Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza katika uzinduzi wa Makao Makuu ya
Jimbo la Mashariki la Kanisa la Moravian Tanzania eneo la Chamazi, Dar
es Salaam jana.
Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini nchini kuitumia mikutano ya
mahubiri kutoa elimu kwa waumini wao na wananchi kwa ujumla kuachana na
imani za kishirikina za kukata viungo na kuwaua walemavu wa ngozi
(albino ).
Pia, amewaomba kutumia mahubiri hayo kutoa elimu juu ya athari za dawa za kulevya kwa waumini wao na Watanzania wote kwa ujumla.
Pinda alitoa wito huo jana wakati wa ibada ya
uzinduzi wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Mashariki uliyofanyika
kwenye makao makuu ya jimbo hilo, Mbagala Chamazi. Jimbo hilo
linajumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Lindi, Mtwara na Pwani.
Akizungumza mbele ya viongozi hao wa dini kutoka
ndani na nje ya nchi, Pinda alisema Tanzania bado inakabiliwa na
changamoto kubwa ya matumizi ya dawa za kulevya hasa kwa vijana.
“Nchi yetu imekuwa ikitajwa kwamba inatumika kwa
kasi katika kusafirisha dawa za kulevya. Ni jana tu tumesikia taarifa
katika vyombo vya habari zikitaja kwamba meli moja ya Tanzania
imekamatwa huko Uingereza ikiwa imebeba tani tatu za dawa za kulevya,”
alisema na kuongeza: “Niwaombe sasa viongozi wa taasisi zote za dini,
tuungane na Serikali kutoa elimu juu ya athari za biashara ya dawa za
kulevya na matumizi yake katika jamii. Ninawasihi tuhakikishe kwenye
mikutano yote tunayoifanya tusimalize bila kutoa elimu kuhusu athari za
dawa za kulevya kwa waumini wetu na umma kwa ujumla.”
Pinda alisema, viongozi wa dini wana jukumu kubwa
la kuwalea zaidi vijana ili wasijiingize kwenye matumizi ya dawa za
kulevya kwa sababu wao ndiyo kundi kubwa zaidi miongoni mwa waumini.
Akizungumzia mauaji ya albino, aliwaomba viongozi wa dini kushirikiana na Serikali kukemea kwa nguvu zote vitendo hivyo.
“Tangu mwaka 2006 kumetokea mauaji ya watu 46
niwaombe tena taasisi zote za dini zitusaidie kuondoa au kubadili imani
hizi za kishirikina miongoni mwa jamii. Ninaamini tukiunganisha nguvu
zetu kwa pamoja dhidi ya fedheha hii tutashinda,” alisisitiza.
Askofu Kiongozi wa kanisa hilo, Dk Issack Nikodemo
aliwataka waumini wa Kikristo kuomba kwa ajili ya amani ya Taifa hasa
katika kipindi hiki ambacho linajiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.
Mwenyekiti wa Jimbo la Kigoma, Charles Katare
alisema kanisa hilo lipo tayari kumchangia Waziri Mkuu fedha za kununua
fomu kugombea urais, kwani wamesikia anataka kuwania nafasi hiyo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment