
Mradi wa mabasi yaendayo kasi
Wakati Watanzania hasa wakazi wa jiji la Dar es
Salaam wakisubiri kwa hamu kuanza kwa mradi wa mabasi yaendayo kasi,
kizungumkuti kimewakumba wadau wa mradi huo kuhusu nani apewe zabuni ya
kuusimamia.
Kukiwa kumebakia karibu mwezi mmoja na nusu kabla
ya kuanza kwake mwezi Juni, wadau wanahoji nani anapaswa kuuendesha
mradi huo wa kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki kati ya
wawekezaji wa kigeni au wazawa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, gharama tu za
mabasi yatakayotumika katika mradi huo, achilia mbali zile za ujenzi wa
miundombinu yake, zinagharimu zaidi ya Sh180 bilioni.
Watanzania tutaonekana kituko kama tutaacha fedha
hizi na nyinginezo zipotee bure bileshi, kama Serikali yetu itatoa
zabuni kwa mwekezaji asiye na sifa.
Hatuoni mantiki ya kizungumkuti kilichopo au
mjadala unaoendelea kuhusu nani aendeshe mradi kati ya wazawa na wageni.
Tunachoamini sisi ni kuwa ili mradi huu ulete matunda yaliyokusudiwa
kwa wananchi na Serikali, hauna budi kusimamiwa vilivyo na mwekezaji
mwenye weledi na umahiri mkubwa wa masuala ya usafiri hasa wa kisasa.
Sisi hatuamini katika aina, asili au mahala
anakotoka mwekezaji, bali tunaamini katika sifa stahiki za uendeshaji wa
mabasi haya ambayo tunasikitika kusema kuwa baadhi ya watu wanafikiri
uendeshaji wake unaweza kuwa mithili ya ule wa mabasi ya daladala.
Kuukubali tu mradi wenyewe unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, kunatoa
picha ya namna Serikali yetu ilivyo na dhamira ya dhati ya kupambana na
changamoto za usafiri katika jiji la Dar es Salaam.
Mradi huu unaelezwa kuwa pamoja na mambo mengine
utasaidia kupunguza foleni za magari barabarani ambazo takwimu
zinaonyesha zinachangia kupotea kwa takribani Sh 4 bilioni kila siku.
Hiki si kima kidogo katika uchumi unaoyumbayumba wa nchi yetu. Hii ni dhamira njema, hivyo Serikali isikubali kuja kutoka mikono mitupu kwa kuukabidhi mradi kwa mwekezaji dhaifu.
Tunaamini Serikali ina mfumo mzuri wa kutoa zabuni
katika miradi yake, tuache mchakato huo uchukue hatamu ili hatimaye
apatikane mwekezaji makini na mwenye uwezo wa kusimamia mradi huo
mkubwa.
Kama tunataka kuona athari chanya ya mradi huu
katika uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi, katu tusiruhusu ubabaishaji
au upendeleo kwa hoja ya uzawa au ugeni. Sote tunahitaji kuona
mafanikio ya mradi huu pasipo kujali mwekezaji anatoka ndani ya nchi au
nje.
Jambo zuri ni kuwa nchi hii tuna uzoefu mzuri wa
kufeli kwa mashirika mbalimbali ya umma yaliyojishughulisha na sekta ya
usafiri hasa wa abiria. Pamoja na sababu nyingizo mashirika haya
yalianguka kwa sababu ya kuendeshwa kiubabaishaji.
Hakukuwapo na utashi wa wahusika kuviendesha
vyombo hivyo kwa weledi, utaalamu na umahiri, hatimaye vikafa na sasa
vimebaki historia. Hata pale baadhi vilipobinafishwa, tunadiriki kusema kuwa bado
vimeendeelea na usimamizi uleule wa ‘bora liende’. Matokeo yake vyombo
hivyo vinasuasua, huku vikiwa havina mchango wowote wa maana kwa nchi na
wananchi walio wengi.
Huu si mradi wa kitoto na kama kweli tunaamini
kuwa ni uwekezaji muhimu na mkubwa kwa Taifa, Serikali haina budi kumpa
zabuni mwekezaji mwenye uwezo na sifa zinazorandana na umuhimu na ukubwa
wa mradi wenyewe.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment