“Askari lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu wajue kuwa kuna mtu
hatari dhidi yao. Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu
utapungua tu na hivyo kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache
wanaoendelea na vitendo hivyo.”
Omari Mahita
Inspekta
Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Omary Mahita amesema askari polisi kwa
sasa wamepoteza hadhi, hawaogopwi na wahalifu na ndiyo sababu kubwa ya
kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu kila kukicha. Mahita aliyestaafu mwaka 2006, alisema mbali na
kuongezeka kwa uhalifu, inafikia hatua wahalifu wanawaingilia polisi kwa
kuvamia vituo vya polisi na kupora silaha ilhali zamani hakukuwa na
matukio hayo.
Hata hivyo, IGP, Ernest Mangu amejibu kauli hiyo
akisema: “Siwezi kutumia mbinu za Mahita kwa sababu alichokuwa
anakabiliana nacho, kwa sasa hakipo.”
Kauli ya Mahita
Kauli ya Mahita imekuja miezi minane baada ya
askari 10 kuuawa na bunduki zaidi ya 20 kuporwa katika matukio
mbalimbali ya uvamizi wa polisi na vituo vya polisi.
Akizungumza na mwandishi wetu baada ya kutoa
heshima za mwisho kwa mwili wa Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali
ya Hewa, Dk Mohamed Mhita, Oysterbay Dar es Salaam juzi, Mahita alisema:
“Ili kupunguza vitendo vya kihalifu vinavyozidi kuongezeka kila
kukicha, ni lazima askari warudishe hadhi yao ya kuogopwa na wahalifu
popote walipo.
“Askari lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu
wajue kuwa kuna mtu hatari dhidi yao. Kama mhalifu atatiwa woga na
uwepo wa polisi, uhalifu utapungua tu na hivyo kubakiwa na kazi ndogo ya
kuwakamata wachache wanaoendelea na vitendo hivyo.”
Mahita alikosoa kitendo cha askari polisi kuwa
wapole na kueleza kuwa hilo ni suala lisilotakiwa kabisa kufanywa ndani
ya jeshi hilo na polisi. “Unambembelezaje mhalifu? Hawa ni watu
wanaostahili kubanwa kwa kila namna ili kukomesha vitendo vyao katika
jamii. Mhalifu yeyote akiachiwa, madhara yake ni makubwa katika jamii.”
Licha ya suala hilo, IGP huyo mstaafu alieleza
umuhimu wa doria katika kudhibiti uhalifu wa kila siku ambao hupunguza
amani miongoni mwa jamii na kuwafanya wananchi washindwe kutekeleza
majukumu yao kwa ufanisi na ratiba waliyojiwekea. Alitolea mfano wa vikundi vya uhalifu
vilivyojitokea hivi karibuni kama ‘Panya Road’, ‘Mbwamwitu’ na ‘Libya’
kwamba vimekuwapo kutokana na kupungua kwa doria inayotakiwa ifanywe na
jeshi hilo nchi nzima na hasa maeneo ya mijini.
“Enzi zangu doria ilipewa kipaumbele. Magari na
pikipiki yalikuwa yanazunguka kote katika jiji hili na kwingineko
mikoani karibu kila siku na walikuwa wanaogopeka kwa sasa yapo lakini
sidhani kama wanafanya kazi kama ilivyokuwa enzi zile,” alisema Mahita.
“Wahalifu walikuwa wanajua kuwa polisi wapo kazini
muda wote. Lakini sasa hivi mambo hayo hayapewi uzito unaotakiwa ndiyo
maana unaona kikundi kama Panya Road kinatingisha mji mkubwa kama huu
(Dar es Salaam). “Inawezekana vipi kikundi kama hicho kikatingisha amani ya jiji hili lenye viongozi wote wa jeshi?” alihoji Mahita.
IGP Mangu
CHANZO: MWANANCHI
Mahita alikuwa maarufu kwa jina la ‘Ngunguri’
kutokana na kauli yake alipokuwa akikabiliana na maandamano ya wafuasi
wa CUF kwamba kama viongozi wake wako ngangari basi polisi iko ngunguri
kukabiliana nao. Akizungumzia uhalifu katika vituo vya polisi,
Mahita alisema polisi imekosa kuungwa mkono hivyo kupunguza ufanisi wake
katika kutekeleza majukumu yake.
“Hata jamii ipo mbali pia… Raia ndiyo wanavamia na
kuua askari. Watu hawa wanaishi katika jamii hiihii. Hivyo ni vyema
ikajirudi na kuona kuwa hii ni taasisi muhimu kwa maisha na mali ya kila
mwananchi.”
Akizungumzia vifo vya askari hao, Mahita alisema
kuwa jamii imewasahau na kuwatenga kwani hakuna anayeshtuka pindi
wanapoteza maisha hata kama mauti hayo huwakuta wakiwa kazini.
IGP Mangu
Akizungumzia hoja hizo, Mangu alisema mabadiliko ya jamii na maendeleo ya kiuchumi yamebadili mbinu za uhalifu. “Mbinu za kiuhalifu zimebadilika kiasi cha
kulilazimu jeshi pia kubadilika ili kuendana na mbinu hizo mpya.
Haiwezekani jeshi likabaki kama ilivyokuwa miaka 20 iliyopita.
“Jamii ya wakati wa Mahita ni tofauti na ya sasa.
Hata askari hawawezi kuendelea kuwa wale waliokuwapo. Mazingira na kila
kitu vimebadilika. Enzi hizo kulikuwa na uhalifu wa ulipuaji wa mabomu
na utakumbuka ilishatokea huko Arusha na Zanzibar matukio ambayo hayapo
kwa sasa,” alisema Mangu. Alisema ni vigumu kulinganisha vipindi tofauti
vya viongozi na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kutowatendea haki kwani
wanakuwa wanaongoza katika mazingira tofauti kwa kila kitu.
“Kubadilika kwa mbinu na aina za uhalifu
kunamlazimu kiongozi husika kuitikia mabadiliko hayo pia. Mimi siwezi
kutumia mbinu za Mahita kwa sababu alichokuwa anakabiliana nacho hakipo
sasa hivi.
Hapakuwa na mauaji ya albino wakati wake, hili peke yake linaonyesha jamii iliyopo ni tofauti na iliyokuwapo,” alisema. “Hata mimi nikistaafu baada ya Uchaguzi Mkuu
Oktoba atakayekuja atapata changamoto tofauti na hizi ninazokutana nazo
au walizokutana nazo watangulizi wangu,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment