Social Icons

Pages

Tuesday, May 26, 2015

PROFESA ABDALLAH SAFARI: MAKAMU MWENYEKITI CHADEMA

Profesa Abdallah Safari 
WASIFU Umri: Miaka 64 Elimu: Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria, Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza. Kazi: Wakili wa Kujitegemea na Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara).
Historia yake
Profesa Abdallah Safari ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wakili wa kujitegemea Tanzania. Alizaliwa Juni 3, 1951, katika Kata ya Ngamiani, Tanga (anatimiza miaka 64 Juni).
Baba yake mzazi alikuwa mfanyakazi na mwendeshaji wa mashine kubwa za kazi viwandani na barabarani katika Shamba la Mkonge Mwera. Kwa ujumla, Safari amekulia Mwera japokuwa asili yake ni Nyanguge, Mwanza (Baba yake mzazi ni Msukuma kwa asili). Safari alianza elimu katika Shule ya Msingi Pangani mwaka 1958 – 1966 na kuhitimu darasa la nane, mwaka 1966 – 1967 akaendelea na elimu ya kidato cha kwanza na cha pili katika Shule ya Sekondari Lushoto (siku hizi ni Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa) kisha akahamia shule ya sekondari Karimjee (sasa hivi inaitwa Shule ya Sekondari Usagara) ambako alihitimu kidato cha nne mwaka 1972.
Safari amesoma kidato cha tano na sita akiwa mtahiniwa binafsi (private candidate) na akapata cheti cha kuhitimu masomo ya juu ya sekondari mwaka 1972 katika Shule ya Sekondari Azania kisha akajiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), baada ya miaka michache akisomea sheria na kuhitimu shahada hiyo mwaka 1979.
Profesa Safari alifanya Shahada ya Uzamili ya Sheria hapohapo UDSM na kuhitimu mwaka 1985 na mwaka 1987 akafuzu na kusajiliwa kuwa Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kabla ya kuendelea na masomo ya juu kabisa kwa maana ya Shahada ya Uzamivu aliyosomea katika Chuo Kikuu cha Sussex Uingereza na kuhitimu mwana 1995.

Safari ana historia ndefu ya kufanya kazi nchini.
Mwaka 1972 – 1975 alifanya kazi UDSM katika Taasisi ya Utafiti wa Kiswahili akiwa mtafiti msaidizi, mwaka 1974 – 1976 alifanya kazi katika Shirika la Uchapishaji Tanzania akiwa mhariri, mwaka 1979 – 1986 alifanya kazi katika Wizara ya Sheria akiwa wakili wa Serikali, mwaka 1987 aliajiriwa na Chuo cha Diplomasia (Centre for Foreign Relations – CFR) akiwa ofisa wa uchapishaji na utafiti, mwaka 1988 – 1991 baadaye akapanda na kuwa mhadhiri wa sheria na mwaka 1991 – 1995 kisha mhadhiri mwandamizi.
Kuanzia mwaka 1996 hadi 2001, Safari alipanda na kuwa Mkurugenzi wa Masomo na Programu chuoni hapo na mwaka 2000 alipanda ngazi kitaaluma na kuwa Profesa Mshiriki wa Sheria katika kituo hichohicho.
Lakini pia, Profesa Safari amewahi kushika nyadhifa nyingine ambazo hazikuwa ajira ya moja kwa moja. Kwa mfano, mwaka 1978 – 1979 alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1983 – 1986 aliongoza kitengo cha mafunzo kwa vitendo ya wanasheria katika Wizara ya Sheria, mwaka 1996 – 2000 alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Vitabu Tanzania (Uwavita), mwaka 1999 – 2000 akawa Katibu Mkuu wa Kituo cha Usuluhishi wa Migogoro cha Tanzania.
Msomi huyu ameandika vitabu zaidi ya saba vya kisheria na vingine vinaendelea kuchapishwa, huku pia akiwa mdau mkubwa wa lugha ya Kiswahili akiwa ameandika riwaya na vitabu vya kawaida kwa lugha za Kiingereza na Kiswahili na vingi vinauzwa madukani. Ameoa na ana watoto wawili.

Mbio za ubunge
Profesa Safari hakuwahi kuombea ubunge au kuwa mbunge. Amekuwa mpenzi wa siasa, mfuatiliaji na mwenye kiu kubwa ya kushiriki katika masuala ya kisiasa moja kwa moja tangu alipokuwa UDSM.
Akiwa Mlimani, ndiye aliyekuwa mhariri wa kijarida cha kimapinduzi kilichokuwa kikitolewa hapo kikiwa na picha ya mwenge na kilitokea kupendwa sana. Ameniambia kwamba huo ndiyo wakati ambao alizidi kuipenda siasa, japokuwa aliwahi kuvutiwa na baba yake ambaye alikuwa anashiriki katika harakati za kisiasa.
Alipotoka Uingereza kwa masomo ya shahada ya uzamivu, alikuta joto la mabadiliko limepamba moto Tanzania. Kwa sababu alikuwa anafahamiana vizuri na Profesa Ibrahim Lipumba, aliamua kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF), amenisisitiza kuwa hakufuatwa wala kuombwa, aliamua mwenyewe. Tangu wakati huo alikuwa mshauri wa viongozi wa chama akisaidia masuala muhimu ya kisheria.
Mwaka 2009 aliamua kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea uenyekiti wa CUF akipambana na Profesa Lipumba lakini hakufanikiwa kuchaguliwa. Baadaye alisikika akisema kuwa hakutendewa haki katika uchaguzi huo, akaamua kujiondoa na miaka miwili baadaye akahamia Chadema na kuwa mjumbe wa Kamati Kuu kabla ya kugombea umakamu mwenyekiti wa chama hicho (Bara), mwaka jana na kushinda.

Mbio za urais
Profesa Safari hajatangaza rasmi kuwa atagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini ni mmoja wa viongozi wa Chadema wanaotajwa kuwa wana sifa, uwezo na vigezo vya kwenda Ikulu na wakaipeleka nchi mbele. Kwa sababu lengo la safu hii ni kuwachambua wale wote waliotangaza kugombea urais na wale wanaotajwa, ndiyo maana na yeye yumo.
Nilipomuuliza ikiwa maoni hayo ya wana Chadema anaweza kuyafanyia kazi alisisitiza kuwa muda ukifika tutajua, maana chama chake kina taratibu za kufuata.

Nguvu yake
Kwanza, Profesa Safari ni mwanasheria na msomi aliyebobea kwa kiwango cha juu. Ni moja ya hazina kubwa za utaalamu wa sheria hapa Tanzania. Nakumbuka tulipokuwa naye kwenye Bunge Maalumu la Katiba na tukiwa kwenye vikao vya pembeni, yeye peke yake ndiye aliyekuwa na uwezo mzuri wa kunyoosha hoja za Tundu Lissu ambaye mwanasheria mzuri. Profesa Safari ni mbobezi wa hali ya juu, anaweza kukueleza masuala ya sheria na ukayaelewa kwa lugha rahisi na huenda kwa uwezo huo wa kisheria, anaweza pia kuutumia katika kujenga uongozi imara wa nchi.
Jambo la pili ambalo ni sifa na nguvu ya Profesa Safari ni utulivu na busara za hali ya juu. Moja ya sifa kubwa ya kiongozi wa nchi ni kutokurupuka katika kutoka uamuzi. Huyu si mtu wa kukurupuka, anafanya kila jambo kwa wakati na kwa utulivu mkubwa. Mathalan, alipojiondoa CUF mwaka 2009 alikaa chini kwa takriban miaka miwili kabla ya kujiunga na Chadema. Wanasiasa wengi hudhani kuwa siasa ni biashara, mtu akihama chama hiki leo, kesho amejiunga chama kingine kama biashara ya karanga. Baadhi ya wahadhiri niliozungumza nao pale Chuo cha Diplomasia, wameniambia kuwa wao pia wanamfahamu hivyo. Hili ni jambo muhimu kwa rais yeyote anayetaka kuifikisha mbali nchi yake.
Lakini jambo la tatu ambalo ni muhimu pia, Profesa Safari anapenda na kuthamini sanaa na utamaduni wa mtu mweusi na ni moja ya masuala ambayo ametumia muda wake mwingi kuyakuza. Licha ya kuwa ni msomi wa sheria kwa ngazi ya uzamivu, ni mwandishi wa vitabu vya kawaida vya Kiswahili, kamusi na miswada mbalimbali yenye lengo la kukuza na kuimarisha lugha hiyo, kama alama muhimu ya Taifa. Mara nyingi amekuwa pia akifanya vipindi vya televisheni na redio kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuendelea kukuza na kukitumia Kiswahili. Binafsi namuona kama mwanasheria na mwanazuoni anayekipigania Kiswahili kuliko hata baadhi ya wabobezi wa lugha hiyo wenye shahada za uzamivu. Kwa sababu Taifa letu limeshaondoka katika misingi ya kujali utu, udugu, utamaduni na hadhi ya Mwafrika, huenda watu wenye mtizamo kama wake wanaweza kuwa sahihi kwa Tanzania tuitafutayo.
Mwisho, msomi huyu ni mpiganaji na mpambanaji ambaye anathubutu kwa kadri awezavyo. Mathalan, akiwa mwajiriwa wa Chuo cha Diplomasia kinachomilikiwa na Serikali, alimtetea Profesa Lipumba katika kesi ya uchochezi ya mwaka 2001 ambayo ilitokana na mauaji ya Zanzibar ya Januari 2001. Amenieleza kuwa kitendo kile kilisababisha kufukuzwa kazi mwaka huohuo.
Nilipomuuliza kama hakujua kuwa kitendo kile kingetafsiriwa hivyo na Serikali, alinijulisha kuwa utetezi wa mtu anayeonewa katika hali ngumu kama ile haukuwa unakwepeka na kwamba hata leo haukwepeki. Uthubutu huu wa Profesa Safari, kuwa tayari kupoteza kazi ili kulinda na kuimarisha demokrasia ndani ya nchi unamfanya awe mmoja wa viongozi wa kupigiwa mfano na labda wanaohitajika kuongoza nchi.

Udhaifu wake
Moja ya jambo ninalolitizama kama udhaifu wa Profesa Safari ni kuwa na misimamo mikali katika baadhi ya masuala ya kisiasa anayoyaamini. Tunatambua kuwa kiongozi wa nchi anapaswa kuwa na misimamo imara na inayoeleweka, lakini misimamo hiyo inapokuwa michungu inageuka na kuanza kuwa na madhara.
Kwa mfano, kutokana na kukosekana kwa tume huru ya uchaguzi na mizengwe ambayo chama kinachoongoza dola kimekuwa kikiitenda dhidi ya vyama vya upinzani, Profesa Safari aliwahi kukaririwa akivieleza vyombo vya habari kuwa msimamo wake ni vyama vya upinzani kutoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. Safari aliwahi tena kuhojiwa kwenye kipindi kimoja cha televisheni na akasisitiza kuwa vyama vya upinzani visiishie kulalamika kwa maneno, vinapaswa kususia uchaguzi ili CCM wachaguane wao wenyewe.
Msimamo ule wa Profesa Safari ulinishangaza kwa sababu anajua historia ya Afrika, kwamba kufanya hivyo hapa Afrika ni kuwaneemesha watawala na kuwabinya wananchi wa kawaida. Lakini pia watu niliozungumza nao na waliowahi kufanya naye kazi UDSM, Diplomasia na hata Chadema wanasisitiza sifa hii kwa Profesa Safari, sijui kama leo hii akiulizwa tena kuhusu hali ile anaweza kudai vyama vya upinzani visuse uchaguzi.
Lakini udhaifu wa pili wa Profesa Safari ni kutopenda kufahamika. Wakati mwingine sifa kubwa ya mwanasiasa ni kufahamika kwa watu wanaomzunguka. Yeye si mtu wa kupenda malumbano na mapambano ya maneno kama wanavyoweza kufanya wanasiasa wengi duniani na nadhani hapendi kushambuliwa kwa mambo ambayo anadhani anayajua vizuri. Kwa siasa za Afrika, mwanasiasa imara lazima awe tayari kwa malumbano mazito yanayokaribia hata kushikanisha miili. Aina ya tabia ya kuhitaji siasa ziwe safi na kuzishiriki zikiwa safi, ni jambo ambalo halipo Afrika na kwa hiyo kutokuthubutu kuzifanya kwa nguvu kila inapohitajika na utaratibu kila unapohitajika utaratibu, ni udhaifu wa kutosha.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Moja ya mambo yanayoweza kumfanya apitishwe kuwania urais kupitia Chadema na hata Ukawa ni ikiwa chama hicho ndicho kitaachiwa jukumu la kutoa mgombea urais. Naamini kabisa, yeye ni mmoja wa wana Chadema wachache wenye sifa na uwezo wa kuongoza nchi ikiwa atapewa nafasi hiyo.
Pili, kwa sababu Profesa Safari amefanya kazi Diplomasia kwa miaka mingi amekuwa na uzoefu mkubwa wa kushughulikia masuala ya kimataifa, kwa muktadha huo ana sifa za ziada za kupewa fursa hiyo na Chadema na baadaye Ukawa.
Tatu, yeye ni mmoja wa Watanzania wanaoifahamu vizuri historia ya nchi yetu, amefanya tafiti nyingi kuhusu maendeleo na utamaduni wa nchi katika mikoa mbalimbali na kufanya kazi serikalini kwa muda mrefu. Kwa hivyo nadhani anaifahamu Serikali na namna inavyofanya kazi, lakini pia anawafahamu wafanyakazi na wananchi wa kawaida kiasi cha kutosha kujua nini kiini cha shida na umaskini wao.

Nini kinaweza kumwangusha?
Jambo la kwanza ambalo litamuondoa Profesa Safari katika mtanange wa kusaka urais wa Tanzania ni ikiwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa atapewa jukumu la kupeperusha bendera ya Ukawa kupitia Chadema. Kwa sababu ndani ya vyama huwa kuna taratibu zake. Huenda akajikuta anampisha kwa utaratibu huo.
Jambo jingine linaloweza kumuengua ni ikiwa Ukawa itakubaliana kusimamisha mgombea urais kutoka vyama vya NLD, CUF au NCCR. Hili nalo lina maana kuwa Profesa Safari atalazimika kumuunga mkono mgombea wa moja ya vyama hivyo.
Jambo la tatu ambalo naliona nadra kutokea ni ikiwa Ukawa itapa mgombea kutoka Zanzibar, hili nalo linamhukumu Profesa Safari kwani ni Mbara.
Ndiyo kusema kuwa, kama mambo hayo matatu hayatatokea basi Profesa Safari anaweza kuwa na fursa kubwa ya kutumwa na Ukawa kusaka kura na hatimaye kuwa Rais wa Tanzania ikiwa umoja huo utapewa ridhaa hiyo.

Asipochaguliwa (Mpango B)
Anaweza kuwa na mambo matatu ikiwa hatapita kwenye mchujo wa Ukawa kuwania urais wa Tanzania.
Mpango wa kwanza utakuwa ni kuendelea na shughuli za uwakili kwa kesi za vyama vya Ukawa na nyingine za wananchi kwa ujumla. Tukumbuke kuwa Profesa Safari ni mmoja wa mawakili wazoefu na waliwahi kusimamia kesi kubwa zilizotikisa vyombo vya habari, ikiwamo ile ya kiongozi wa Chadema Jimbo la Kinondoni, Henry Kilewo ya ugaidi kule mkoani Tabora. Akijikita huku, ataendelea kutoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa demokrasia.
Lakini pia anaweza kuendeleza kwa nguvu juhudi za uandishi wa vitabu. Tayari ameshaandika vitabu kadhaa vya sheria na vya taaluma zisizo za sheria ikiwamo vya lugha. Kutogombea urais na labda kutoingia Ikulu kutampa fursa hii adhimu.
Mwisho, Profesa Safari ni msomi mwenye mchango ambao bado unahitajika. Kama hataingia kwenye urais, ana fursa ya kipekee kujipanga kushiriki uchaguzi katika ngazi ya jimbo, akitafuta tiketi ya kuwa mbunge na kuwawakilisha wananchi, kazi ambayo inaweza kumpeleka mbali kisiasa.

Hitimisho
Namtazama Profesa Safari kuwa ni Mtanzania anayependa zaidi kushiriki katika harakati za kidemokrasia na kushauri namna bora ya kuzifanya kuliko kuwa mstari wa mbele akiongoza. Tulipokuwa Bunge Maalumu la Katiba, hata kama viongozi kadhaa wa vyama visivyoongoza dola hawakuwapo, yeye hakuchukua jukumu la kuongoza mijadala na vikao, badala yake alikuwa anapenda kupendekeza vijana wafanye kazi hiyo huku akiwa msikilizaji na mshauri
Namtakia Profesa Safari kila la heri katika kukamilisha mipango muhimu ya kidemokrasia katika uchaguzi wa mwaka huu na chaguzi zijazo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: