubwa kwa
kiongozi.
Mawaziri wengi waliofanya kazi na Profesa
Mwandosya, wananiambia kuwa ni mpole sana na anapoona mambo yamemzidia
huwa na tabia ya kukaa kimya.
Ni mtu wa namna hiyo. Ikiwa unataka kuwa Rais wa
Tanzania, nchi ambayo imeporomoka kiutendaji ndani ya Serikali, hupaswi
kuwa mpole kupita kiasi. Nimetafuta rekodi nzito za kiuongozi
alizozisimamia Profesa Mwandosya na hadi sasa sijazipata. Kwamba
tumkumbuke kwa lipi katika wizara alizopitia nimelikosa.
Hana rekodi nzito kwenye wizara alizopitia,
amewahi kuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wakati wa Mkapa, akawa
Waziri wa Maji na Umwagiliaji wakati wa Kikwete na sasa akiwa ni Waziri
akishughulikia Kazi Maalumu. Sielewi Watanzania watakaa wamkumbuke kwa mabadiliko yapi makubwa aliyoyasimamia katika utumishi wake wa juu serikalini.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Ikiwa CCM itahitaji mgombea mwenye uzoefu mkubwa ndani ya chama
hicho na Serikali, basi Profesa Mwandosya ni mmoja wao. Miaka 40 ya
utendaji ndani ya Serikali na ndani ya CCM kwa nyakati na vipindi
tofauti, vinaweza kumfanya avuke kizingiti hiki.
Naweza kusema kuwa Profesa Mwandosya anaifahamu
vizuri Serikali, nchi na hata wizara na idara zake kwa weledi mzuri na
usio na shaka. Profesa Mwandosya hana makundi na hii ni tabia yake. Ninapozungumzia makundi simaanishi kamati ya kusaidia kwenye kampeni.
CCM kuna makundi na makundi hayo hufanya jambo
lolote hata liwe chafu au hatari kwa watu wengine, maisha yao na ustawi
wao, wao hulifanya tu. Kamati ya kampeni yenyewe hufanya yale tu yaliyo
ndani ya sheria na taratibu. Naambiwa Profesa Mwandosya anaamini anastahili
kuupata urais kwa njia sahihi na za kidemokrasia kuliko hila, fitina na
makundi. Jambo hili nalo ni silaha muhimu kwake.
Jambo la tatu linalombeba ni uadilifu. Huenda
Profesa Mwandosya ni mwana CCM mwingine ambaye kwake ‘kupokea rushwa na
kuiba au kutapanya mali na fedha za umma ni mwiko” (kama zilivyo zile
ahadi za mwana Tanu). Tangu amekuwa waziri kwa miaka 15 sasa, katibu
mkuu wa wizara kwa miaka kadhaa sasa, hakuwahi kuhisiwa, kutuhumiwa au
kufikiriwa kuwa mmoja wa viongozi wala rushwa.
Lakini juhudi za waziwazi za vitendo na mapambano
makubwa yakuzuia rushwa serikalini na katika maeneo aliyopata kuongoza
havikuwahi kuonekana, ndiyo kusema kuwa yeye anachukia rushwa lakini
hajaonyesha kama ana uwezo mkubwa wa kupambana nayo.
Nini kinaweza kumwangusha?
Sababu zilizomwangusha mwaka 2005 zinaweza kuwa
kikwazo cha kwanza katika kuvuka mchujo ndani ya CCM mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa, mwaka 2005 Profesa Mwandosya aliangushwa na Kikwete. Inawezekana mbinu alizotumia kutafuta urais mwaka
2005 akaukosa, ndizo anazotumia kutafuta urais mwaka 2015 katika chama
ambacho watu ambao hupita vikwazo na kuwa wagombea urais huhitaji
mipango fulani kama aliyopitia Kikwete mwaka na hata ile ya kupigiwa
debe na mtu mwenye nguvu kama Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1995.
Ikiwa Profesa Mwandosya hajabadilisha mipango
yake, yaleyale ya 2005 yatamwangusha mara nyingine kwa sababu chama ni
kilekile na washindi wake hupita michujo kwa staili zilezile. Pia, Profesa Mwandosya anaweza kupimwa kutokana na utendaji wake katika wizara alizopitia.
Asipopitishwa (Mpango B)
Hitimisho
Hii ni changamoto kubwa. Suala la utendaji katika
Serikali nadhani litazingatiwa, nimeshaeleza kuwa kwa wana jamii hakuna
rekodi nzito ya mambo ya kujivunia ambayo aliwahi kuyasimamia.
Hivi karibuni, ndiyo kwanza amekuwa waziri, kazi maalumu (kazi zake ni maalumu tu na wananchi hawazijui).
Ikiwa mgombea wa urais ajae atapimwa pia kwa
kigezo cha utendaji wake alipokuwa waziri, Profesa Mwandosya anaweza
kuonekana kama waziri wa kawaida mno na hili litaweza kumwangusha. Nguvu ya makundi yenye fedha ndani ya CCM ni kitisho chake cha tatu.
Kama nilivyoeleza Profesa Mwandosya ni mwadilifu
sana na baadhi ya makundi ya kusaka uongozi ndani ya CCM yanawachukia
watu waadilifu maana wanaweza kuharibu safari ya makundi hayo. Nathubutu kusema kuwa Profesa Mwandosya ni mmoja
wa wana CCM ambao anaweza kuyatia woga makundi hayo na kama ndivyo basi
anaweza kung’olewa kwenye safari hii kirahisi tu.
Asipopitishwa (Mpango B)
Kama ilivyo kwa maprofesa nguli kama yeye, moja ya
mipango ya Profesa Mwandosya inaweza kuwa ni kurudi vyuoni kufundisha.
Sekta ya nishati hususani umeme inahitaji mabadiliko makubwa Tanzania.
Profesa Mwandosya anaweza kuwa na mchango mkubwa kuendelea kuzalisha vijana wapya wengi huko, ikiwa hatagombea urais.
Lakini pili, kwa sababu ya busara, utulivu na upole wake, yeye ni mshauri mzuri. Nadhani anaweza kujihusisha na shughuli za
kidiplomasia na utatuzi wa migogoro ndani na hata nje ya nchi. Tukumbuke
kuwa hadi leo, bado wakulima na wafugaji wanauana, wafanyakazi wanagoma
kila siku, watu wenye uwezo, ujuzi, maarifa na stadi kama Profesa
Mwandosya wanaweza kabisa kutusaidia katika eneo hilo.
Hitimisho
Profesa Mwandosya amekuwa kiongozi ambaye
ametimiza wajibu wake kwa kiasi kikubwa katika Taifa hili, pamoja na
udhaifu wake, amekuwa na mchango mkubwa na anaheshimika mno.
Naamini pamoja na yote niliyoyaeleza juu yake,
anaendelea kuwa mmoja wa watu wanaoonekana kuwa afadhali ndani ya CCM
katika kurithi mikoba ya Rais Kikwete. Namtakia kila la heri katika
kutimiza ndoto yake ya utumishi wa umma kwa vitendo.
CHANZO: MWANACHI
CHANZO: MWANACHI

No comments:
Post a Comment