Social Icons

Pages

Tuesday, March 17, 2015

'WIKI YA MAJI' IMEPOTEZA MAANA?

Moja ya visima vinavyotumiwa na wanawake kuteka maji.
Maadhimisho ya ‘Wiki ya Maji’, ambayo hufanyika Machi 16 hadi Machi 22 kila mwaka yalianza jana nchini kote. Mwaka huu maadhimisho hayo yanafanyika kitaifa mkoani Mara na Serikali imesema kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Maji kwa Maendeleo Endelevu’. 
Pamoja na maadhimisho hayo kufanyika kitaifa katika moja ya mikoa nchini, wilaya na mikoa mingine pia huadhimisha ‘Wiki ya Maji’, lengo likiwa ni kujadili kero na changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji nchini, ambapo Serikali huelezea utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo katika Sekta ya Maji.
Sherehe za maadhimisho hayo zilianza mwaka 1988. Pamoja na maadhimisho hayo kutumia fedha nyingi kila mwaka na viongozi kutoa ahadi lukuki ambazo wananchi wengi hawaoni kama zinatekelezeka, uhaba wa maji umeendelea kuwa kero kubwa mijini na vijijini.
Kama ilivyokuwa wakati wa maadhimisho hayo miaka iliyopita, maadhimisho ya mwaka huu tayari yameshuhudia wananchi wakiuliza maswali magumu kuhusu hali mbaya ya maji nchini. Katika toleo la gazeti hili jana, wananchi waliohojiwa kuhusu maadhimisho ya ‘Wiki ya Maji” walisema maadhimisho hayo hayana faida yoyote na kuendelea kuwapo ni matumizi mabaya ya fedha za walipakodi.
Hoja ya wananchi wengi ni kwamba Serikali bado haijui ukubwa wa tatizo la maji nchini. Kwamba haijatambua kwamba tatizo hilo linachangiwa sana na ongezeko la idadi ya watu, ukuaji wa shughuli za uzalishaji viwandani, umwagiliaji, uchimbaji madini, ufugaji na sekta nyingine.
Wanasema Serikali inaonekana kujikita zaidi katika ukusanyaji wa takwimu nyingi zisizo na uhalisia kuhusu tatizo la maji, pasipo kutafsiri takwimu hizo katika muktadha wa uharibifu wa vyanzo vya maji, ubovu wa miundombinu ya kusambaza maji, mipango mibovu ya kushughulikia tatizo la maji, athari za vitendo vya rushwa na ufisadi katika kuendesha na kusimamia miradi ya maji.
Inashangaza kuona kuwa, tatizo la maji vijijini na mijini limezidi kuwa kubwa, licha ya kuwapo mikakati mbalimbali ya kulitatua. Hii ni pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2015; Mpango wa Maendeleo wa Milenia 2015; Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania; na Programu ya Maendeleo ya Kisekta iliyoanza mwaka 2007/08.
Lakini pia inashangaza kuona Serikali ikishindwa kuweka mifumo ya usimamizi wa miradi ya maji, hivyo kuwapo baadhi ya watumishi wake wanaohujumu miradi hiyo, ikiwamo iliyoanzishwa na Benki ya Dunia (WB). Kutokana na hujuma hizo, benki hiyo miaka miwili iliyopita iliamua kusimamia yenyewe udhibiti wa matumizi mabaya ya fedha inazotoa kwa miradi hiyo, lakini tatizo hilo bado halijaisha hadi leo.
Tatizo hapa ni mfumo wa ufisadi uliojikita serikalini, hivyo kuchangia kufanya ahadi za Serikali za upatikanaji wa maji kutotekelezwa.
Kwa muda mrefu sasa, limekuwapo pendekezo linaloitaka Serikali kuunda chombo kinachoitwa Wakala wa Maji, kama ilivyo kwa Wakala wa Barabara, yaani Tanroads. Haijulikani kwa nini Serikali haitekelezi pendekezo hilo, hasa tukiangalia mafanikio na ufanisi ambao Tanroads imeupata katika muda mfupi tangu ianzishwe. Tunadhani wakati umefika kwa Serikali kuona upatikanaji wa maji kama haki ya msingi kwa wananchi. Ikumbukwe kwamba suala la upatikanaji wa maji ni sehemu ya makubaliano ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia kupitia Mpango wa Malengo ya Milenia unaoratibiwa na Umoja wa Mataifa (UN).

CHANZO: MWANANCHI

No comments: