
Dk. Willibrod Slaa na mke wake Josephine Mushumbusi.
Mke wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, jana
alitoa ushahidi katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam,
kuhusiana na tuhuma zinazomkabili Khalid Kagenzi, za kutaka kumdhuru
mumewe.
Kutokana na hatua hiyo ya Mushumbusi, Dk. Slaa alisema tayari
wamefunga ushahidi kwa upande wake. Mushumbusi ambaye aliongozana na
mumewe, Dk. Slaa walifika katika kituo hicho saa 4:00 asubuhi na kutoka
saa 7:25 mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari baadaye, Dk. Slaa alisema alimsindikiza mkewe kituoni hapo kutoa maelezo akiwa shahidi yake. “Leo mke wangu alikuja kutoa ushahidi. Na maelezo yote aliyoyatoa
yameandikwa. Ameyapitia na mimi nimeyapitia. Hivyo, kwa upande wangu
ushahidi nimekamilisha. Imebaki kwao tu kwa hatua zaidi pamoja na faili
letu kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza: “Ninaomba ieleweke kwamba mke wangu ni shahidi na siyo
mtuhumiwa kama ambavyo nimekwisha kueleza. Naomba msipotoshe kama
ilivyotokea awali.”
Kwa upande wake, Mushumbuzi alisema wakati tukio linatokea,
alishindwa kutoa ushahidi alipoitwa na Jeshi la Polisi kwa sababu
alikuwa safarini, lakini baada ya kurudi alitoa taarifa kwa jeshi hilo. “Wakati tukio linatokea, niliitwa kutoa ushahidi wangu, lakini
sikufanya hivyo kwa sababu nilikuwa safari. Niliporudi niliwaambia, kwa
hiyo wakaniambia nije leo,” alisema Mushumbusi.
Aliongeza: “Maelezo ambayo nimeyatoa ni yale yale niliyosema kwenye
vyombo vya habari. Kwa hiyo yameandikwa na nimeyapitia nikajiridhisha.”
Awali, akizungumza na waandishi wa habari juu ya wito wa mke wa Dk.
Slaa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
alisema hakuwa na taarifa na jambo hilo na kwamba suala hilo
linawezekana kwa kuwa ni utaratibu wa kawaida wa utendaji kazi kwa jeshi
hilo. “Sina taarifa juu ya jambo hilo. Lakini hilo ni jambo la kawaida.
Siyo jambo kubwa sana na ni utaratibu wa kawaida wa utendaji kazi wa
polisi. Na kama amekuja kuhojiwa ni wito, ambao anaweza kuitwa mtu
mwingine yeyote,” alisema Kova.
Katika maelezo yake kwa vyombo vya habari, Mushumbusi alidai
alibaini njama za Kagenzi ambaye alikuwa mlinzi wa Dk. Slaa, kutaka
kumuua mumewe baada kukutwa na msaidizi wake wa ndani akiwa katika meza
ya chakula, ambayo hutumika kwa ajili ya kuandalia chai ya mumewe
japokuwa haikuwa kawaida yake kunywa chai katika meza hiyo.
Alisema hata hivyo, baada ya kukutwa na msaidizi wake wa kazi za
ndani, Kagenzi alishtuka na kumwaga chai na hata alipoulizwa sababu za
kufanya hivyo, hakutoa sababu za msingi. Taarifa za awali za Kagenzi kutaka kumdhuru Dk. Slaa zilitolewa na
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, mbele ya waandishi wa
habari, ambaye alieleza kuwa amekuwa akitumiwa na maofisa 22 wa vyombo
vya usalama katika miaka miwili iliyopita kufanya mipango hiyo dhidi ya
chama hicho.
Alidai Kagenzi amekuwa akitumiwa na maofisa usalama wa vyombo
hivyo kupata taarifa nyingi za Chadema na kuziwasilisha kwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM). Marando alidai mipango hiyo iligunduliwa na kitengo cha usalama cha
Chadema kupitia simu za Kagenzi na kwamba, ililenga kuiumiza Chadema
kisiasa.
Alidai katika hujuma hizo, Kagenzi amekuwa akiwasiliana na mmoja wa vigogo wa ngazi ya taifa wa CCM. Marando alidai kuanzia Desemba, mwaka jana, Kagenzi alikuwa
amekwishafadhiliwa Sh. milioni saba kwa ajili ya matumizi ya mawasiliano
ya simu kufanikisha upatikanaji wa taarifa za Chadema kupitia vikao
vyake mbalimbali ikiwamo Kamati Kuu.
Alidai alipohojiwa na Chama, Kagenzi aliwapa kitabu chake cha
kutunza kumbukumbu ambacho kinaonyesha mawasiliano kati yake na baadhi
ya maofisa wa vyombo vya usalama aliowataja kwa majina na namba za simu
zao za mikononi.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment