Social Icons

Pages

Friday, April 17, 2015

KIMBUNGA BANDARI, TRL

Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, amewasimamisha kazi vigogo watano wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wake, Kipallo Kisamfu, kutokana kubainika kuihujumu serikali katika sakata la ununuzi wa mabehewa feki 274  ya mizigo na kuisababishia hasara ya  Sh. bilioni 230.
Wengine waliosimamishwa ni Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles; Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa; Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka. Sitta alisema baada ya kuwasimamisha vigogo hao, utafanyika uchunguzi dhidi yao kwa wiki tatu kuanzia Jumatatu ijayo.
Kufuatia uamuzi huo, Sitta amemteua aliyekuwa Mhandisi wa TRL, Elias Mshana, kuwa Kaimu Mkurugenzi wa kampuni hiyo, na kumwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, kusimamia kuundwa kwa kamati ya uchunguzi huo.
Alisema kamati hiyo itaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akishirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA) pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Sitta alichukua uamuzi huo baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi ya kamati iliyoundwa na Waziri aliyemtangulia wizarani hapo, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambayo imegundua kuwako kwa hujuma mbalimbali katika kuendesha TRL.
Kabla ya kuchukua uamuzi wa jana, Waziri Sitta aliiagiza bodi ya Wakurugenzi ya Reli kupitia taarifa hiyo na kutoa maelezo kwake juu ya suala ya ununuzi wa mabehewa hayo. Aliongeza kuwa baada ya bodi kupitia taarifa hiyo, ilibaini kuwa mabehewa mengi kati ya yaliyoagizwa nchini yalikuwa na kasoro, kuwapo kwa uzembe katika uagizaji na ufuatiliaji kuanzia kiwandani yalipokuwa yanatengenezwa na kuwako kwa uzembe katika mchakato wa kuyapokea licha ya ubovu wake.
Sitta alisema kamati hiyo iliyokuwa ikichunguza suala hilo ilibaini ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi na masharti ya mkataba wa ununuzi wa mabehewa hayo ambao ulipangwa kufanyika kwa awamu tatu, lakini malipo yalifanyika yote kwa asilimia 100.
Alisema katika makubaliano ya ununuzi, walikubaliana kufanya malipo kwa awamu kwa kuanza na asimilia 50 awamu ya kwanza, asilimia 40 awamu ya pili na awamu ya mwisho asilimia 10 ambayo ilipaswa kufanyika baada ya mabehewa hayo kufanyiwa majaribio kwa mwaka mmoja.
“Siku ya Jumatatu, Aprili 13, mwaka huu, Wizara ilishtushwa na kugundua kinyume cha taarifa za awali na masharti ya mkataba wa ununuzi wa mabehewa hayo, kwamba malipo yangefanyika kwa awamu, lakini malipo ya mabehewa hayo mabovu yamefanyika kikamilifu, yaani watengenezaji wamelipwa asilimia 100 ya fedha kinyume cha masharti ya mkataba,” alisema Sitta.
Alisema: “Mazingira ya utekelezaji wa mkataba huu yana dalili za hujuma kwa TRL na kwa nchi yetu na siyo uzembe, na pia tumebaini haikushirikisha watendaji wa chini. Jambo hili limenisikitisha sana na siwezi kumfumbia macho yeyote aliyehusika katika hujuma hii kwa sababu Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimetuweka hapa kwa ajili ya kufanya kazi kwa kutenda haki na si vinginevyo, natamani wakibainika wapelekwe mahakamani na wafungwe kabisa.”
Sitta alisema hayuko tayari kuona watu wanaifanyia serikali hujuma kama hizo na kuahidi kupambana nao bila kumwangalia mtu. Alisema katika mkataba huo, mabehewa yaliyoagizwa ni 274 na yaliyoletwa nchini ni 150 huku mengine 124 yakizuiliwa kuletwa baada ya kubainika yaliyoletwa kutokuwa na ubora unaotakiwa.
Alisema wataomba ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuangalia hatua za kuchukua kuhusiana na mabehewa hayo feki yaliyoingizwa nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luaga Mpina, hivi karibuni alisema kamati yake iliwahoji PPRA kuhusu ushiriki wao kwenye ununuzi wa mabehewa hayo na kubaini kuwa mamlaka hiyo haikushirikishwa.
Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa (CCM), alisema hali hiyo inaonyesha mambo kufanywa kinyume cha taratibu katika mchakato wa ununuzi wa mabehewa hayo na imechangia kuingizia hasara serikali. Mabehewa hayo yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya M/S Hindustan Engineering and Industrial Limited ya India ikishirikiana na kampuni moja nchini inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja ambaye amekuwa akijihusisha na biashara nyingi za kulaghai mashirika ya umma na kujipatia ukwasi wa kupindukia.
Mabehewa hayo yaligundulika kuwa mabovu baada ya kufanyiwa majaribio na baadhi kuanguka kwa kukosa ‘stability’ yakiwa relini na yaliyopokelewa na Dk. Mwakyembe Julai 24, mwaka jana, hayakupitiwa na jopo la mafundi wa TRL ili kuthibitisha ubora wake. 
 
 KIPANDE AONDOLEWA RASMI BANDARINI
Katika hatua nyingine, Sitta, alitangaza kumuondoa rasmi kwenye nafasi yake aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande kwa makosa ya utawala mbovu. Aidha, Sitta amemteua Awadhi Massawe, kuendelea kukaimu nafasi iliyoachwa na Kipande ambaye sasa atapelekwa Idara Kuu ya Utumishi kupangiwa kazi nyingine. Sitta alitangaza uamuzi huo baada ya kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza tuhuma zinazomkabili Kipande, kuanzia Februri 16 hadi Machi 20, mwaka huu.
Sitta alisema ripoti hiyo aliisoma na kushauriana na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala hayo na kukubaliana kumuondoa katika kazi ya kuongoza bandari. “Baada ya kuisoma ripoti ya kamati pamoja na kushauriana na taasisi zinazohusika, tumejiridhisha pasipo na shaka yoyote kwamba isingefaa Madeni Kipande, kuendelea na kazi hii. Hii inatokana na kudhihirika utawala wake ni mbovu, hawezi kuiongoza Bandari kwa sababu ana mabavu na maamuzi ya papara, ambayo yamesababisha manungu’niko kwa wafanyakazi,” alisema Sitta.
Alisema kutokana na utawala mbovu, mamlaka ilipata manung’uniko mengi miongoni  mwa wateja na wadau wa Bandari na kusababisha mgawanyiko kwa wafanyakazi. Kuhusu kumrejesha kazini mtumishi ambaye ameshindwa kufanya kazi kikamilifu kazi aliyopangiwa, Sitta alisema jukumu la kumpangia kazi inayofaa litafaywa na Katibu Mkuu Kiongozi. “Kipande amebainika hawezi kuiongoza Bandari, kwa hiyo tumemuondoa baada ya tume kumchunguza na tukajiridhisha kwa kushirikiana na taasisi nyingine,” alisema.
“Mamlaka ya kumpangia kazi ambayo ataweza kuifanya anayo Katibu Mkuu Kiongozi, kwa maana hii, ni sifa mbaya ya kushindwa kuongoza sekta ambayo amepewa,” alisema Sitta.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: