Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) limetangaza mgawo wa umeme kwa siku tisa katika
baadhi ya maeneo kutokana na upungufu wa nishati hiyo katika Gridi ya
Taifa.
Hali hiyo imetokana na maombi ya Kampuni ya Pan
African Energy (PAT) inayosimamia uzalishaji wa gesi asilia Songosongo
kusimamisha uzalishaji kwa nyakati tofauti ili kufanya matengenezo na
kubadilisha baadhi ya vifaa kwenye mitambo yake.
Taarifa ya shirika hilo kwa vyombo vya habari
iliyotolewa jana ilisema shughuli hiyo itafanyika kwa siku tofauti kati
ya Aprili 6 na Mei 10.
“Hivyo Shirika linawatangazia wateja wake
waliounganishwa kwenye mfumo wa gridi ya Taifa kwamba kutakuwa na
upungufu wa umeme kwa baadhi ya maeneo kutokana na matengenezo hayo
yanayofanyika kila mwaka,” ilisema.
Tanesco inategemea gesi hiyo kuendesha mitambo
yake ya Ubungo 1, Ubungo 2 na Tegeta yenye uwezo wa kufua megawati 245
na kuendesha mitambo mingine ya umeme ya Songas yenye uwezo wa megawati
180.
Taarifa hiyo ilisema pamoja na kutumia vyanzo
vingine vya kufua umeme kama maji na mafuta, katika kukabiliana na
matengenezo hayo, ukosefu huo wa gesi utaathiri ufuaji wa umeme kwa siku
tisa. Hata hivyo, taarifa hiyo ilisema upungufu huo kwa kila siku
utagawanywa kidogokidogo kwenye mikoa iliyopo kwenye gridi na
hautaathiri upatikanaji wa umeme kwa mkoa mzima.
Akizungumzia mgawo huo, Meneja wa Mawasiliano
Tanesco, Adrian Severin alisema ukiondoa tatizo hilo la ukarabati wa
miundombinu ya gesi, shirika lake halina tatizo la kuilazimisha nchi
kuingia katika mgawo kwa sasa.
Pia, aliitaja mikoa ambayo haitaathiriwa na mgawo
huo kuwa ni Kagera, Ruvuma, Kigoma, Lindi, Mtwara na Wilaya ya Loliondo,
Arusha.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment