
Kuna habari za kutatanisha juu ya aliko Rais Pierre
Nkurunziza wa Burundi baada ya kudaiwa kuwa alirejea kwao jana, lakini
kuna taarifa za kiusalama kuwa bado yupo jijini Dar es Salaam. Jana
aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Burundi, Meja Jenerali Godefroid
Niyombare, alitangaza kuwa jeshi la Burundi lilikuwa limetwaa madaraka
wakati Nkurunziza akiwa Dar es Salaam kwenye mkutano wa kusaka suluhu ya
maandamano na machafuko ambayo yameiandama nchi hiyo kwa wiki kadhaa
sasa, wananchi wakipinga uamuzi wa chama cha CNDD cha Nkurunziza kumteua
kugombea tena urais kwenye uchaguzi mkuu mwezi ujao.
Taarifa zilizoifika NIPASHE jana usiku zilisema kuwa Nkurunziza
alikuwa anaelekea Burundi, lakini aligeuza nia baada ya kuelezwa kuwa
jeshi linalomtii lilikuwa limedhibiti hali ya mambo na kwamba Meja
Jenerali Niyombare, alikuwa amekimbia.
Ofisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
wa Tanzania aliliambia NIPASHE kuwa, anachojua ni kwamba viongozi wote
wa EAC wamereja makwao baada ya mkutano. “Sijamuona akirejea hapa hotelini (Serena). Ninachojua ni kwamba
viongozi wote wamekwisha ondoka kureja makwao,” alisema na kuomba
asitajwe kwa kuwa siyo msemaji wa Wizara. Hata hivyo, baadhi ya maofisa
usalama waliozungumza na NIPASHE walisema kuwa Nkurunziza alikuwa Dar es
Salaam na kwamba alikuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Jakaya
Kikwete.
Habari za kiuchunguzi kutoka Hotel ya Serena zilisema maofisa wengi
waliokuwa kwenye kwenye msafara wa Rais Nkurunziza walikuwa maeneo ya
hoteli hiyo kama vile kiongozi angerejea maeneo hayo. Jeshi la Burundi limetangaza kuiangusha Serikali ya Rais Pierre
Nkurunziza. Hata hivyo, Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), wamepinga mapinduzi hayo na kuwataka waliohusika
kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kisheria.
Mapinduzi hayo yamefuatia wiki kadhaa za machafuko ya kisiasa
nchini humo yaliyosababishwa na hatua ya kiongozi huyo kutangaza
kugombea urais kwa muhula wa tatu, huku vyama vya upinzani vikiitisha
maandamano yasiyo na ukomo katika mji mkuu, Bujumbura.
Rais Nkurunziza alipinduliwa jana akiwa jijini Dar es Salaam,
Tanzania kuhudhuria mkutano wa Wakuu wa EAC kujadili hali ya usalama
nchini Burundi. Mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Burundi, Meja Jenerali
Godefroid Niyombare, ndiye aliyetangaza kumpindua Rais Nkurunziza.
Hata hivyo, kwa mujibu wa gazeti la The Guardian la Uingereza,
Mshauri wa Rais Nkuruzinza, Willy Niyamitwe, alikana kutokea kwa
mapinduzi hayo, akiita taarifa ya Jenerali huyo kuwa ni ya utani. Shirika la Habari la Iran (IRIB) lilimkariri Jenerali Niyombare
akitangaza taarifa hizo kupitia redio binafsi ya Isangiro jijini
Bujumbura, akisema: “Kuanzia sasa, Pierre Nkurunziza, si Rais tena wa Burundi, serikali
imevunjwa, makatibu wa kudumu wa mawaziri wataendesha masuala ya nchi
hadi tangazo jingine litakapotolewa.”
Tangazo la Jeja Jenerali Niyombare lilikuja baada ya Jeshi la
Burundi kuzizingira ofisi za Redio ya Taifa katika Jiji la Bujumbura.
Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian, ofisa huyo Mkuu wa zamani wa
Mashushu wa nchi hiyo, alichukua hatua hiyo kutokana Rais Nkurunziza
kukiuka katiba ya nchi hiyo kwa kitendo chake cha kuwania muhula wa tatu
wa urais. Alitoa tangazo hilo kwa waandishi wa habari kwenye kambi moja ya
jeshi iliyoko jijini Bujumbura, wakati Rais Nkurunziza akiwa nje ya
nchi.
Jenerali Niyombare ambaye ni Balozi wa zamani wa Taifa hilo nchini
Kenya, alikuwa amezungukwa na baadhi ya maofisa waandamizi wa Jeshi na
Polisi, akiwamo waziri wa zamani wa ulinzi. Aidha, mbali na sababu ya
kukiuka Katiba ya Burundi, Jenerali Niyombare alisema alimpindua Rais
Nkurunziza kutokana na kukaidi wito wa jumuiya ya kimataifa, uliomtaka
aheshimu katiba na makubaliano ya mkataba wa amani wa Arusha.
Aidha, kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),
Jenerali Niyombare alisema Kamati ya Taifa ya Ukombozi ilikuwa imeundwa,
inayojumuisha majenerali wengine watano wa Jeshi na Polisi. Alisema kupitia Redio ya Taifa kuwa, kazi ya chombo hicho ni
kurejesha umoja wa kitaifa na kuanzisha upya mchakato wa uchaguzi katika
mazingira na hali ya amani.
Awali, taarifa kutoka Burundi zilisema kuwa Polisi walilazimika
kufyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji waliokuwa
wakielekea kwenye makao ya Rais, jijini Bujumbura.
Mwandishi wa BBC aliyoko jijini humo, Maud Jullien, alisema mamia
ya waandamanaji waliandamana hadi umbali wa takribani kilomita moja
kutoka kwa kasri la Rais, walipovamiwa na maofisa wa usalama. Polisi
walifyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi kwa waandamanaji hao
waliokaribia makao ya rais.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa waandamanaji kukaribia kasri la
rais tangu maelfu ya watu walipoanza kuandamana kupinga hatua ya Rais
Nkurunziza kuwania kuingoza nchi hiyo kwa awamu ya tatu, kinyume cha
mwafaka wa amani wa Arusha.
WAKUU EAC WAPINGA
Jijini Dar es Salaam, wakuu wa EAC waliokuwa wakikutana kujadili
hali ya Burundi wakati mapinduzi hayo yanatangazwa, walitoa tamko
wakisema hawakubaliani na hatua hiyo na kuwataka waliofanya mapinduzi
hayo wairudishe nchi hiyo katika utawala wa kisheria.
Wakuu hao waliokutana ni Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, wa
Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa EAC; Rais wa Uganda, Yoweri
Mseveni; Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Rwanda, Paul Kagame. Wengine ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa;
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Nkosazana Dlamini-Zuma;
Katibu Mkuu EAC, Dk. Dk. Richard Sezibera.
Rais Kikwete alizungumza na waandishi wa habari jana jioni Ikulu na
kutoa maazimio yaliyofikiwa na viongozi hao baada ya kumalizika kwa
mkutano huo.
MAAZIMIO
Alisema viongozi wakuu wa EAC hawakubaliani na hali iliyotokea nchini Burundi. Alisema kutokana na hali hiyo, wametoa maazimio matatu ambayo ni
kuwataka waliofanya mapinduzi warudishe nchi katika utawala wa kisheria.
Azimio lingine ni uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike mwezi ujao nchini
Burundi, usifanyike hadi hapo hali ya amani itakaporejeshwa nchini humo.
Rais Kikwete alisema hali ya amani itakapokuwa shwari Burundi, uchaguzi
utakapofanyika ufuate utaratibu wa kisheria na pia uzingatie
makubaliano ya mwaka 2005 yaliyofikiwa Arusha.
Aliongeza kuwa viongozi hao wakuu wa nchi watakutana tena Dar es
Salaam baada ya wiki mbili ili kuangalia kama hali ya amani imerejea
Burundi.
HALI ILIVYOKUWA
Wakati viongozi hao wakiendelea na mkutano, baada ya kuwapo taarifa
kwamba Jeshi la Burundi limeipindua nchi hiyo, watu waliokuwapo katika
viwanja vya Ikulu Dar es Salaam walianza kujikusanya katika makundi
kujadiliana hali hiyo.
Ilipofika saa 10:05 jioni, Rais Kikwete alitoka nje ya ukumbi
kulikokuwa kunafanyika mkutano huo na baada ya dakika tatu alirejea tena
huku akiwasihi waandishi wasimuulize jambo lolote kuhusiana na mambo
yaliyokuwa yakijadiliwa.
Wakati viongozi hao wakiendelea na mjadala, Rais Nkurunzinza
ambaye alikuwapo Dar es Salaam hadi jioni, hakuwa ameingia katika
mkutano huo hadi unamalizika. Kabla ya kumalizika kwa mkutano huo, Rais Museveni aliondoka
ukumbi saa 11:03 jioni. Mkutano huo ulianza saa 6:00 mchana na
kumalizika 11:20 jioni.
ULINZI WAIMARISHWA
Ulinzi katika hoteli ya Serena alikokuwa Rais Nkurunziza ulikuwa wa
‘kutisha’ ukihusisha askari polisi wenye silaha za moto pamoja na
Usalama wa Taifa uliotanda kila kona ya hoteli. Askari walikuwa na silaha yakiwamo mabomu ya kurusha. Majira ya saa
10:00 jioni, aliwasili Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Rashid
Othman, ambaye taarifa zinasema kuwa alikwenda kuzungumza na Nkurunziza.
Baada ya takribani saa moja, Rais Nkurunziza alitoka nje chini ya
ulinzi mkali wa maofisa Usalama wa Taifa, akiongozwa na Othman na
kupanda moja kwa moja kwenye gari aina ya Land Cruiser lililokuwa na
Bendera ya Burundi ambalo pia liliandikwa Burundi kwenye kibao cha
namba.
Taarifa zinaeleza kuwa Rais huyo alielekea nchini kwake kwa kile kilichoelezwa ni ‘kukwama’ kwa mapinduzi. Waandishi wa habari walizuiwa kuzungumza naye wala kumpiga picha.
AREJEA BURUNDI
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye jana jioni na kunukuliwa
na BBC, zilieleza jana jioni kuwa, Rais Nkuruziza aliondoka na ndege ya
Rais wa Burundi kurudi nchini humo.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment