Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mathias Chikawe, imetoa tamko kali la kutishia kuanza kutekeleza
sheria inayodhibiti asasi za kijamii na kidini, ikizitaka taasisi hizo
kuacha mara moja kutoa matamko yanayolenga kuwashawishi waumini wao
waikatae Katiba Inayopendekezwa na pia kuwapangia nini cha kufanya
katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua
kali.
Uamuzi huo wa Serikali umekuja baada ya Jukwaa la
Wakristo kutoa tamko la kuwataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi
katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa
na kujitokeza kuikataa kwa kupigia kura ya hapana.
Kwa mujibu wa tamko hilo kutowasilisha hesabu za
mwaka na kujihusisha na siasa ni ukiukaji wa sheria na adhabu yake ni
kufutiwa usajili. Hatutetei uvunjaji wa sheria, lakini uamuzi wa
Serikali unazua maswali mengi kuliko majibu. Mfano kwanini uamuzi huu
umekuja wakati kuna tamko la Jukwaa la Wakristo au sintofahamu kati ya
Polisi na Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat
Gwajima.
Inawezekana uamuzi huu ni kukasirishwa na mtazamo
wa taasisi za dini unaopinga na kuhamasisha waumini wake (si Watanzania
wote) kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa. Kama huo ndiyo
ukweli ni ipi nafasi ya viongozi wa Serikali, makada na taasisi zingine
ambao wanahamasisha kura ya ndiyo kwa Katiba Inayopendekezwa.
Tunavyofahamu kura ya maoni inatumika katika
demokrasia ili kuchagua viongozi wa nchi au kuamua kama sheria fulani
itumike. Kawaida kura ya maoni hupigwa na wale wote wenye umri halali wa
kupiga kura ili kukubali au kukataa pendekezo, sera, sheria, mabadiliko
ya katiba, katiba mpya, kukataa au kumuunga mkono kiongozi fulani. Kura
ya maoni huchukuliwa kuwa ni aina mojawapo ya demokrasia ya moja kwa
moja.
Kwa hoja hiyo, viongozi wa dini walikuwa wanatumia
haki yao ya kidemokrasia kutoa mawazo yao, kama wanavyofanya wengine
wanaohamasisha kura ya ndiyo kwa Katiba Inayopendekezwa.
Lakini sote ni mashahidi kuhusu Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Sheria hii inatamka aina tatu za
Wajumbe wa Bunge la Katiba, Wabunge, Wawakilishi na Wajumbe 201 kutoka
makundi mbalimbali 10 wanaotajwa na Kifungu na. 22(1c) cha sheria hiyo.
Ndani yake kuna kundi la Taasisi za Kidini lenye wajumbe 20.
Tunaamini na ndivyo ilivyo wajumbe 20 kutoka
taasisi za kidini, waliteuliwa kwenda kujadili na kulinda maslahi yao
ndani ya Bunge la Katiba, na ndiyo maana masuala ya mivutano ya kidini,
mfano Mahakama ya Kadhi, yalijadiliwa kwa upana wake kuanzia kwenye
kamati hadi ndani ya Bunge zima.
Baada ya Bunge kumalizika wajumbe wote zikiwemo
taasisi za kidini walirudi kwenye maeneo yao kupeleka mrejesho, kuna
makundi hayakuridhika kwa sababu mambo yao mengi yalitupwa na kuna
makundi yaliridhika na walichopata. Ubaya uko wapi kwa wanaoipinga
Katiba Inayopendekezwa. Ndiyo maana kwenye Kura ya Maoni kuna ‘ndiyo’ na
‘hapana’. Kama Serikali inataka watu wote wapige kura ya ndiyo hakuna
maana ya kutumia fedha nyingi kuitisha Kura ya Maoni.
Tunaiomba Serikali iache demokrasia ishamiri,
Wajumbe wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba wana haki ya kusema hapana
au ndiyo kwa makundi yao. Makundi hayo ndiyo yaliyowatuma bungeni.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment