Social Icons

Pages

Thursday, March 19, 2015

BAADHI YA MAKOSA YANAYOJITOKEZA KATIKA BAADHI YA MAGAZETI YA KISWAHILI


MAKOSA  yanayojitokeza katika magazeti  mengi ya Kiswahili ni kutokana na waandishi kutokuwa makini na wengine kutokuwa na ujuzi wa kutosha katika sarufi na fasihi Ya Kiswahili. Hebu soma sentensi zifuatazo:
“Jukwaa la Wanarukwa lina dhumuni la kuhamasisha watu kuchangia sekta za kilimo, siasa, elimu, uchumi, utamaduni na jamii.”
Waandishi wengi huwa hawaelewi kuwa wazungumzaji wanapotumia ‘ma’ mbele ya baadhi ya maneno wanafanya makosa. Kwa mfano liko neno ‘dhumuni’ ambalo halitumiki kwa usahihi. Kwa usahihi lingekuwa neno madhumuni. Madhumuni hutumika katika umoja na wingi. Dhumuni haliko katika msamiati wa Kiswahili fasaha ila linalazimishwa na wasiokuwa weledi wa lugha hii. Ni sahihi kuandika, “Jukwaa la Wanarukwa lina madhumuni ya kuhamasisha watu kuchangia sekta ya kilimo, siasa, elimu, uchumi, utamaduni na ustawi wa jamii.” “Mtizamo wa aina hii ni batili na hauwezi kuleta matunda mazuri.”
Hapa tena mwandishi anaandika kama wanavyozungumza watu badala ya kufuata  misingi ya uandishi bora.  Kuna wakati tunasikia watu wakisema, ‘Mtizamo wangu ni tofauti na wako’. Hata hivyo, wakati wa kuandikatunapoandika neno sahihi  ni ‘Mtazamo’.  Hivyo iandikwe,”Mtazamo wa aina hii ni batili na hauwezi kuleta matunda mazuri.” “Keshokutwa Ijumaa hatma ya madiwani wanane wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliotimua na waliotimuliwa itajulikana mjini Dodoma”.
Neno keshokutwa haliunganishwi na kuwa neno moja bali ni maneno mawili tofauti. Vilevile tunaandika hatima na wala siyo hatma kama tunavyozungumza. Hapa tena tuchanganya lugha ya mazungumzo na ile ya kuandika.  Kwa hiyo kwa usahihi ingeandikwa, “Kesho kutwa Ijumaa hatima ya madiwani wanane wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliotimuliwa itajulikana mjini Dodoma.” “Umati wa watu wakifatilia juu ya maiti zilizoingizwa hospitalini hapo.”
Kwa Kiswahili fasaha kuandika  “ juu ya” ni makosa. Ilitakiwa kuandikwa kwa kutumia neno “kuhusu’ hivyo isomeke, “ Umati wa watu wakifuatilia kuhusu maiti zilizoingizwa hospitalini hapo.”
Lugha ya mazungumzo haina budi kuepukwa katika uandishi. Wako wasemaji wanaotumia ‘kufatia’ lakini wa usahihi ni ‘kufuatia’. Pia ‘zikiingizwa’ ziandikwe ‘wakiingizwa’. Kwa mila na utamaduni wa Mwafrika tunatumia maiti hawa na siyo maiti hizi. “Nadhani unakumbuka tukio la mfanyabiashara  aliyeuliwa juzi kati.”
Matumizi ya maneno ‘juzi kati’ yanakanganya na kwa kweli hayaleti maana kabisa. Ni bora angesema ‘ bila kuongeza neno ‘kati’. Kwa mfano: “ Nadhani unakumbuka tukio la mfanyabiashara aliyeuliwa juzi.
“ Watoto wake wawili  mapacha John na Anthony walikuwa wamesimamia biashara ya baba yao.” Yako mazoea ya watu wengi tena kwa asilimia kubwa ya Watanzania  hawaelewi tofauti baina ya mapacha na pacha. Kwa usahihi neno linalofaa ni ‘pacha’na siyo ‘mapacha’. Maana ya watoto pacha ni watoto waliozaliwa kutokana na mimba moja. Pia inawezekana kuwa na ndizi pacha au vidole pacha kwa maana ya watoto au ndizi kushikana. Kamwe hatusetumi watoto ‘mapacha’. “Anasema idadi inayodahiliwa ni kidogo ikilinganishwa na nchi za jirani.”
Ningependa kufafanua maana ya maneno mawili ambayo yanayotumika vibaya. Maneno haya ni dahili na sajili. Maana ya kudahili ni kudadisi jambo, kutaka kujua habari za watu kwa kuulizauliza. Kwa wanafunzi wanaoomba kujiunga na vyuo au shule, hatua ya kwanza ni kuwadahili. Baada ya kupata taarifa kamili kuwa wana sifa zinazofaa,  ndipo wanasajiliwa. Kwa hiyo kusajili ni hatua ya mwisho baada ya uchunguzi kukamilika  na hivyo kuorodheshwa kwa majina na sifa zao katika daftari la kudumu. Wanafunzi waliosajiliwa wameorodheshwa katika daftari la kudumu na hivyo huwa ni wanafunzi kamili wa chuo husika.
“ Adolphina Chialo aliyasema hayo juzi alipokuwa akifungua mafunzo kuhusu makosa ya unyanyasaji wa kijinsia.”  Kwa ufasaha maneno aliyasema hayo ingekuwa ‘alisema alipokuwa akifungua’. Kwa hiyo isomeke, “Adolphina Chialo alisema alipokuwa akifungua mafunzo kuhusu makosa ya unyanyasaji wa kijinsia.”

CHANZO: MWANANCHI

No comments: