
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Kufuatia makundi mbalimbali yanayojitokeza kwenda
nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kumshawishi kugombea
urais, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hatua hiyo itamfanya akose
sifa za kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari waliopo katika msafara wa Katibu
Mkuu wa CCM waliotaka ufafanuzi kuhusu hali hiyo, Katibu wa Halmashauri
Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema matendo
yanayoendelea kufanywa na Lowassa, ambaye ni Mbunge wa Monduli ni
kampeni za wazi zinazokiuka katiba na kanuni za chama hicho.
“Hivyo kuendelea nazo kunaweza kumfanya akose sifa za kugombea
nafasi ya urais. Na anachofanya Lowassa ni kuvunja kanuni na kiburi. Ni
matendo ya wazi ya kampeni. Bila shaka anajua adhabu yake. Matendo hayo
yanaweza kumpotezea sifa za kuwa mgombea kupitia CCM,” alisema Nape. Pia alisema Lowassa ni miongoni mwa wana-CCM sita waliopewa adhabu
na CCM mwaka mmoja na kwamba, mpaka sasa bado wapo kwenye kipindi cha
uangalizi wakati vikao husika vikiendelea na tathmini dhidi yao.
“Matendo yanayoendelea hivi sasa ni dhahiri kuwa ni kiburi kisicho
na maana dhidi ya CCM. Na Lowassa anajua utaratibu wa chama katika
kuwapata wagombea wake kwa ngazi mbalimbali, kuanzia udiwani mpaka
urais. Hivyo, kuendelea na matendo, ambayo yanatafsiri ya wazi kuwa ni
kampeni, ni kiburi cha wazi,” alisisitiza Nape.
Alisema kwa matendo hayo labda awe na dhamira ya kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya urais kupitia chama kingine na siyo CCM. “Ni vema wagombea wa ngazi mbalimbali wakahakikisha wanazingatia
katiba na kanuni za chama hicho ili wasiingie kwenye kundi la kutokuwa
na sifa ya kuomba ridhaa ya kugombea udiwani, ubunge na urais,” alisema
Nape.
Aliwakumbusha wagombea wote wenye nia ya kugombea kupitia CCM
kuheshimu kanuni na taratibu za kupata ridhaa kugombea kwa ngazi ya
chama. Juhudi za kumpata Lowassa jana kuzungumzia kauli hiyo ya Nape ziligonga ukuta.
Hata hivyo, Msemaji wake, Abubakari Liongo, alipotakiwa kuzungumzia
kauli hiyo ya Nape alimwelekeza mwandishi kuwasiliana na Hussein Bashe.
BASHE
Akizungumza kwa niaba ya Lowassa, Bashe alisema kinachotokea
nyumbani kwa Lowassa mjini Dodoma ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa
na Rais Kikwete wakati wa sherehe za CCM mjini Songea, mkoani Ruvuma
alipowaruhusu watu wakashawishi wanaoona wanafaa kuwania urais.
“Rais hakusema kushawishi namna gani, hakusema kushawishi kwa barua
wala kwa sms (ujumbe mfupi wa simu ya mkononi), bali alisema
wawashawishi. Na huwezi kumshawishi mtu ndotoni, utamshawishi kwa
kumfuata na kumwambia,” alisema Bashe.
Aliongeza: “Ndiyo maana Nape yuko mikoani anashawishi Watanzania
juu ya kukiamini Chama Cha Mapinduzi. Hajakaa chumbani kwake,
amewafuata. Kuna watu wanamshawishi Mwandosya, kuna wanaomshawishi
Muhongo na vyombo vya habari vinaripoti.” “Umefika wakati Nape atangaze mgombea wake wa urais hadharani,
ambaye mimi Bashe namjua, badala ya kuwatisha wana-CCM wengine kwa
kutumia kofia ya Ukatibu Mwenezi wa chama.”
“Kwa hiyo, mimi kama Bashe, ambaye ni mwana-CCM nataka tu
nimhakikishie Nape na wenzake kuwa hawana hatimiliki ya CCM. Wote
wanaCCM tuna kadi moja ya rangi moja na tunalipia ada sawasawa. Hakuna
mwanachama wa daraja la kwanza wala wa daraja la pili.”
Bashe ambaye ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, alisema kauli ya
Nape ya kumtaka Lowassa kwenda nje ya CCM, haiwezekani, kwani hajawahi
kufanya hivyo kama alivyowahi kufanya yeye (Nape). Hivyo, akasema wana-CCM wanaomshawishi Lowassa na Watanzania
wanatekeleza ushauri uliotolewa na Mwenekiti wa chama hicho, Rais
Kikwete.
“Imefika wakati sasa Nape atazamwe kauli anazoongea. Na sisi
tunaomfahamu Nape hii kawaida ya kuropoka, siyo maa yake ya kwanza.
Aliwahi kusema Kikwete akishinda mwaka 2005 atahama nchi, lakini
hajahama , akapewa na U-DC (ukuu wa wilaya) na Kikwete na hivi sasa ni
katibu mwenezi wa CCM,” alisema Bashe.
Aliongeza: “(Nape pia) aliwahi kusema mkataba wa jengo la Umoja wa
Vijana (UVCCM) ni wa kifisadi na yeye (Nape) leo anaishi kwenye jengo
hilo hilo na linakipa chama mapato.” Alisema mtu pekee, ambaye anaweza kutengua kauli ya Rais Kikwete
aliyoitoa Songea mwezi uliopita, ni yeye mwenyewe (Rais Kikwete) kwa
sababu ndiye aliyetoa maelekeo na sasa Watanzania wanayatekeleza.
Aliongeza: “Na mkumbuke mwaka 2011 kuelekea 2012, ni huyu huyu
ndiye aliyekuwa anapita kwenye vyombo vya habari akiwaambia wanahabari
kwamba, wanakwenda kumfukuza Lowassa Dodoma na leo anamhukumu kuwa
anakosa sifa na kumwambia aende nje ya CCM. “Nataka nimhakikishie kuwa Lowassa hawezi kuondoka CCM kwa sababu hajakutana na CCM barabarani.
Alisema wanaCCM wataendelea kuheshimu ushauri wa mwenyekiti wao na
kwamba, Lowassa amekuwa akiheshimu kanuni na taratibu za chama. “Na Nape na genge lake wakumbuke kwamba, Lowassa amevumilia mengi
sana. Na asidhani yeye na wenzake wana hatimiliki ya chama hiki.
Aliongeza: “Hawa wanaosema haya leo, aliyasema mwaka 2009, 2010 na
2011 kwamba Lowassa hachaguliki, hakubaliki. Nyimbo yao ilipokosa soko,
wakaja na nyimbo mpya ni fisadi, nayo ikakosa soko. Wakaja na nyimbo
mpya ni mgonjwa, nayo ikakosa soko. walimtabiria hadi kifo, nayo ikakosa
soko.
“Baada ya kuona kwamba, anaungwa mkono na makundi mengi ya kijamii
mgombea wao wa kwenye brifkesi anakosa uhalali katika umma, sasa
wanaanza kutoa kauli za vitisho na kusema watu wamenunuliwa. Kuwadhalilisha Watanzania tuna bei. Kwamba, unanunulika. Na hiyo ni
kudhalilisha utu wa Kitanzania na uwezo wa Watanzania wa kutafakari.
Alisema hakuna mtu anayenunuliwa na Lowassa, bali watu wote
wanaongozwa na akili zao katika kutafakari na kuamua na kwamba, msingi
wote wa chama chochote cha siasa, ni imani, demokrsia na haki. “Nimtahadharishe Nape sehemu yoyote, ambayo haki na demokrasia kulazimishwa kufinywafinywa huathirika,” alisema Bashe.
“Kwa hiyo, kama wanafikri njia zinazotumiwa na Watanzania
kushawishi siyo sahihi, basi atoe maelekezo ya namna ya kushawishi.
Hatutavumilia kuona haki haitendeki.” Karibu wiki mbili sasa, nyumbani kwa Lowassa, mjini Dodoma, makundi
mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakipishana na kupigana vikumbo
yakimshawishi agombee urais baadaye mwaka huu.
Awali, walianza wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Wilaya ya
Arumeru, kisha marafiki wa Lowassa, Kanda ya Kaskazini na Uongozi wa
Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania (Shiuma). Baadaye, walikwenda nyumbani kwake masheikh 50 kutoka wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
Masheikh hao walifuatiwa na wanafunzi wa vyuo vikuu sita mkoani
Dodoma, wenyeviti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, wamachinga na waendesha
bodaboda zaidi 350 kabla wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste
kutoka sehemu mbalimbali nchini kufuata nyayo hizo juzi.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment