Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Dk. Willibrod Slaa, akimjulia hali Askofu Josephat Gwajima,
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima aliyelazwa kwenye hospitali ya TMJ jijini
Dar es Salaam kwa matibabu.Kiongozi wa Kanisa la Ufunuo na Uzima, Askofu
Josephat Gwajima, amefunguka na kueleza kuwa bastola aliyokutwa nayo
mmoja wa wafuasi wake, ni mali yake anayoimiliki kihalali. Hata hivyo, suala la umiliki wa bastola hiyo limeibua utata baada ya Jeshi la Polisi kusema kuwa inamilikiwa kinyume cha sheria.
Akizungumza kwa mara ya kwanza siku chache baada ya kuishiwa nguvu
na kuzirai kisha kulazwa hospitalini, Askofu Gwajima alisema kuwa
aliwatuma wasaidizi wake waichukue bastola hiyo nyumbani kwake
kumpelekea hospitalini alikolazwa.
Alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana akiwa katika chumba cha
wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) kufuatia kukamatwa kwa
wafuasi wa kanisa lake 15.
Wafuasi hao wanatuhumiwa kupanga njama za kumtorosha kiongozi huyo kutoka Hospitali ya TMJ alikolazwa.
Askofu Gwajima alisema baada ya kuzagaa kwa taarifa za uvumi katika
mitandao ya kijamii kwamba amefariki dunia, aliwaita wasaidizi wake
kumlinda hospitalini hapo akihofia kuwapo kwa njama za kumuua.
Askofu Gwajima aliyekuwa akizungumza kwa shida kutokana na hali
yake ya kiafya, alisema miongoni mwa wasaidizi hao aliwatuma kwenda
nyumbani kwake kuchukua mkoba uliokuwa na silaha hiyo ndani yake
wampelekee hospitalini hapo kwa ajili ya kile alichokiita kujikinga
mwenyewe.
Aliongeza kuwa kabla ya wasaidizi wake kumkabidhi mkoba huo, ndipo
Polisi walipowavamia na kuwakamata kisha kuondoka nao ukiwa na bastola
ndani yake. “Ile bastola ni ya kwangu na ninaimiliki kihalali, hata nyaraka
zake ninazo, lakini ninawashangaa polisi hawajaja kuniuliza wala
kuniomba document (nyaraka) za umiliki wake,” alisema Gwajima kwa taabu
huku akijishika tumbo.
Kutokana na hali hiyo, Askofu Gwajima alisema kuanzia sasa hana
imani na Jeshi la Polisi kutokana na vitendo wanavyomfanyia pamoja na
wafuasi wake.
Kadhalika, Askofu huyo alisema hana ugomvi wowote na Askofu Mkuu wa
Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
bali alimtolea maneno kauli anazodaiwa kumtukana na kumkashifu kwa kwa
lengo la kumkosoa lilifuatia kutoa kauli iliyopingana na tamko
lililotolewa na Jukwaa la Kikristo Tanzania (TCF).
Askofu Gwajima alipoulizwa anasemaje baada ya Askofu Pengo
kutangaza kwamba amemsamehe, alijibu kuwa anamheshimu Askofu na hana
ugomvi bali alimkemea tu. Alisema Askofu Pengo hajaonyesha nia ya kumshtaki wala kumdhihaki bali Jeshi la Polisi ndilo linalokuza mambo.
ALIVYOPATA TAARIFA
Askofu Gwajima alisema kuwa alipokuwa jijini Arusha alisoma
matangazo na taarifa za vyombo vya habari kuwa anatafutwa na Jeshi la
Polisi kwa mahojiano. Alisema alirudi jijini Dar es Salaam na kwenda Kituo Kikuu cha
Polisi na kuonana na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova, na ndipo alipoanza kuhojiwa. “Mimi sikupigiwa simu wala sikupewa
taarifa, ila niliona matangazo katika vyombo vya habari kuwa
ninatafutwa na Polisi kwa mahojiano, ndipo nilipotii amri na kwenda
Kituo Kikuu cha Polisi,” alisema Gwajima.
CHANZO CHA KUUGUA
Askofu Gwajima akizungumza huku akihema, alisema akiwa katika mahojiano na Polisi, ghafla alisikia maumivu makali ya kichwa.
POLISI: ANAMILIKI SILAHA KINYUME
Wakati Askofu Gwajima akidai ana umiliki halali wa bastola hiyo,
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema silaha
waliokamatwa nayo wafuasi wa Askofu Gwajima, haimilikiwi kihalali na
wafuasi hao wala Askofu Gwajima mwenyewe.
Kauli hiyo ilitolewa na Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova,
wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kufahamu hatma ya
wafuasi hao waliokamatwa tangu juzi na jeshi hilo. Kova alisema hilo ni jambo jipya ambalo wamelibaini na kwamba
umiliki wa silaha hiyo ni kinyume cha sheria kwa kuwa haionyeshi mmiliki
kati ya pande hizo mbili.
“Wafuasi wa Askofu Gwajima bado tunawahoji, lakini jambo jipya
ambalo tumebaini ni kwamba silaha waliokamatwa nayo haionyeshi mmiliki
kati ya wao na Askofu Gwajima mwenyewe,” alisema Kova na kuongeza: “Kuhusiana na sababu zilizosababisha wafuasi hao kutaka kumtorosha
Gwajima bado tunaendelea kuwahoji na tunatarajia kukamilisha uchunguzi
haraka iwezekanavyo.”
Hata hivyo, Kova hakutaja sababu zilizosababisha Askofu Gwajima kuzimia, akisema daktari wake ndiye anayeweza kuelezea hilo.
LIPUMBA, SLAA WAMTEMBELEA
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, jana
alimtembea Askofu Gwajima hospitalini hapo kumjulia hali. Hata hivyo,
Prof. Lipumba alishangazwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kutotii sheria
za haki za binadamu. Alisema Askofu Gwajima alikuwa anatoa hisia zake
baada ya TCF kutoa tamko lao. Alisema Polisi wanapaswa kulaumiwa kwa kusababisha maradhi ya Askofu Gwajima.
Alisema hata yeye aliwahi kuugua ghafla akiwa mikononi mwa Jeshi la
Polisi akihojiwa na alipowaeleza hawakulizingatia. Aliongeza kwamba kwa
kuwa Kardinali Pengo ameshatangaza msamaha kwa Askofu Gwajima, hakuna
haja ya kuendelea kumshikilia.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Dk. Willibrod Slaa, alifika hospitalini hapo kumjulia hali Gwajima na
kusema Polisi ndiyo wanaopaswa kulaumiwa kwa kusababisha afya ya Askofu
Gwajima kudhoofika ghafla.
DC MAKONDA: NAMSUBIRI
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, naye alifika hospitalini
hapo kumjulia hali Askofu Gwajima na kusema kuwa jana Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Wilaya ilipanga kukutana na Askofu kwa mahojiano.
Alisema yeye (Makonda) kama Mwenyekiti wa kamati hiyo, ana jukumu la kuhakikisha kunakuwapo na usalama katika wilaya. Alisema hadi sasa kamati hiyo haina uhakika kama maneno yaliyomo
katika mitandao yalitamkwa na Askofu Gwajima na ndiyo maana wanahitaji
kumhoji.
Makonda alisema Askofu Gwajima atakapotoka hospitalini kamati hiyo
itamhoji ili kujiridhisha kama kweli maneno hayo aliyatoa mwenyewe. Alipoulizwa ikibainika ni kweli maneno hayo ni ya Askofu Gwajima
watamchulia adhabu gani, Makonda alisema Kamati ndiyo itakayoamua.
“Tutamhoji ili tujiridhishe, tutamuuliza kama maneno yale ni ya
kwake kweli, na kama anafahamu uhuru wa kusifu na kuabudu,” alisema
Makonda. Alisema ni jambo la ajabu na la aibu kwa kiongozi kama Gwajima kumtukana Askofu Pengo kwa matusi makubwa hadharani.
DAKTARI AZUNGUMZA
Daktari anayemtibu Askofu Gwajima, Dk. Fortunatus Mazigo,
aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Askofu Gwajima anaendelea vizuri na
kwa sasa anatarajia kuanza mazoezi mepesi. Alisema Askofu Gwajima anatibiwa na jopo la madaktari watatu na anaweza kuruhusiwa wakati wowote.
Hata hivyo, taarifa tulizozipata kutoka Jeshi la Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam wakati tukienda mitambozi zilieleza kuwa
uchunguzi wa kina umebaini kuwa Askofu Gwajima anamiliki bastola hiyo
hiyo kihalali.
"Uchunguzi wa kina na wa kitaalam sasa umethibitisha kwamba silaha
hiyo inamilikiwa kihalali na Askofu Josephat Gwajima. Kuhusu risasi 17
za shotgun ni kwamba Askofu Gwajima anamiliki bunduki aina ya shotgun
yenye namba 102837 ambayo inatumia risasi za aina ya hizo
zilizokamatwa," ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamanda wa kanda
hiyo, Suleiman Kova.
Iliongeza: "Kuhusu watu 15 wanaotuhumiwa kujaribu kumtorosha
Askofu Josephat Gwajima, bado uchunguzi unaendelea. Aidha, watu hao pia
wanahojiwa kuhusu suala la kukutwa na silaha na risasi zilizotajwa hapo
juu wakati wao siyo wamiliki halali za silaha hiyo na risasi hizo na
idadi iliyotajwa kwa mujibu wa sheria."
Taarifa ilisisitiza kuwa baada ya uchunguzi wa suala hilo, jalada
la kesi litapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali kabla hawajafikishwa
mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment