Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.
Machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Burundi, yamesababisha mamia ya raia wa nchi hiyo kukimbilia Tanzania kama wakimbizi.
Raia hao walianza kuingia nchini jana kwa ajili ya kutafuta hifadhi mkoani Kigoma. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilithibitisha kuingia kwa
wakimbizi zaidi ya 200. Msemaji wa wizara hiyo, Isaack Nantanga,
aliliambia NIPASHE kuwa wakimbizi hao waliingia mkoani Kigoma kupitia
vijiji vya Kagunga, Kakonko, Kijaje na Chakeoya.
Nantanga alisema kuwa baada ya wakimbizi yao kuingia katika maeneo
hayo, maofisa wa Idara ya Uhamiaji walikuwa wanaendelea na taratibu za
kawaida za kuwapokea wakimbizi. Hata hivyo, mwandishi wa NIPASHE alipofika katika eneo la mpaka wa
Tanzania na Burundi, Manyovu na kuzungumza na maofisa mbalimbali wa
Serikali, walimthibitishia kwamba kuna wakimbizi walioingia mkoani
Kigoma na wengine wanaendelea kuingia.
Mmoja wa maofisa Uhamiaji ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa
maelezo kuwa siyo msemaji, alisema kuwa wakimbizi 150 kutoka Burundi
waliingia mkoani humo na walikuwa katika kijiji cha Kagunga, wilaya ya
Kigoma Vijijini.
Alisema kuwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji waliondoka jana kwenda
Kagunga kuwachukua wakimbizi hao kwa boti na kuwapeleka katika kambi ya
wakimbizi ya Nyarugusu kwa ajili ya kuwahifadhi. Alisema kuwa watakaa kambini hapo hadi hali ya utulivu itakaporejea nchini Burundi.
Awali kabla ya kuthibitisha taarifa kuwa kuna kundi la wakimbizi
waliokuwa wameingia nchini kutoka Burundi, Nantanga aliliambia gazeti
hili kuwa serikali ilikuwa imeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo
ya mipakani katika mikoa ya Kigoma na Kagera kufuatia hofu ya baadhi ya
wakazi wa mikoa hiyo kwamba kuna wakimbizi kutoka Burundi ambao
wataingia nchini bila kufuata taratibu.
Nantanga alisema pamoja na kuwapo taarifa kuwa kuna baadhi ya
wakimbizi katika maeneo ya mipakani, hakuna taarifa ya wakimbizi
walioingia na watakaoingia nchini bila kibali. “Hali ni shwari katika maeneo ya mpakani na hakuna matatizo wala
tukio la mkimbizi au wakimbizi kuingia nchini bila kufuata taratibu,
inawezekana wakawapo wawili au mmoja ambao wamepita njia za porini kwa
kuwa kuna mapori,” alisema Nantanga. Alisema iwapo kuna wakimbizi ambao
wataingia nchini, vipo vituo maalum ambavyo ni kwa ajili ya kupitia
wakimbizi.
MACHAFUKO BURUNDI
Burundi imekumbwa na ghasia kutokana na maandamano yanayofanyika
katika mji mkuu, Bujumbura na wafuasi wa vyama vya upinzani wanaopinga
hatua ya Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza, kutaka kugombea tena
urais, baada ya kumaliza muda wake wa mihula miwili.
Katiba ya Burundi inatajwa muda wa urais kuwa vipindi viwili,
lakini Rais Nkurunziza anasema kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa
Arusha, kipindi chake kinaanza pale mkataba wa Arusha uliposainiwa,
hivyo muda aliokuwa madarakani kabla ya kusainiwa usihesabike.
Anasema kuwa hiki kitakuwa kipindi chake cha pili na cha mwisho. Hata hivyo, upinzani unapinga na yamekuwapo maandamano kuanzia
Jumamosi ya kupinga hatua hiyo na tayari watu kadhaa wametiwa nguvuni na
baadhi wanadaiwa kupoteza maisha.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment