Chama cha
Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vimepata
hati zenye mashaka katika ukaguzi wa hesabu zake, uliofanywa na Mkaguzi
na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa kipindi cha mwaka wa
fedha ulioishia Juni 2013.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyopatikana jijini
Dar es Salaam jana, CAG ameainisha vigezo saba tofauti vilivyosababisha
hesabu za CCM kupata hati yenye mashaka na kueleza kuwa CCM imekosa
uhalali wa kisheria kumiliki baadhi ya mali ilizonazo. Upande wa Chadema, CAG ameanisha vigezo vitatu
vya kupata hati hiyo na kubainisha kuwa zaidi ya Sh500 milioni
zilitumika na chama hicho kununulia magari kumi bila kuidhinishwa na
bodi ya zabuni.
Ukaguzi huo wa CAG umefanyika kwa mujibu wa Sheria
namba 5 ya mwaka 1992 ya Vyama vya Siasa, iliyofanyiwa marekebisho na
Sheria namba 7 ya mwaka 2009, inayompa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za
vyama vya siasa. “Naamini ushahidi niliopata unatosha na sahihi
kutoa maoni kuhusu ukaguzi wangu,” ilisema sehemu ya taarifa ya CAG kwa
mwaka 2012/13 kwa vyama hivyo na kuongeza:
“CCM haikutenganisha thamani ya ardhi na nyumba
vilivyo na thamani ya Sh 11,422,576,990.52. Hatukuweza kupata taarifa
ya fedha ya CCM iliyokaguliwa kuhusu rasilimali zake zinazofikia
Sh 9,632,576,701.57.”
Ilibainisha vigezo vingine vya hati yenye mashaka
kuwa ni CCM kutowasilisha taarifa ya mapato yake ya fedha kutoka kwa
wafadhili mbalimbali zilizofikia Sh1,526,536,802, huku CAG pia
akishindwa kupata nyaraka za kuthibitisha matumizi na malipo
yaliyofanywa na chama hicho yanayofikia Sh6,045,438,052.
Hata hivyo, mwaka jana CCM kilitangaza kuwa CAG, amekamilisha ukaguzi wa hesabu za chama hicho zilizoishia Juni mwaka 2012/13.
CCM ilieleza kuwa ukaguzi huo ulikuwa wa hesabu
zilizoishia Juni 30, 2013 na ulifanywa kuanzia Mei 19, 2014 mpaka Oktoba
2014 na kueleza kuwa imekuwa ikikagua hesabu zake kwa wakati kila mwaka
bila kutoa wito kwa CAG kutosita kutoa taarifa kwa umma inapotokea
chama cha siasa hakitoi ushirikiano katika kutimiza matakwa ya ukaguzi
kisheria.
Kwa upande wa Chadema, taarifa hiyo ya CAG
ilisema: “Katika ukaguzi tulibaini kwamba Chadema ina zaidi ya akaunti
200 katika benki mbalimbali nchini lakini fedha zilizotajwa kuwapo
katika taarifa zake katika mwaka ulioishia Juni 2013 ni
Sh224,824.750.56 kati ya hizo Sh221,060,446.41 zikiwa ni salio katika
akaunti zake sita na kuacha salio la Sh3,764,304.15 kwa akaunti zaidi ya
194 zilizosalia:
Magari 10 yalinunuliwa kwa Sh559,031,330 bila
kuidhinishwa. Sh27,500,000 zilitumika kukodi jenereta bila kuwa na
nyaraka zinazohalalisha matumizi yake.”
Taarifa hiyo ya CAG ilieleza kuwa katika vitabu
vya risiti vya Chadema pia ilishindwa kuwasilisha kwa ukaguzi kitabu
cha risiti chenye namba 451-500 kilichotumika kukusanya Sh30,163,152
hivyo kuzuia kufanyika kwa ukaguzi.
Hata hivyo, mwaka uliopita Chadema pia kilieleza kuhusu kuwepo kwa akaunti hizo na kufafanua kwamba akaunti kuu ya chama ndiyo inatoa fedha kwa akaunti za mikoani, hivyo wanaona kwamba mgao wa fedha walioufanya ni sehemu ya matumizi yao.
CHANZO: MWANANCHI
Hata hivyo, mwaka uliopita Chadema pia kilieleza kuhusu kuwepo kwa akaunti hizo na kufafanua kwamba akaunti kuu ya chama ndiyo inatoa fedha kwa akaunti za mikoani, hivyo wanaona kwamba mgao wa fedha walioufanya ni sehemu ya matumizi yao.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment