Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali
Iddi, amewanasihi Wajumbe wa Baraza hilo kuweka kando jazba
wanapojadili mambo ya Kitaifa na badala yake watekeleze vyema wajibu
unaowahusu kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.
Alisema alitoa ushauri huo kufuatia mvutano kati ya wawakilishi wa
CCM na CUF juzi kuhusiana na uandikishaji wananchi katika daftari la
Mzanzibari mkaazi. Na kwamba kwa kufanya hivyo, lengo kuwafikia litakuwa
limefikiwa.
Alisema ni vyema Wawakilishi hao wakaelewa kuwa wananchi wengi
wanafuatilia matendo yao ndani ya Baraza na iko siku wananchi hao
watafikia uamuzi wa kuwahukumu kwa matendo yao. Balozi Iddi alitoa kauli
hiyo wakati akiufunga Mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi na
kuongeza kuwa mambo yaliyotokea ndani ya Baraza hilo Machi 11, mwaka huu
wakati wa kuwasilishwa sheria ya Kura ya Maoni nambari 11 ya mwaka 2013
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Kifungu 131 (2) cha
Katiba ya Zanzibar mwaka 1984 yamewasikitisha wananchi wengi.
Alisema vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyofanywa na baadhi ya
Wajumbe vilitoa sura mbaya ya Baraza hilo mbele ya wananchi
wanaowawakilisha katika chombo hicho muhimu. Balozi Seif alisema kupitia vyombo vya habari vilivyokuwa vinarusha
matangazo ya vikao vya Baraza hilo, wananchi wengi walishuhudia mchezo
wa baadhi ya wawakilishi hao badala ya kufanya kazi waliyotumwa.
Alitahadharisha kwamba kutofautiana kwa wawakilishi kwenye Baraza
au Bunge wakati wa mijadala ni mambo ya kawaida, lakini itapendeza kuona
kuwa busara inatumika katika jambo wanalotofautiana badala ya kutumia
jazba.
Aliwaomba viongozi wote wa kisiasa na wa kijamii pamoja na wananchi
kushirikiana na Serikali katika kuendeleza na kudumisha amani na
utulivu uliopo. Kuhusu vitambulisho vya Mzanzibari ambalo lilionekana kuibua
mjadala mkali ndani ya baraza hilo, alisema kila Mzanzibari anastahiki
kupata kitambulisho hicho baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa
kisheria.
Alisisitiza na kuwaomba Wawakilishi na wananchi kuelewa kuwa
Serikali haitamnyima haki Mzanzibari yeyote aliyetimiza masharti ya
kupata kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment