Social Icons

Pages

Monday, January 05, 2015

NYALANDU: TUNAENDELEA KULETA HELKOPTA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema, serikali itaendelea kuleta ndege nyingine aina ya helkopta baada ya ile ya awali kupata ajali. Waziri Nyalandu alisema lengo ni kuimarisha usalama wa wanyama ndani na nje ya maeneo ya hifadhi na hivyo  kukuza sekta ya utalii nchini.
“Bado tunaendelea kuongeza ndege nyingine nchini baada ya ile ya kwanza kupata ajali...pia kuwafundisha marubani,” alisema. Katika kuhakikisha kunakuwapo maboresho makubwa katika kuikuza sekta hiyo, Waziri Nyalandu alisema, wizara yake ina mpango wa kuwaleta watengeneza filamu kutoka shirika la filamu la Hollywood nchini Marekani. Kwa mujibu wa Nyalandu, wataalamu hao watatengeneza filamu inayolenga kuitangaza Tanzania na rasilimali zake  na kisha kurushwa kwenye mashirika ya kimataifa ya utangazaji.
“Tutatengeneza sinema kwa kuwatumia wataalamu kutoka shirika la kutengeneza filamu la Marekani la Hollywood, ili tutangaze Tanzania,” alisema. Alisema kwa sasa sekta hiyo inapokea watalii takribani milioni 1.2 na kwamba mipango ya wizara ni kuongeza idadi hiyo hadi  kufikia watalii milioni mbili mwaka 2017 na milioni 17 baada ya miaka mitano.
Aliongeza kuwa matukio ya ujasusi katika nchi jirani na kuibuka kwa ugonjwa wa ebola, zilikuwa ni baadhi ya changamoto katika eneo hilo la utalii nchini. Alisema changamoto nyingine ni kwa watendaji kufanya kazi kwa mazoea hivyo wizara yake itaendelea kufanya maboresha ya mfumo wa kiutendaji.
Pia kuuawa kwa wanyama wanaokuwa nje ya maeneo ya hifadhi ilikuwa ni moja ya changamoto hizo. “Changamoto ya ujangili bado hasa kwenye maeneo yaliyoko nje ya hifadhi. Pia watu kufanya kazi kwa mazoea… lakini ninachokifanya sasa ni kujitahidi kubadili mfumo wa utendaji…ni lazima tukubaliane na mabadiliko,” alisema Nyalandu.
Katika kukabiliana na hilo, alisema kuna vifaa maalumu ambavyo maafisa wanyama pori kuvitumia kwenye hifadhi kuhakikisha usalama wa wanyama unakuwapo muda wote.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: