Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akizungumza bungeni wakati wa
kupitisha Muswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki wa Mwaka 2014 na
Sheria wa Makosa ya Mtandao wa Mwaka 2015 mjini Dodoma, juzi usiku.
Mwanasheria Mkuu wa
Chadema, Tundu Lissu amesema Kura ya Maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba
Inayopendekezwa haitaendeshwa bila kuifanyia marekebisho sheria
inayoongoza mchakato huo.
Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki,
alisema hayo jana wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani ya
makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano)
mjini hapa.
Kura ya Maoni ilipangwa kufanyika Aprili 30 lakini
ikaahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kasi ndogo ya
uandikishaji wapigakura, lakini Lissu aliliambia Bunge jana baada ya
kuahirishwa kuwa hakuna uwezekano wa kura hiyo kupigwa bila ya kufanyia
marekebisho Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013.
Vikao vinavyoendelea mjini Dodoma ni vya mwisho
kwa Bunge la 10 lililochaguliwa mwaka 2010 na iwapo Serikali
haitawasilisha muswada wa marekebisho ya sheria hiyo, Kura ya Maoni
haitafanyika mwaka huu, kwa mujibu wa Lissu.
“Kwa kifupi Mheshimiwa Spika, hakuna uwezekano
kisheria wa kurudia tena hatua zozote muhimu ambazo zilikwishachukuliwa
kwa ajili ya kufanyika kwa Kura ya Maoni iliyokuwa imepangwa Aprili 30,
2015,” alisema Lissu.
“Mpaka sasa Serikali hii ya CCM haijawasilisha
muswada wowote wa marekebisho ya sheria hiyo ili kuwezesha kufanyika kwa
kura ya maoni siku za usoni.
“Kama ilivyokuwa kwa ahadi ya Kura ya Maoni ya
Aprili 30, Serikali hii ya CCM inadanganya Watanzania kuwa kutakuwa na
Kura ya Maoni wakati kila mwenye akili timamu anajua hilo haliwezekani
bila kwanza kuwa na mazingira wezeshi ya kisheria.”
Akiwasilisha hotuba ya upinzani, Lissu alisema
kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa, haiwezekani kuahirishwa wala
kuongezewa muda kama ilivyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na
Serikali. Lissu alisema kitendo cha kutofuata muda uliowekwa katika sheria hiyo, kinaiondolea sheria hiyo uhalali wa kuendelea kutumika.
Lissu, ambaye ni wakili wa kujitegemea, alisema
ndani ya siku 14 tangu tarehe ya kupokea Katiba Inayopendekezwa, Rais
alitakiwa kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, kuielekeza Tume ya
Uchaguzi kwa amri iliyotangazwa katika Gazeti la Serikali kuendesha Kura
ya Maoni.
Alisema amri ya Kura ya Maoni inatakiwa kufafanua kipindi cha kampeni na kipindi ambacho kura hiyo inatakiwa kufanyika.
“Rais Kikwete alikwishatoa amri kwa mujibu wa
kifungu cha 4 cha Sheria ya Kura ya Maoni, lakini hana mamlaka yoyote,
kwa mujibu wa sheria hii, ya kutengua amri yake au kutoa amri mpya ili
kuwezesha kura ya maoni kufanyika kwa tarehe nyingine tofauti na tarehe
iliyotangazwa kwenye amri ya kwanza,” alisema.
Kauli ya Waziri
Alisema ndani ya siku saba baada ya kuchapishwa kwa Katiba
Inayopendekezwa, NEC inatakiwa kuandaa swali la Kura ya Maoni na
kulichapisha katika gazeti la Serikali. “Na ndani ya siku 14 baada ya kuchapisha swali
hilo, Tume inatakiwa kutoa taarifa ya kufanyika kwa Kura ya Maoni,
itakayoeleza kipindi cha kuhamasisha na kuelimisha umma juu ya kura hiyo
na siku ya kura ya maoni,” alisema.
Alisisitiza kuwa kila msimamizi wa kura anatakiwa
ndani ya siku 21 baada ya kuchapishwa kwa taarifa ya NEC, kuwajulisha
wananchi katika jimbo lake la uchaguzi kuhusu utaratibu wa kufanyika kwa
Kura ya Maoni.
Mbunge huyo aliongeza kuwa Tume inatakiwa kutoa
elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa muda wa siku 60 tangu
Katiba Inayopendekezwa ilipochapishwa. “Tume ilishaandaa na kuchapisha swali la kura ya
maoni na ilikwishatoa taarifa ya kura ya maoni na ratiba yake nzima na
haina mamlaka yoyote, kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, kutengua
taarifa yake na kutoa taarifa nyingine, au kuweka ratiba nyingine badala
ya ratiba iliyokwishatolewa.
“Vile vile, Tume haiwezi kujiongezea muda wa kutoa
elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa au kujipa muda mwingine
kwa vile muda uliowekwa na sheria haukutumika ipasavyo.”
Alisema wasimamizi wa Kura ya Maoni hawana mamlaka
yoyote kisheria ya kuongeza au kuongezewa muda wa kutoa taarifa kwa
umma chini ya kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Kura ya Maoni.
Lissu pia aligusia suala la Muungano, akisema
Zanzibar haipati mgawo wa fedha za nje kwa ajili ya miradi ya maendeleo
zikijumuisha misaada na mikopo, kwa kuwa mwaka 2013/14 zilikuwa Sh2,292
bilioni, lakini zilikuwa kwa miradi ya maendeleo ya Tanzania Bara.
Kauli ya Waziri
Akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais
Mazingira na Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Samia Suluhu Hassan
aligusia jinsi Serikali ya Awamu ya Nne ilivyodumisha Muungano na
kulinda mazingira. Bajeti ya wizara hiyo ni Sh43 bilioni.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment