Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
 amesema anashindwa kujitokeza kuzungumzia au kufanya mambo 
yanayohusiana na urais kwa kuwa Kamati ya Maadili ya CCM inamfuatilia 
kwa karibu.
Alisema hayo jana alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais
 Jakaya Kikwete wiki iliyopita akiwa Marekani ambako alielezea mafanikio
 na changamoto alizokumbana nazo wakati wa uongozi wake wa miaka 10.
Kikwete alisema: “Wakati unaingia Ikulu unakuwa na
 shauku kubwa pamoja na furaha ya ushindi, lakini hakika urais ni kadhia
 kubwa. Ukipata fursa ya kuwa rais kwa awamu mbili kama mimi nadhani 
zinatosha kabisa. Nimefanya mengi kwa nchi yangu atakayekuja ataendeleza
 nilipoishia.”
Kauli ya Lowassa inakuja ikiwa ni siku chache 
baada ya makada wengine wanaotajwa kuwania urais kupitia CCM kueleza 
maoni yao juu ya kauli hiyo ya Rais.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na 
Teknolojia, January Makamba ameshalieleza gazeti hili kuwa kauli hiyo 
inampa hamasa kwa nia yake ya kutaka kuwania urais na kwamba alitangaza 
nia hiyo huku akifahamu kwa asilimia 100 uzito wa jambo hilo akisema 
kufahamu changamoto hizo ndiyo moja ya vitu vilivyomsukuma kuchukua 
uamuzi huo.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema: 
“Kama mtu ameamua kuwania nafasi hiyo ina maana anafahamu anachokitaka. 
Tunajua ziko changamoto na namna ya kukabiliana nazo, kwa hiyo hakuna 
sababu ya kuwa na wasiwasi.”
Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla alisema: 
“Kauli kama hiyo haiwezi kumvunja mtu moyo, ari itabaki palepale tu kwa 
aliyetangaza nia. Aliyetangaza nia anataka kutoa utumishi wake kwa nchi 
yake kama mimi.”
Lowassa hajatangaza wazi nia hiyo zaidi ya kusema 
ameshawishika kuwania urais baada ya hivi karibuni, makundi mbalimbali 
kufika nyumbani kwake mjini Dodoma kumshawishi achukue fomu kuwania 
nafasi hiyo.
Miongoni mwa makundi yaliyojitokeza na kumshawishi
 pamoja na kumchangia fedha za kuchukua fomu ya kugombea urais ndani ya 
CCM ni pamoja na masheikh kutoka wilayani Bagamoyo, wachungaji wa 
makanisa ya Kipentekoste, wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na madereva 
bodaboda.
Msimamo wake hadi jana
Akizungumza jana wakati wa kuaga mwili wa 
Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk 
Mohamed Mhita nyumbani kwa marehemu Oysterbay jijini Dar es Salaam, 
Lowassa alisema: “Muda mwafaka ukifika nitatangaza nia na kuweka 
mikakati yangu wazi ili wananchi waijue. Kwa sasa siwezi kusema chochote
 kwa sababu ninatazamwa sana na chama. Ninachoweza kusema, siku 
nitakayotangaza nia, nitaeleza ni nini nitafanya kukabiliana na 
changamoto zote zilizopo Ikulu.
“Ninafahamu kuna changamoto nyingi, lakini siwezi 
kusema, subirini siku nitakapotangaza nia, nitaelezea ni kwa namna gani 
nitakabiliana na changamoto zilizopo katika ofisi hiyo nyeti nchini.”
Waziri mkuu huyo wa zamani, mmoja kati ya makada wa CCM ambao 
wameonyesha nia ya kutaka kumrithi Rais Kikwete katika Uchaguzi Mkuu 
utakaofanyika Oktoba na pia ni miongoni mwa makada sita wa chama hicho 
waliokuwa wamefungiwa kwa miezi 12 na kamati kuu kwa kufanya shughuli 
zinazoashiria kufanya kampeni mapema.
Wana-CCM wengine waliotangaza nia na wanaotajwa 
katika kinyang’anyiro hicho ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro 
Nyalandu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, Waziri 
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa 
Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja 
na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
 

No comments:
Post a Comment