
Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Said Miraaj.
Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC),
kimesema kitendo cha Ikulu kusafisha baadhi ya Mawaziri waliohusika
katika dhambi ya kuteswa na kunyanyasa wananchi katika operesheni
tokomeza ni kuwafedhehesha wananchi na ni aibu kwa Taifa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Said Miraaj, wakati akihutubia wananchi wa Tanga Mjini. Alisema vitendo walivyofanyiwa wananchi katika operesheni hizo ni
vya kinyama na vilionekana kukusudiwa, hivyo mawaziri walitakiwa
kuwajibika moja kwa moja.
Miraaj alisema maamuzi hayo yamewasaliti wananchi na kuliomba Bunge
kuingilia kati suala hilo kwa maslahi ya wananchi ili wote waliohusika
wachukuliwe hatua. “Kitendo cha serikali inataka kukifanya cha kuwasafisha baadhi ya
mawaziri wake waliohusika katika vitendo vya kuwanyanyasa na kuwatesa
wananchi ni cha aibu na cha kufedhehesha," alisema Miraaj.
Aliongeza: "Tayari wananchi hawana imani na viongozi hao,
walishindwa kutimiza wajibu wao na kuacha wananchi wakateswa na
kunyanyasika na kufanyiwa vitendo vya aibu, kwa kosa hilo walipaswa
kuwajibishwa, hatukutegemea serikali kufanya hivi walivyofanya, naliomba
Bunge lisilifumbie macho jambo hili."
Miraaj alimuomba Rais Jakaya Kikwete kutumia hekima na busara
kufanya maamuzi katika hilo ili aepuke kuacha doa katika kipindi kifupi
cha uongozi wake kilichobaki. "Muda wa uongozi wa rais Kikwete umebaki mfupi, Mungu akitujalia
Oktoba mwaka huu anamaliza, hivyo ni vema asitie doa uongozi wake
kupitia hawa mawaziri wake, atumie hekima na busara kufanya maamuzi ili
hata kama akiondoka wananchi wasiwe na kinyongo naye," alisema Miraaj.
Mawaziri waliosafishwa ni Dk. Emmanuel Nchimbi aliyekuwa Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi; Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii);
Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT) na Mathayo David Mathayo (Mifugo na
Uvuvi).
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment