Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, akipata maelezo kutoka
kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya Farm Equip Tanzania Limited
(FETL), Rattan Singh (wa tatu kushoto) juu ya matumizi ya zana za kisasa
za kilimo.
Akiwa kwenye maonyesho ya wadau wa kilimo kwa
nchi za Afrika Mashariki yaliyofanyika Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Dk
Mohamed Gharib Bilal anasema Serikali imejipanga kuhakikisha inakifanya
kilimo ni mkombozi wa kumuondoa mkulima kwenye umaskini.
Anasema hayo akiamini mipango iliyowekwa na
Serikali ya ‘Kilimo Kwanza’ na Matokeo Makubwa Sasa (BRN) itaweza
kufanikiwa kwa kushirikiana na wadau waliowekeza katika kilimo nchini.
“Ni mkakati wa kuwasaidia wakulima kuondokana na
kilimo kisicho na tija na kuingia katika kilimo cha manufaa kwa
maendeleo ya Taifa letu hivyo tumejipanga kutekeleza hilo kwa nguvu
zote,” anasema Dk Bilal.
Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira
anakiri Serikali ina wajibu mkubwa wa kuwekeza katika kilimo ili
Watanzania watoke katika ukulima wa kujikimu na kuingia katika kile
chenye tija.
Anakiri kuwa umaskini huu mkubwa unawakumba zaidi
watu wa vijijini na kwamba Tanzania haiwezi kuwaondoa kwenye umaskini
huo bila kuweka mipango bora zaidi na mahususi ya kuwekeza katika
kilimo.
“Lingine muhimu ni kuwa kilimo bila viwanda,
hakiwezi kuwa na tija, hivyo ni lazima viwapo viwanda vya kuongeza
thamani za mazao ili kilimo kiwanufaishe wakulima,” anasema Wasira.
Miongoni mwa kampuni zilizowekeza katika
kutekeleza mpango wa Kilimo Kwanza ni Farm Equip Tanzania Limited (FETL)
ambayo inajihusisha na usambazaji wa zana za kilimo pamoja na
uelimishaji.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa FETL, Rattan Singh
anasema ili kufikia kilele cha mafanikio katika haya ni lazima wakulima
wapewe vifaa vya kisasa katika kilimo, elimu na wataalamu wa kuwasaidia.
Singh anasema bila kumpa mkulima elimu itakuwa ni ndoto kutekeleza mbinu za kufanikisha mapinduzi ya kijani. “Ni lazima mkulima kufahamu matumizi bora kwa
kilimo chenye tija,” anasema Singh akisisitiza kuwa mpango huo umeanza
kutekelezwa na kampuni yake kupitia vyuo mbalimbali nchini.
Anasema wanafunzi hao ni wale walio katika vyuo
vya kilimo na ufundi ili kuwawezesha pindi wakimaliza masomo wanaweza
kutumia teknolojia hiyo kwa wakulima.
Miongoni mwa teknolojia hizo anasema ni utumiaji
wa zana za kisasa za kilimo kuanzia za kulima, kupalilia, kuvuna na
usafirishaji. “Hivi sasa tunatoa udhamini kwa wanafunzi wanaosomea uhandisi
katika wa zana za kilimo mafunzo katika vyuo vya kilimo na teknolojia
ambavyo ni mdau mkubwa wa maendeleo ya kilimo nchini,” anasema Singh.
Lengo la mpango huo anasema ni ili watokapo vyuoni
wawe na uwezo wa kutoa elimu kwa wakulima, ikijumuisha uendeshaji
mashine na mitambo ya kilimo.
Anatoa mfano mkakati wa hivi karibuni wa kutoia
vyeti kwa wahitimu wa teknolojia hizo katika Taaisi ya Taasisi ya
Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na kwamba huo ni mpango endelevu.
Malengo mengine, Singh anasema ni kuelimisha wakulima kupitia maonyesho mbalimbali nchini kwa kutumia zana zao. Singh anasema hata uuzaji wa zana za kilimo
tofauti na biashara nyingine, hizi zinahitaji ukaribu wa wataalamu
wanaoelewa kwa undani teknolojia ya mashine zinazotumika.
Wingi wa jamii katika sekta ya kilimo inaweza kuwa
ni tatizo la Serikali kutekeleza na kufanikisha mikakati ya BRN na
Kilimo Kwanza. Serikali lazima ishirikiane na wadau wa sekta hiyo, hasa
waliowekeza katika kilimo, ili kuhakikisha wanakuwa ni sehemu ya
kufanikisha mipango hiyo.
Serikali ina kila sababu ya kuweka mazingira mazuri yatakayowaunganisha moja kwa moja, wakulima na wawekezaji wa sekta hiyo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment