Social Icons

Pages

Wednesday, March 25, 2015

KINANA: SERIKALI ILILIFANYA KOSA KUBINAFSISHA MASHAMBA


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahaman Kinana. 
Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema ubinafsishaji mashamba uliofanywa na Serikali miaka ya nyuma, haukuwa na tija kwa wananchi hata kwa wakati huo.
Vilevile, CCM imedai kuwa uwekezaji huo ulilenga zaidi kuwapa haki matajiri wachache na kuwanyima maskini, jambo ambalo limesababisha kuwapo migogoro mingi ya ardhi nchini. Kauli hiyo ilitolewa juzi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana wakati akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa CCM, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.
“Haikuwa sawa hata kidogo, maana ardhi ilichukuliwa kwa watu tukaikabidhi kwa umma, hivyo baada ya kushindwa kuiendeleza tulipaswa kuirudisha kwa wenye ardhi, siyo kuwapa watu wengine ambao nao wameshindwa na hawataki kukiri kuwa wameshindwa...ni aibu,” alisema Kinana.
Katibu huyo alisema kuwa uwekezezaji wenye tija ni ule unaowanufaisha wananchi wote na siyo baadhi ya watu kama ilivyo hivi sasa. Kinana alisema mpango huo ulitekelezwa bila ya kuangalia masilahi ya wenye ardhi kwa siku za usoni, badala yake uliangalia matajiri na kampuni kubwa pekee ambazo leo hii ndiyo chanzo cha migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
Alisema kitendo cha wananchi kukodi ardhi na kulipa fedha wakati ilikuwa mali yao, kinaamsha hasira na baadhi kuanza kuichukia Serikali yao. “Hiyo ni sawa na kuendelea kukumbatia ukabaila ambao hayati Mwalimu Juliusu Nyerere alishaufukuza na sisi tumekuwa tukiupiga vita,” alisema.
Alitaja moja ya makosa ambayo Serikali inatakiwa kuyajutia ni uuzwaji wa Kiwanda cha Bia (TBL), ambacho kwa maelezo yake kilipanga kulima shayiri, lakini hadi sasa kimeshindwa na huwa kinaagiza nje ya nchi wakati ardhi wanaikodishi kwa wananchi kwa gharama kubwa.
Mbunge wa Siha, Aggrey Mwanri, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), alisema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM imetekelezwa katika jimbo lake kwa zaidi ya asilimia 100.
Mwanri alisema katika jimbo lake, vijijini vyote vina maji safi na salama, umeme kila kijiji na barabara zinapitika wakati wote.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: