Kiongozi mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto
Kabwe, amesema tatizo la elimu, afya na miundo mbinu ya
barabara nchini limekuwa sugu na kuongeza kundi kubwa la vijana wasio na
ajira.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mkendo,
Musoma mjini, Zitto, alisema matatizo yanayoikabili taifa ni mengi na
kuwakosesha ajira vijana wanaoteseka baada ya serikali kuamua
kubinafsisha viwanda nchi nzima. “Wanasiasa tunatakiwa kutafuta ufumbuzi wa matatizo waliyonayo
wananchi hususani vijana kwa kukosa ajira, tatizo ambalo kwetu ni bomu
kwa taifa…rasilimali za nchi zinanufaisha wachache, ufisadi na rushwa
umekuwa changamoto kubwa,” alisema Zitto.
Alisema: “Watoto hawana elimu bora, huduma za afya haziridhishi na
miundombinu ya barabara imekuwa tatizo kubwa nchini, tuzungumzie hali
hiyo badala ya kunyoosheana vidole.” Katika hatua nyingine, Zitto alisema hawezi kutumika na Chama Cha
Mapinduzi (CCM), bali mambo yanayozungumzwa kuhusu chama hicho ni
upotoshaji mkubwa.
“Sishangazwi na kauli hizo kwani hata CUF waliitwa ‘mashoga’ baada
ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, Mbatia (James) naye
aliitwa CCM B baada ya kuteuliwa ubunge na Rais Jakaya Kikwete na Mabere
Marando akaitwa pandikizwi, baada ya kugombana na Mrema,” alisema
Zitto.
Alisema Tanzania ni nchi tajiri, lakini wananchi wake ni maskini
hali inayotokana na viongozi wa nchi kutojali maisha ya wananchi kwa
kutoweka utaratibu wa kuhakikisha kila mmoja anaishi katika hali nzuri
ya maisha kulingana na uchumi unaozalishwa nchini.
Naye mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Ngwira, alisema nia na
madhumuni ya chama hicho ni kutetea maslahi ya wananchi kwa kufuata
mafundisho ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyoyataja
ni undugu, uzalendo na uwajibikaji.
Ngwira alisema endapo haki itatendeka katika utendaji wa serikali
kulingana na hali halisi ya utajiri wa nchi, ni vyema kila Mtanzania
akaanza kulipwa mafao ya uzeeni kutoka katika mifuko ya hifadhi ya jamii
kwa kuwahamasisha wananchi kuchangia gharama kidogo kulingana na hali
halisi ya maisha anayoishi.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Shabani Mambo, alisema
siasa ni maisha endelevu na kuwataka wananchi kutochezea siasa kwa
kudanganywa na kwamba ikiwa watachezea siasa watakuwa wamechezea maisha.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment