Wazee wanaoishi katika mazingira magumu jijini Mwanza wakiomba msaada
kutoka kwa wasamaria wema kandokando ya mzunguko wa Mnara wa Mashujaa.
Si kila ombaomba aliye katika mitaa ya jijini Dar es Salaam au majiji na miji mingine nchini anatoka mkoani Dodoma. Hata hivyo, ipo dhana katika fikra za walio wengi
kuwa daima ombaomba hutokea mkoani Dodoma, jambo ambalo limedhihirika
kuwa halina ukweli, ingawa ni ukweli usiopingika kuwa wengi hutoka
katika baadhi ya vijiji vilivyo kwenye mwambao wa reli ya kati mkoani
humo.
Sababu za hali hiyo zinatajwa kuwa ni za
kimazingira ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa wananchi wa maaneo hayo
kuwa maskini, lakini nyingine inaelezwa ni hulka ya watu wengi katika
maeneo hayo kutopenda kufanya kazi ngumu hasa kilimo hivyo kuwa
ombaomba.
Makala haya hayalengi kuwazungumzia ombaomba, bali
maisha na changamoto za Hamisi Peter (44), mlemavu wa viungo ambaye
amekimbiwa na mkewe baada ya kupata ajali na kuthibitika kwamba atakuwa
akiishi maisha ya ulemavu.
Pia lengo si kuelezea tukio la Peter kukimbiwa na mkewe, bali maelezo yake kwamba hapendi na anachukia maisha ya kuombaomba. “Mimi sipendi maisha haya ya kuombaomba, mwili
wangu unanilazimisha niishi hivi. Napenda nitoke katika maisha haya ya
aibu na manyanyaso makubwa. Nafsi yangu haifurahii maisha haya
yasiyokuwa na heshima, lakini nitafanya nini wakati watoto wawili
wananitazama mimi na mama yangu ambaye ni kikogwe pia ananitazama mimi?
Sina namna zaidi ya kuomba,” anasema Peter na kusisitiza:
“Ndiyo hivyo tena, ‘roho ipo radhi, lakini mwili
ni dhaifu’, sina budi kuishi kwa kuombaomba ili kunusuru maisha yangu na
watoto wawili waliotelekezewa na mke wangu.”
Anasema hawezi kuusahau mwaka 2011 kwani ndiyo uliobadili maisha yake na kuyaweka katika mitazamo mitatu. “Nilijishughulisha na kazi halali za kuniingizia
kipato, lakini sasa ni ombaomba, pili; mwaka 2011 uliweka alama ya
mwisho wa uhusiano wa ndoa kati yangu na mke wangu, tatu; ni mwaka
uliogharimu viungo vyangu na sasa wananiita ‘Hamisi mlemavu,” anasema.
Anasema kuwa mwaka huo akiwa mkoani Morogoro
akifanya kazi ya kuuza nyama katika bucha lililomilikiwa na Hassan Idd,
siku moja alfajiri wakati wakienda machinjioni, gari walilotumia
lilipata ajali iliyogharimu maisha ya wenzake wawili, huku yeye
akiachiwa ulemavu.
Anasimulia kuwa baada ya ajali hiyo, alijikuta
akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ambako kutokana na
hali yake ilivyokuwa, wataalamu katika hospitali hiyo walishauri
apelekwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), KCMC au Hospitali ya
Mkoa ya Dodoma (General Hospital) kwani huko kuna wataalamu wa mifupa
waliobobea.
Kutokana na ushauri huo, Peter anasema aliamua
kwenda Hospitali ya Dodoma kwa kuwa ni jirani na nyumbani kwao akiamini
ingekuwa rahisi kupata hata huduma nyingine. Hakika, akiwa hospitalini
hapo alihudumiwa ipasavyo akapona, ingawa amebaki akiwa mlemavu wa
viungo kutokana na nyoga na mguu wa kulia kuthibitika kuwa viliathirika
zaidi. Anasema alipopata ajali, mkewe na watoto wake wawili walikuwa wamerudi kijiji kwa ajili ya msimu wa kilimo.
Hakuonana na mkewe tangu alipopata ajali hadi alipopelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. “Inaweza kuwa ilikuwa ni mkosi vile, mke wangu
tangu kupata ajali tulikuwa hatujaonana kwa sababu zinazofahamika
kabisa; alikuwa kijijini na watoto. Nilipoletwa hapa hospitali Dodoma
alikuja kuniona. Nilifurahi kuonana naye nikiwa hai,” anaeleza Peter
huku akianza kulia, kisha anaendelea:
“Nilifikiri kuwa alikuja kuniona tu, kumbe ndiyo
alikuwa ananiaga, maana baada ya kutoka tu hospitali alikwenda kukusanya
alivyoona vinamfaa, huyoo, akatokomea alipojua mwenyewe na mimi na
watoto hatujamuona tena. Mwaka wa nne sasa. Nasikia yuko Dar es Salaam,
ila sina uhakika.”
Anaeleza kuwa taarifa kuwa mkewe amemkimbia alizipata akiwa hospitali na hakuwa na la kufanya. “Nilijitazama, nikakumbuka siku ile tuliyofunga
ndoa Kanisa la Katoliki Parokia ya Kigwe. Duh! Yaani, inauma. Kumbe vile
viapo vya ndoa ni bure kwake. Aliniahidi tutakuwa naye kwa shida na
raha, mbona sasa amenikimbia nikiwa katika hali hii? Naomba akumbuke
kiapo kile, arudi tulee watoto,” anasema Peter.
Anasema kitendo cha mkewe kumkimbia ndicho
kinachomsababishia jeraha la ulemavu wake kuwa kubwa na kwamba mara
nyingi akijitazama haamini kama kweli amemkimbia. “Yaani mke wangu tumeishi naye kwa taabu pale
Morogoro mimi nikiwa nafanya vibarua vya kulisha ng’ombe kwa malipo ya
Sh30,000 kwa mwezi kabla ya kupata kazi ya bucha ambayo nilikuwa
nikilipwa Sh10,000 kwa siku, alivumilia maisha yakasonga. Sasa kwa nini
ulemavu wangu umkwaze?
Mimi ni yuleyule, nafsi yangu haijabadilika zaidi
ya kuwa mlemavu. Aje tu, anawasababishia watoto wake ukiwa,” anaeleza
kwa masikitiko. Peter anasisitiza kuwa hapendi kuwa ombaomba, lakini atatokaje katika kadhia hiyo yenye adha ilhali mwili wake ni dhaifu?
Mwenyewe anajibu akisema kwamba baada ya
kujitathmini, anaamini ulemavu wake bado si kikwazo, anaweza kufanya
biashara na hata kujishughulisha na kazi za kilimo endapo atapata viungo
bandia.
“Naomba wasamaria wanisaidie kupata viungo bandia ili niweze kufanya biashara, hata kulima kuliko kuombaomba,” anasema Peter.
Peter alizaliwa miaka 44 iliyopita katika Kijiji cha Nkhurugano, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma. Alisoma katika Shule ya Msingi Nkhurugano na kuhitimu mwaka 1989 na hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari. Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, alianza
kujishughulisha na kilimo hadi alipofunga ndoa mwaka 2002 na kupata
watoto wawili Neema (12) na Deus (7).
Hata hivyo, kutokana na maisha ya kilimo cha jembe
la mkono kwenye sehemu ambayo ekologia yake siyo rafiki kwa kilimo,
aliamua kubadili maisha kwa kwenda mkoani Morogoro.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment