
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil.
     
Serikali imeshindwa kuwachukulia hatua watumishi wa 
Idara ya Uhamiaji nchini waliohusika na ajira 200 za upendeleo kwa 
nafasi ya Konstebo na Koplo, licha ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa na 
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, kubaini kashfa hiyo.
Katika uchunguzi wake, kamati hiyo ilibaini kuwa walioitwa katika 
ajira hizo walikuwa ni ndugu na jamaa za maafisa wa idara hiyo. Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, 
Msemaji wa wizara hiyo, Isaac Nantanga, alisema kuwa watumishi hao 
wameshindwa kuchukuliwa hatua kwa kuwa hakuna ushahidi wa wazi 
uliopatikana kuthibitisha tuhuma za upendeleo zilizoelekezwa kwao.
Alisema ndugu na jamaa za maafisa hao walikuwa na sifa za kuajiriwa
 ndani ya idara hiyo na hivyo, kukosekana kigezo cha kuwachukulia hatua. Hata hivyo, alisema Wizara ilitoa onyo dhidi ya waliohusika na 
mchakato huo kutokana na kutoa mwanya wa kuzuka malalamiko kutoka kwa 
wananchi kuhusiana na ajira hizo. “Waliitwa kazini, walistahili kuajiriwa, kwani walikuwa na sifa. 
Pia walistahili kuomba mara ya pili, maombi hayakubagua, bali 
zilizingatiwa sifa tu,” alisema Nantanga.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa malalamiko ya kuajiriwa ndugu na jamaa
 za maafisa hao hayakuwa na msingi wowote na kwamba, onyo la wizara 
limelenga kuwatahadharisha waliohusika na mchakato huo ili tukio kama 
hilo lisijirudie tena ndani ya idara hiyo. Alisema watumishi wa umma nao pia wanalindwa na sheria ya ajira, 
hivyo, hawawezi kufukuzwa kazi kwa kutuhumiwa tu, lazima uthibisho 
uwasilishwe na mamlaka husika zijiridhishe.  
Agosti 22, mwaka jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak 
Abdulwakil, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na 
kusema baada ya waombaji wa nafasi hizo kufanyiwa usaili na kuitwa 
kazini, ziliibuka tuhuma mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya
 habari na mitandao ya kijamii. Tuhuma hizo zilihusu upendeleo wa ajira kwa ndugu na jamaa za 
watumishi wa idara hiyo, hivyo wizara ililazimika kuzisitisha na kuunda 
kamati ndogo ya watu watano ili kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai 
hayo.
Kamati hiyo ilipewa siku 10, kuanzia Agosti mosi, mwaka jana 
kukamilisha kazi hiyo, ambayo waliifanya kwa muda waliopewa na kutoa 
matokeo. “Katika uchunguzi wao, kamati imebaini kuwa baadhi ya wasailiwa 
waliolalamikiwa wamethibitika kuwa ni watoto wa ndugu au jamaa wa 
watumishi wa idara hii. “Baadhi ya waombaji wa nafasi hizi, walikuwa na umri mkubwa zaidi 
ya ule uliotajwa kwenye matangazo ya kazi (Konstebo miaka 25 na Koplo 
miaka 30), lakini walisailiwa na kuitwa kazini,” alisema Abdulwakil.
Alisema baadhi ya wasailiwa waliopata alama za juu katika ufaulu 
hawakuitwa kazini na hakuna sababu maalumu, ambazo zimetolewa, matangazo
 ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari, yalikuwa ya jumla na 
hayakuainisha viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza kidato cha 
nne na sita. Abdulwakil alisema kutokana na matokeo ya uchunguzi huo, ajira hizo zimefutwa na zitatangazwa upya. Awali, ajira hizo zilitangazwa na Kamishna wa Uhamiaji katika 
Gazeti la Serikali, Februari 17, mwaka jana na kutoa tangazo hilo kwenye
 tovuti ya wizara na idara ya Uhamiaji.
Baada ya kutangazwa ajira hizo, maombi 15,707 yalipokelewa na 
waombaji 1,005 waliitwa katika usaili. Kati yao, 200 walishinda na 
kuitwa kazini, lakini baada ya kutoa tangazo la kuitwa kazini, 
malalamiko yalitolewa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii 
kuwa walioitwa katika ajira hizi ni watoto wa jamaa na ndugu.
     CHANZO:
     NIPASHE
    
 

No comments:
Post a Comment