Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara,
Philip Mangula, amewajia juu baadhi ya viongozi wa dini kwamba
wanawapotosha wananchi waikatae Katiba inayopendekezwa kwa kuwa
inapendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.Mangula amesema kuwa katiba hiyo haina ibara inayozungumzia masuala
ya dini na Mahakama ya Kadhi na kuwataka wamuonyeshe kipengele
kinachotaja masuala hayo. Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanafunzi wa sekondari, wanachuo na walimu wa Shule ya Sekondari Hagaf.
Mangula alifafanua kuwa ameisoma Katiba yote na hajaona ibara wala sura inayozungumzia masuala ya udini wala Mahakama ya Kadhi. Mangula alisema kuwa viongozi wa dini wanawaelekeza wananchi
kuikataa katiba hiyo, lakini walichofanya maaskofu ni kutoa matamko ya
kupinga kuwasilishwa bungeni na kupitishwa kwa muswada wa kuanzishwa kwa
Mahakama ya Kadhi.Maelekezo yao kwa waumini wao kutokuipigia Katiba
kura ya ndiyo, yalitokana na kutoridhishwa kwa viongozi hao na mchakato
mzima ikiwamo kusuasua kwa uandikishaji wa wapigakura, kuchelewa
kupelekwa kwa nakala za Katiba na mgawanyiko katika Bunge Maalum la
Katiba.
“Katiba hii inayopendekezwa nimeisoma yote, lakini sijaona mahali
hata panapozungumzia masuala ya dini fulani, lakini nashangaa katika
makanisa wananchi wanashawishiwa kutoipigia kura kwa sababu inaunga
mkono Mahakama ya Kadhi, hakuna kitu kama hicho,” alisema Mangula.
Alisema alikuwa katika kanisa moja anakosali na Mchungaji
aliwaeleza waumini wasiipigie kura Katiba inayopendekezwa kwa kuwa ina
masuala ya Mahakama ya Kadhi na kwamba alipomuuliza ni ibara gani
inayozungumzia mahakama hiyo, mchungaji huyo alishindwa kuitaja na
kusema haifahamu.
“Jumapili moja kanisani, Mchungaji aliwahimiza wananchi
kijiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na wasiipigie
Katiba inayopendekezwa kura ya ndiyo kwa sababu katika katiba hiyo kuna
masuala ya udini na Mahakama ya Kadhi. Lakini nilipomuuliza alisema kuwa
yeye kasoma waraka na Katiba bado hajaisoma na akawa anashangaa kama
kipengele kimo ama hakimo,” alisema Mangula.
Mangula aliwaeleza walimu na wanafunzi hao kuwa kiongozi yeyote
atakayewataka kutoipigia kura katiba hiyo kwa maelezo kuwa ina mrengo wa
dini fulani, wamwambie aeleze ni ibara gani inayozungumzia suala hilo. Alisema anawashangaa wanaowashawishi wananchi kutoipigia kura katiba hiyo wakati hawajaisoma na kuelewa mambo yaliyomo.
Alisema kilichomo katika Katiba hiyo ni ibara inayozungumzia utawala wa sheria na kuwapo kwa Mahakama huru. Alisema kuwa kuna ibara inayoeleza kuwa Jamhuri ya Tanzania itakuwa na utawala wa sheria na huru isiyofungamana na dini yoyote.
“Watu wameanza kuzua mambo ya ajabu sana na wanaizuia Katiba,
Katiba hii inasema Tanzania itakuwa ni nchi inayofuata misingi ya
demokrasia na utawala wa sheria, inayojitegemea na isiyo fungamana na
dini yoyote,” alisema Mangula na kuongeza: “Anza ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho, hakuna sehemu inayozungumzia Mahakama ya Kadhi,” alisisitiza.
Alisema katiba hiyo ina mambo mengi mapya tofauti na ya zamani
kama ufafanuzi wa makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 na kuwa
makubaliano hayo ndiyo msingi wa nchi. Alisema kuwa katika Katiba inayopendekezwa, kuna misingi ya
utawala bora na umiliki wa ardhi na kuwa ardhi hiyo inatunzwa na mali ya
Mtanzania wa kizazi cha sasa na cha baadaye.
Katika hatua nyingine, Mangula alikubaliana na kauli ya Askofu Mkuu
wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp
Kardinali Pengo, kuwataka viongozi wa dini kutowaelekeza wananchi wapige
kura ya aina gani, bali waachwe wafanye maamuzi yao.
Alisema kuwa wananchi wakiisoma Katiba inayopendekezwa kama kuna
mapungufu watayaona na kama kuikataa, basi wafanye hivyo wenyewe. Mangula aliongeza kuwa kwa wanaosema Katiba inayopendekezwa ipigiwe
kura ya hapana, watoe hoja badala ya kutoa maelekezo bila kuwa na hoja
zisizo na mashiko.
Jukwaa la Kikristo Tanzania linaloundwa na Baraza la Maaskofu
(Tec), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Makanisa ya
Pentekoste Tanzania (PCT), limekuwa likitoa matamko kadhaa ya kupinga
kuwapo kwa Mahakama ya kadhi nchini. Muswada huo hadi sasa umeshindikana kuwasilishwa bungeni katika
mkutano wa 18 na 19 baada ya wabunge kugawanyika wakati wa semina ya
kuujadili.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment