Social Icons

Pages

Friday, March 13, 2015

NAIBU WAZIRI ATOA SIKU 14 KWA TRA


Naibu Waziri Wizara ya Fedha, Adam Malima ametoa siku 14 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukaa na wafanyabiashara nchini na kutatua kero zote za kodi zilizopo.
Alisema hayo katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara kilichowataka wafanyabiashara kueleza kero zao na Kamishna wa TRA kuzijibu. Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Johnson Minja alilalamikia kutokuwapo kwa uwazi katika ulipaji kodi na utapeli uliopo miongoni mwa kampuni za kutoa na kupokea mizigo.
Alisema wakiagiza kontena la mzigo, ushuru wa TRA unaweza kulipa Sh100 milioni huku kwa mawakala wa kutoa na kupokea mizigo ukitoa Sh40 milioni lakini unapewa risiti ya Sh12 milioni. Minja aliomba uwepo mfumo wa ulipaji kodi unaoonyesha gharama halisi za mzigo husika na siyo mfumo wa sasa unaowaumiza na uliojaa rushwa.
Mbunge wa Ziwani, Ahmed Ngwali ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo alisema, kutokana na kuwapo kwa rushwa iliyokithiri TRA haina sababu ya Kamishna, Rished Bade kuendelea kuwapo kwenye taasisi hiyo.
Ngwali alisema, Bade alikuwa akikaimu nafasi hiyo na sasa ni kamishna kamili hivyo angeweza kumaliza tatizo la rushwa TRA, lakini ameshangazwa na ongezeko la vitendo hivyo.
Alibainisha kuwa, fedha walizotegemea ziende kwenye miundombinu na afya sasa zinaenda kwenye mifuko ya watu. Kuhusu na mfanyabiashara wa Home Shopping Centre, Mbunge wa Konde, Khatibu Said alihoji kwa nini anahodhi zaidi ya asilimia 90 ya makontena bandarini na hakuna ripoti ya taarifa yoyote kuhusu hilo licha ya kamati kuiomba.
Akijibu tuhuma hizo, Kamishna Bade alisema, suala hilo alikwishalisikia na wanafanya kila njia kuwakamata lakini peke yake hawezi, lazima washirikiane. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Luaga Mpina alisema ni lazima Watanzania wote walipe kodi na wapo tayari kugombana na wakwepa kodi, kwani nchi zote zilizoendelea zilikusanya kodi.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: