Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ameibua
upya kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya
Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), baada ya kuhoji
sababu za vigogo waliopewa mgawo wa Sh. bilioni 73 kutoka Benki ya
Stanbic kutohojiwa wala kuchukuliwa hatua hadi sasa.
Alisema hayo jana bungeni wakati akichangia Muswada wa Sheria ya Mifumo ya Taifa wa Mwaka 2015. Mnyika alisema kutungwa kwa sheria hiyo kunatia mashaka kama
itaweza kufanya kazi vizuri kwa sababu mwaka 2006 zilitungwa sheria
mbili muhimu, ambazo hata hivyo hazijasaidia kukomesha vitendo vya
ufisadi.
Alizitaja sheria hizo zilizotungwa mwaka huo kuwa ni sheria ya
mabenki na taasisi za fedha na sheria ya BoT ya mwaka 2006, ambazo kama
zingeweza kufanya kazi vizuri zingesidia kutatua matatizo yanayojitokeza
kwenye miamala.
“Kutungwa kwa sheria kunaweza kusiwe suluhisho la matatizo haya
kwenye miamala, mfano ilikuwaje ikaruhusiwa kutolewa fedha katika Benki
ya Stanbic dola za Marekani milioni 122 kwenda katika akaunti
zisizoeleweka kwenda Austaria na Afrika Kusini,” alisema Mnyika.
Alisema pia Sh. bilioni 73 zilichotwa katika benki hiyo na
kuingizwa kwenye akaunti za watu, ambao hawaeleweki na hakuna hatua
zilizochukuliwa hadi sasa na kumekuwa na usiri mkubwa wa suala hilo. Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema uchunguzi wa kashfa ya Escrow
bado unaendelea na kwamba, taarifa zitatolewa utakapokamilika.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment