Umati wa wafanyabiashara wa Jiji la Mbeya wakiwa wamekusanyika katika
jengo la Mahakama ya Mwanzo jana baada ya mwenyekiti wao, Honolela
Mbogela kufikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kuzuia watumishi wa
serikali kufanya kazi ya kukusanya ushuru katika Soko la Soweto jijini
hapo.
Wafanyabiashara zaidi ya
500 kutoka masoko ya Soweto, Uhindi na Soko la Matola mjini hapa, jana
walikusanyika kwenye Mahakama ya Mwanzo mjini hapa kusikiliza kesi ya
mwenyekiti wao, Honolela Mbogela aliyekamatwa wiki iliyopita kwa tuhuma
za kuwazuia maofisa wa Serikali kufanya kazi zao.
Tukio hilo pia lilisababisha maduka yaliyo karibu na masoko hayo kufungwa kuanzia asubuhi hadi mchana.
Wakizungumza nje ya mahakama, wafanyabiashara wawili kati yao, John Katia na Jane Kapesa walisema wanaamini jiji linawaonea.
Walidai kuwa chanzo cha mwenyekiti wao kufikishwa
mahakamani ni mgogoro kati ya jiji na wafanyabiashara kutokana na
kushindwa kuzoa takataka licha ya michango mingi kutolewa na
wafanyabiashara. “Tumefika hapa kusikiliza mashtaka ya mwenyekiti.
Tunajua hana kosa, siyo yeye aliyegoma kulipa michango sokoni,” alisema
Kapesa.
“Mshikamano huu ni kuonyesha jinsi gani ambavyo
hatukubaliani na jiji wanavyowanyanyasa wafanyabiashara na kuwanyima
haki zao za msingi za kufanya shughuli zao.” Kutokana na wafanyabiashara hao kujaa mahakamani, iliwalazimu polisi kuimarisha ulinzi.
Sambamba na hali hiyo, Mbogela alipanda kizimbani na kusomewa mashtaka ya kuzuia watumishi wa Serikali kufanya kazi. Ilidaiwa mbele ya Hakimu Ubaswege Marthew kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Januari 10, mwaka huu katika eneo la Soko la Soweto. Anatuhumiwa kuwazuia watoza ushuru kufanya shughuli zao, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi. Mshtakiwa alikana kosa na hakimu aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment