
Ni dhahiri sasa kuwa
hatua ya vikao vya juu vya CCM kuwafungulia makada wake waliokuwa
wamefungiwa kwa kuanza kampeni mapema na kutangaza tarehe za kuanza
kuchukua fomu, vimechochea harakati za kusaka urais na kuongeza urefu wa
foleni ya wanaotaka kuelekea Ikulu kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yamejitokeza ndani ya siku nne baada ya
uamuzi huo wa CCM kutangazwa mjini Dodoma na kuwafanya makada wake,
kuanza kujitokeza hadharani wakiweka bayana tarehe za kutangaza nia
hiyo.
WanaCCM waliojitokeza ni mtoto wa Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, Makongoro Nyerere, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa
Sospeter Muhongo ambao kwa nyakati tofauti wamethibitisha kuwa
wanatangaza nia hiyo wiki ijayo.
Wakati Makongoro akisema sasa anajisikia kuomba
kazi ya urais na anatarajia kutangaza nia hiyo kabla ya Juni 3, Profesa
Muhongo ameahidi kufanya hivyo kati ya Mei 31 na Juni 3, huku Profesa
Mwandosya akisema ataweka wazi kila kitu Jumatatu ijayo. Tarehe ya
kuanza kuchukua fomu kwa chama hicho ni Juni 3 na kurejesha ni Julai 2.
Kuingia ulingoni kwa mada hao ambao kwa muda mrefu
hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, kunaongeza orodha ya makada
waliokwishajipanga kwenye foleni hiyo akiwamo Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa anayetarajia kutangaza kile anachoita ‘safari ya
matumaini’ Jumamosi mjini Arusha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe aliyetangaza nia hiyo juzi, akifafanua kuwa
atafanya hivyo hivi karibuni huko Mtama, Lindi alikozaliwa.
Pia wamo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Stephen Wasira aliyekwishaeleza nia hiyo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba aliyejiuzulu unaibu Katibu Mkuu wa CCM Jumapili ili aweze
kuwania urais bila mgongano wa masilahi katika vikao vya chama hicho,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Dk
Hamis Kigwangalla, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba na Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU) katika
Umoja wa Mataifa (UN), Amina Salum Ali. Katika mlolongo huo wapo makada waliokuwa
wanatajwa muda mrefu ambao wanasubiriwa kuweka bayana ni hiyo ambao ni
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Kauli ya Makongoro
Akiwa mjini Mbeya juzi, mbunge huyo wa Afrika
Mashariki alisema: “Najisikia kuomba kazi ya kuwaongoza Watanzania
katika ngazi ya juu ya uongozi, kwani uwezo ninao, afya na muda wa
kufanya hivyo vinaniruhusu.”
Makongoro alisema hayo wakati akitoa shukrani kwa
viongozi wa dini baada ya kumkabidhi Tuzo ya Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere kwa niaba ya familia, ikiwa ni ishara ya kuenzi na kukumbuka
kazi alizofanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake.
Awali, viongozi wa dini na machifu walioshiriki
hafla hiyo, walimtaka Makongoro ‘kuvunja tetesi’ zinazosambazwa kupitia
vyombo vya habari juu yake kuhusu kuwania urais na kumtaka atamke wazi
juzi hilo kwa kuwa wako tayari kumsaidia katika harakati zake.
Kiongozi wa machifu wa Busokelo, Prince Mwaihojo
alisema wananchi wa Mbeya wana imani kubwa na familia ya Mwalimu Nyerere
kwa kuwa mwasisi huyo wa Taifa alikuwa akitangaza mambo mazito akiwa
mkoani hapo.
Profesa Mwandosya
Mwaihojo alisema wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere
alizungumza jinsi rushwa inavyoitafuna nchi na umuhimu wa michezo kwa
nyakati tofauti. “Wazee wanasema watakusaidia katika harakati zako
za kisiasa na mambo mengine, lakini ni muda mrefu wamekuwa wakisikia tu
kwenye vyombo vya habari, hivyo wanataka uweke wazi suala hili ukiwa
mkoani Mbeya, kama alivyofanya Mwalimu Nyerere kuzungumzia masuala nyeti
akiwa hapa (Mbeya),” alisema Mwaihojo.
Askofu wa Makanisa ya Pentecostal Assemblies of
God mkoani Mbeya, Damiano Kongoro alisema Taifa linatakiwa kuongozwa na
mtu anayejua kwamba nchi ni maskini ndani ya utajiri uliotukuka ambaye
atawaondoa Watanzania katika hali hiyo, mwenye kufuata maadili na
misingi aliyoiacha Mwalimu Nyerere.
Hata hivyo, Makongoro aliwaambia viongozi hao
kwamba asingeweza kutamka chochote juu ya minong’ono hiyo katika hafla
inayomhusu baba yake, Mwalimu Nyerere.
“Nimewasikia wazee wangu waliofanya kazi na
Mwalimu Nyerere na viongozi wa dini hapa, mlichosema nimewaelewa ila
hapa siyo mahala sahihi pa kuzungumzia suala hili, tumekuja kupokea
nishani ya kumuenzi Mwalimu Nyerere. “Ila najisikia kuomba kura za kazi za kuwaongoza
wananchi kwani nina afya nzuri, uwezo ninao na ni muda mwafaka kabisa
lakini siku mbili kabla ya tarehe 3 Juni nitakutana na wanahabari
kulizungumzia jambo hili,” alisema Makongoro.
Alisema anakumbuka baba yake alivyokataa kumbeba
mwaka 1995 wakati akitaka kugombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini na
kwamba ndiyo maana anasita kutamka mambo makubwa kwenye hafla hiyo.
“Baada ya kuona ile ngoma kwenye CCM imedunda,
nikasema ngoja nijaribu kumweleza baba nigombee kupitia chama cha
upinzani, hapo nilitegemea kupata jibu tofauti, lakini akaniuliza
nagombea kwa chama kipi, nikamwambia NCCR-Mageuzi, akasema hapo safi na
kunisisitizia nikiingia huko nikamsaidie sana (Augustine) Mrema,”
alisema Makongoro. Mrema, alikuwa mwenyekiti wa chama hicho wakati huo.
Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Sabina
Gereja akizungumza katika hafla hiyo, alisema umefika wakati wa
Watanzania kuienzi familia ya Nyerere ambayo iliishi katika maisha ya
kawaida enzi za uongozi wake. Alisema kuna haja kwa Serikali nayo kuhakikisha inaendelea kuwaenzi wanafamilia hiyo wanaoongozwa na Mama Maria Nyerere.
Profesa Mwandosya
Jana, Profesa Mwandosya alisema amepanga
kuzungumza na vyombo vya habari, Juni Mosi jijini Mbeya, pamoja na mambo
mengine, juu ya mbio zake za urais. Pamoja na Profesa Mwandosya kutoingia kwa undani kuhusu suala
hilo, alipoulizwa iwapo siku hiyo atatangaza nia, alisema mambo hayo na
mengine yote yatajulikana siku hiyo.
Profesa Muhongo
CHANZO: MWANANCHI
Mmoja wa watu walio katika kamati ya maandalizi
ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema upo uwezekano waziri
huyo akatamka suala la kuwania urais.
“Hadi sasa maandalizi ni mazuri, tunatarajia
kufanya shughuli hii na Profesa Mwandosya atazungumza na wananchi,
waandishi wa habari na wanachama wa CCM na kueleza mipango yake na
vipaumbele iwapo atafanikiwa katika safari yake hiyo,” alisema.
Profesa Muhongo
Hatimaye minong’ono imekuwa kweli baada ya Profesa
Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, kujitosa katika
kinyang’anyiro hicho akipanga kutangaza nia kati ya Mei 31 na Juni, 3.
Profesa Muhongo aliliambia gazeti hili kwa ujumbe
mfupi wa simu ya mkononi kuwa atatoa tamko lake juu ya “Tanzania ijayo
(2015 - 2025)” kabla ya kuchukua fomu na kuwaomba makada wa CCM
kujitokeza kumdhamini muda ukiwadia.
Kabla ya uthibitisho huo, kulikuwa na taarifa
zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii ya Whatsapp, Twitter na
Facebook, kuwa mtaalamu huyo wa jiolojia ataweka bayana safari yake
mpya ya kutafuta cheo cha juu zaidi nchini.
Alipotakiwa kuthibitisha ukweli wa ujumbe huo, alijibu kifupi: “Ndiyo. Ni kweli. SM.” Hata hivyo, Profesa Muhongo hakuweka bayana eneo atakalotolea tamko hilo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment