Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Sasa yagundulika aliyeleta mabehewa feki alikuwa na bei ya juu kuliko wote, aliruhusiwa na kufanyia marekebisho zabuni yake
kinyemela.Madudu zaidi yameendelea kuibuka katika sakata la
mabehewa feki 274 yaliyonunuliwa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), na
sasa imebainika kuwa kampuni iliyopewa zabuni ya kuleta mabehewa hayo
ndiyo iliyokuwa ya bei ya juu zaidi kuliko kampuni 10 zilizokuwa
zimeomba na haikuweka dhamana yoyote kama sheria ya manunuzi inavyotaka.
Aidha, imebainika pia kuwa ya Hindustan Engineering Ltd ya India,
ambayo ilishinda zabuni hiyo, ilibadilishiwa vigezo (specification), vya
aina ya mabehewa kinyemela baada ya zabuni kutangazwa na wazabuni
kuwasilisha maombi yao.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika ambazo NIPASHE imezipata, kampuni
hiyo iliomba kuiuzia TRL mabehewa 174 yenye ‘rubber’ badala ya ‘spring’
kwa dola za Marekani 18,209,317.50 (Sh. bilioni 32.8) wakati kampuni ya
Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd ya China ilikuwa tayari kuleta idadi
hiyo ya mabehewa yenye viwango vinavyokubalika kwa dola za
Marekani 13,907,907 (Sh. bilioni 25).
Kampuni hiyo pia ilishinda zabuni hiyo ambayo ilihusisha kuleta
mabehewa mengine 100 ya mizigo ambayo ni ya muundo wa matangi (tank
wagon) na yasiyofunikwa (flat wagon) kwa dola za Marekani 10,278,182.50
(Sh. bilioni 18.5) wakati kampuni ya Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd ya
China iliyokuwa ndiyo yenye bei ndogo ilikuwa tayari kuleta idadi hiyo
ya mabehewa kwa dola za Marekani 7,272,975 (Sh. bilioni 13.09).
Kampuni hiyo pia ilishinda zabuni ya kuiuzia TRL vipuri kwa thamani
ya dola za Marekani 2,561,187.50 (Sh. bilioni 4.4) baada ya
kuirekebisha na taarifa ya zabuni inaonyesha kuwa iliwasilisha zabuni
iliyorekebishwa na ilikubaliwa.'
Kampuni ya Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd iliomba kuleta vipuri
hivyo kwa dola za Marekani 2,475,835 (Sh. bilioni 4.46) wakati kampuni
nyingine kama Transnet iliomba kwa dola za Marekani 3,108,687 (Sh.
bilioni 5.6) wakati Modern Industries iliyoshindwa kwa kutowasilisha
dhamana iliomba kwa dola za Marekani 3,344,925 (Sh. bilioni 6.02).
Kwa ujumla taarifa zinaonyesha kuwa kampuni ya Hindustan
Engineering ililipwa dola za Marekani 31,048,688 (Sh. bilioni
55.9) wakati kampuni iliyokuwa ya bei ndogo kuliko zote ingeweza
kufanyakazi hiyo kwa dola za Marekani 24,368,757 (Sh. bilioni 43.86)
hatua ambayo ingeokoa dola za Marekani 6,677,931 (Sh. bilioni 12.02) na
kutoitumbukiza nchi kwenye hasara hiyo ya mabehewa feki.
“Mabehewa nyenye rubber hayawezi kabisa kwa namna yoyote ile
kupita kwenye reli yetu. Kilichotokea ni kwamba zabuni iliyotangazwa
ilitaka wazabuni walete mabehewa yenye spring ambayo ndiyo sahihi,
lakini baadaye inaonekana walibadilisha vigezo na kuielekeza kampuni
waliyoipa zabuni vigezo vipya ndiyo maana unaona mabehewa yaliyokuja
hayafai,” alisema mmoja wa wataalam wa reli ambaye hakutaka jina lake
litajwe gazetini.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kampuni ya Hindustan Engineering Ltd
haikuweka dhamana yoyote jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya manunuzi
ya umma na ilitaka ilipwe fedha yote kabla ya kuingiza mabehewa nchini
jambo ambalo TRL ilitekeleza.
Wakati mzabuni huyo akiweka masharti hayo, kampuni nyingine
zilizoomba ikiwamo iliyokuwa ya bei ndogo zaidi, iliweka dhamana na
ilitaka ilipwe kwa awamu hadi itakapokamilisha kazi husika. Taarifa zaidi zinaeleza kuwa pamoja na kwamba kampuni ya Hindustan
Engineering Ltd ilikuwa ya gharama kubwa iliomba kufanya kazi hiyo kwa
miaka miwili, wakati kampuni nyingine zilizoshindana kwenye zabuni
zingeweza kufanya kazi hiyo kwa miezi tisa hadi mwaka mmoja.
Kampuni ya Hindustan Engineering Ltd haikuweka gharama za matengenezo wakati kampuni nyingine zote ziliweka. Taarifa zinaonyesha kuwa kampuni nyingine zilikosa sifa za
kushinda zabuni kwa kutowasilisha dhamana (bid security), ikiwamo ile ya
Modern Industries, DCD rolling stock ambayo pia iliwasilisha bei
zilizokuwa na kasoro za kiuandishi pamoja na Lucky Export.
Kampuni nyingine zilizoomba zabuni hiyo ni Caeic Beigin Ltd, CNR
Import and Export Corporation Ltd, Hyunan Construction Engineering Ltd,
Texmaco Rail and Engineering na Transnet. Taarifa hizo zimeibuliwa siku sita tu baada ya Alhamisi iliyopita
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kuwasimamisha kazi vigogo watano wa
TRL, akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wake, Kipallo Kisamfu, kutokana tuhuma
za kuihujumu serikali katika sakata la ununuzi wa mabehewa feki 274 ya
mizigo na kuisababishia hasara ya Sh. bilioni 230.
Wengine waliosimamishwa ni Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile
Ngosomiles; Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa; Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper
Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka. Sitta alisema baada ya kuwasimamisha vigogo hao, utafanyika uchunguzi dhidi yao kwa wiki tatu kuanzia wiki iliyopita.
Kufuatia uamuzi huo, Sitta alimteua aliyekuwa Mhandisi wa TRL,
Elias Mshana, kuwa Kaimu Mkurugenzi wa kampuni hiyo, na kumwagiza Katibu
Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, kusimamia kuundwa kwa
kamati ya uchunguzi huo.
Alisema kamati hiyo itaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) akishirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya
Umma (PPRA) pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Sitta alichukua uamuzi huo baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi
ya kamati iliyoundwa na Waziri aliyemtangulia wizarani hapo, Dk.
Harrison Mwakyembe, ambaye alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, ambayo imegundua kuwako kuna hujuma mbalimbali katika
kuendesha TRL.
Kabla ya kuchukua uamuzi wa jana, Waziri Sitta aliiagiza bodi ya
Wakurugenzi ya Reli kupitia taarifa hiyo na kutoa maelezo kwake juu ya
suala ya ununuzi wa mabehewa hayo. Mabehewa hayo yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya
M/S Hindustan Engineering and Industrial Limited ya India ikishirikiana
na kampuni moja nchini inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja ambaye
amekuwa akijihusisha na biashara nyingi za kulaghai mashirika ya umma na
kujipatia ukwasi wa kupindukia.
Mabehewa hayo yaligundulika kuwa mabovu baada ya kufanyiwa
majaribio na baadhi kuanguka kwa kukosa ‘stability’ yakiwa relini na
yaliyopokelewa na Dk. Mwakyembe Julai 24, mwaka jana, hayakupitiwa na
jopo la mafundi wa TRL ili kuthibitisha ubora wake. Jana NIPASHE lilimtafuta Waziri Sitta kuzungumzia taarifa hizo
bila mafanikio kutokana na simu zake za mkononi kushindwa kupatikana.
Hata hivyo mmoja wa walinzi wake aliliambia NIPASHE kuwa waziri
huyo alikuwa kwenye kikao ambacho hata hivyo hakueleza kilikuwa
kinafanyikia wapi.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment