Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah.
Ikiwa imebakia miezi sita kufanyika kwa uchaguzi
mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, Taasisi ya Kuzuia na
Kupamba na Rushwa (Takukuru), imetoa tahadhari kwa wananchi wasifanye
makosa kuchagua viongozi wanaotoa rushwa, kwani kufanya hivyo watakuwa
wameiweka nchi rehani.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, alitoa
tahadhari hiyo jana wakati akifungua jengo mpya la taasisi hiyo
lililojengwa katika wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kwa gharama ya Sh. 1,258,457,565, ujenzi ambao ulianza Disemba mwaka juzi na kukamilika Machi
26, mwaka huu.
Alisema katika kipindi cha miezi sita ijayo Taifa litaingia katika
uchaguzi mkuu, hivyo wananchi wahakikishe viongozi watakaochaguliwa wawe
waadilifu na wenye sifa za kuliongoza Taifa na kwamba kiongozi
asiyejihusisha na rushwa ndiye atakayeleta maendeleo.
Dk. Hoseah alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu,
Takukuru imejiandaa kufanya kampeni maalum ya kuelimisha jamii juu ya
umuhimu wa kuchagua viongozi wasiojihusisha na vitendo vya rushwa. “Kila mwananchi afahamu madhara ya kukubali kurubuniwa kwa sukari,
chupa au ubwete ili kuchagua kiongozi, tunapochagua viongozi wanaotoa
rushwa tunaweka rehani nchi yetu,” alisema.
Alisema wananchi wanapaswa kufahamu athari ya rushwa katika siasa
na kupitia kampeni ya kuelimisha wananchi Takukuru inalenga kubadili
fikra za wananchi kwamba jukumu la kuzuia na kupambana na siyo la
Takukuru pekee bali ni la kila mwananchi.
Dk. Hoseah alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi
mwaka huu, kesi mpya 305 zimefunguliwa ambazo zimesaidia kuokoa fedha za
serikali Sh. bilioni 39.9. Aliongeza kuwa katika kipindi hicho zilifanyika tafiti tano zenye
lengo la kuimarisha udhibiti wa rushwa katika sekta ya mafuta na gesi.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkinga, Joseph Sura, aliishukru serikali
kupitia Rais Jakaya Kikwete kwa kufanikisha kujenga ofisi ya Takukuru
katika wilaya ya hiyo.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment