Msitu
Siku chache baada ya wananchi
wilayani Mbinga kupinga uvunaji wa Msitu wa Mbambi, Mkurugenzi Mtendaji
wa wilaya hiyo, Hussein Ngaga amesema huo ni ukikwaji wa sheria.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wananchi hao walizuia
mbao zisiondolewe katika msitu huo kwa madai kuwa uvunaji unaoendelea
utaathiri upatikanaji wa maji ambayo chanzo chake ni msitu huo.
Ngaga alisema juzi kuwa uvunaji wa msitu huo unafanywa kwa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha baraza la madiwani. “Wilaya ina misitu sita ambayo utaratibu unaeleza
kuwa itavunwa iwapo kutakuwa na dharura au mahitaji muhimu. Hayo yote
yamejitokeza ndiyo maana baraza lilipitisha uamuzi wa kuvuna msitu huu,”
alisema Ngaga.
Alisema msitu huo ni mali ya halmashauri na kwamba
ulianzishwa tangu mwaka 1984 na wananchi waliokuwapo eneo hilo baada ya
kulipwa stahiki zao. “Tunavuta msitu huu kwa sababu tumekubaliana na tumejiridhisha kuwa ni wakati mwafaka kufanya hivyo,” alisema.
Ngaga alifafanua kuwa mahitaji yaliyochangia
kufikia huo ni upungufu wa madawati 12,000 katika shule za msingi,
ujenzi wa madaraja sita yaliyopo Mbinga Mjini, Maguu, Mapera na Kipapa. “Tunayo misitu mingine ambayo ni Tukuzi, Mbuji,
Ndengu, Mahenge na Lubera ambayo tumewapa Wilaya ya Nyasa ili wavune.
Nawaomba wananchi wawe wavumilivu na waache dhana ya kuwa jambo hili
linafanywa pasipo kufuata utaratibu,” alisema.
Ngaga alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa
miradi mbalimbali yenye manufaa kwao inatekelezwa kwa kuunganisha nguvu
za wananchi.
Awali, wananchi hao walisema uvunaji huo unafanywa bila kuzingatia mahitaji yao na kwamba hawajashirikishwa. Walisema shughuli hiyo inaendeshwa kwa masilahi binafsi ya baadhi ya watendaji wa wilaya ya hiyo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment