Social Icons

Pages

Monday, January 05, 2015

ZITTO AHOJI BEI YA MAFUTA KUTOSHUKA

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji nchini (EWURA), kueleza umma kwanini bei ya mafuta hazishuki kulingana na bei ya bidhaa hiyo katika soko la Dunia.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamatiya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema katika hali ya kawaida na kwa kutumia mfumo wa kukokotoa bei wa Ewura angalau bei ya mafuta ingeshuka kwa kati ya asilimia 15 na 25. “Wananchi wana haki ya kujua na kama hakuna maelezo basi bei hizo zishuke na wananchi wafaidike na punguzo hilo,” alisema.
Alisema kuanzia Julai mpaka Desemba, mwaka 2014, bei ya mafuta ghafi imekuwa ikishuka kutoka Dola za Marekani 110 kwa pipa mpaka Dola 56 kwa pipa, ikiwa ni mporomoko wa bei wa zaidi ya asilimia 40 lakini haujaleta manufaa kwa mtumiaji wa mafuta ikiwemo wenye daladala na kupelekea nauli za usafiri wa umma kupungua. “Leo bado bei ya mafuta kwenye vituo vya mafuta ni Sh. 2029 kwa Petroli na 1909 kwa dizeli, bei ambayo ni karibia ile ile kwa miezi michache iliyopita...Ewura wanasema bei za hapa nchini hushuka baada ya miezi miwili kwa sababu waagizaji huagiza kwa ujumla mafuta mengi zaidi na hivyo kutofaidika na punguzo la bei,” alibainisha.
Hata hivyo, Zitto alisema bei zimeanza kushuka toka mwezi Julai, mwaka huu, na hatujashuhudia unafuu wowote kwa wananchi na kwamba ingekuwa bei imepanda tungeona bei zimepanda mara moja na sababu za kununua kwa pamoja huwa hazitolewi. “Ni kweli kwamba Tanzania hununua mafuta yaliyosafishwa na hivyo bei inayoshuka siyo hiyo. Lakini hao wasafishaji hununua mafuta ghafi yenye bei ndogo hivi sasa kwa hiyo ni dhahiri lazima bei za pampu zipungue,” alisema na kuongeza:
“Vile vile ni kweli kwamba thamani ya shilingi ya Tanzania imeporomoka hivyo wananchi hawawezi kuona unafuu wa bei ya mafuta kwa sababu hununuliwa kwa fedha za kigeni na kuuzwa kwa Sarafu yetu. Hata hivyo kasi ya kushuka kwa bei ya mafuta ni 40% wakati shilingi imeshuka kwa chini ya 10%.”
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: