Social Icons

Pages

Friday, April 17, 2015

WAZIRI CHIKAWE AENDELEA KUPINGWA

Tamko la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, limeendelea kupingwa na asasi mbalimbali huku asasi ya kiraia inayotoa msaada kisheria na kutetea haki za binadamu nchini (SLPC), ikitaka serikali kuacha kutoa matamko ya vitisho.Mwenyekiti Mtendaji wa SLPC, Masesa Mashauri, alisema serikali kupitia waziri wake iache kuendelea kutoa matamko ya kutishia kuchukua hatua bali ichukue hatua hasa pale inapoonekana na kuthibitika kuwa kuna kila dalili za uvunjifu wa amani.
Jumanne wiki hii, Waziri Chikawe, alitishia kuchukua hatua kali kwa watu binafsi, vyama vya siasa, kijamii na vya kidini vitakavyobainika kuvuruga usalama na utulivu wan chi katika kipindi cha kura ya maoni kwa Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu, huku akitishia kufuta asasi kadhaa kuanzia wiki ijayo.
Mashauri alisema: “Serikali iache kuendelea kutoa matamko ya kutishia kuchukua hatua bali ichukue hatua hasa pale inapoonekana na kuthibitika kuwa kuna kila dalili za uvunjifu wa amani ya nchi yetu, maana ikitoweka haitakuwa rahisi kuirejesha.”
Alisema ni vema ikamuacha mwananchi huru kutoa uamuzi wa ama kuikubali au kuikataa Katiba inayopendekezwa. “Elimu inayotakiwa kutolewa juu ya jambo fulani kama vile kupiga kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa, kisha mtu aachwe huru kufanya maamuzi yake mwenyewe bila kushinikizwa.
Mkoani Morogoro,  mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk. Joel Mmasa, alisema anapinga msimamo wa Serikali kuhusu kusudio au hatua yoyote ile ya kutaka kuvifuta vyama vya kiraia na kidini kwani inaweza kuchochea migogoro mingine.
Alisema kufuta vyama hivyo ambavyo vimekuwa vikisaidia kwa kiasi kikubwa kuleta amani ya nchi pamoja na kuchochea shughuli mbalimbali za maendeleo, kutaanzisha uchochezi, machafuko na kwamba Chikawe amekurupuka kutoa maamuzi hayo ambayo hayana tija kwa Watanzania.
Mmoja wa viongozi wa Taasisi ya Dini ya Kiislam mkoani Morogoro, Abdallah Sareh, alisema kuwa kutishia kufuta taasisi za dini kutokana na kukiuka Katiba zake sio suluhisho bali sasa ni wakati mwafaka kwa Serikali kukaa meza moja nao ili kutatua masuala mbalimbali.
Alisema ikiwa Serikali itashikiria msimamo wake, itaanza kuchochea migogoro mingine ambayo sio mwafaka wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu. Mwenyekiti wa Muungano wa vyama visivyo vya Kiserikali mkoani Morogoro (Ungo), Maliki Malupo, alisema yapo mashirika ambayo yameacha kazi yao ya kuelimisha umma kupitia usajili wao, hivyo badala ya kufikilia kuyafuta kwa sasa, ni vizuri Serikali kwanza ikayaonya ili kurudi katika mstari.
Alisema suala la kuabudu huku likihusisha siasa halihitaji kutolewa tishio na Serikali bali inapaswa kuwaelimisha viongozi wa dini na kukaa nao kuzungumza.

CHANZO: NIPASHE

No comments: