Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Siku chache baada ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na
Madini, Prof. Sospeter Muhongo, kujiuzulu nafasi yake kutokana na
kashfa ya uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, Chama cha
NCCR- Mageuzi kimetaka waliohusishwa na kashfa hiyo kufikishwa
mahakamani mara moja.
Kimewatajwa baadhi ya watu hao kuwa ni Profesa Anna Tibaijuka
ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mbunge wa
bariadi Magharibi, Andrew Chenge; Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja; aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taneesco, Victor Mwambalaswa;
Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona; Mbunge mstaafu wa
Sumbawanga, Paul Kimiti James Rugemalira aliyegawa fedha hizo.
Pia kimemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kama msimamizi mkuu wa
shughuli za Serikali bungeni ajipime na awajibike au awajibishwe
kutokana na uzembe wa kushindwa kuthibiti sakata hilo. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Mosena Nyambabe, alisema wameshuhudia
maofisa wa ngazi ya chini waliohusika katika kashfa hiyo wakifikishwa
mahakamani huku viongozi hao wakubwa wakiendelea kutesa mitaani.
Nyambabe alisema kama ambavyo Bunge liliazimia kuwajibika ama
kuwajibishwa kwa viongozi wote waliohusika katika sakata hilo kwa namna
moja ama nyingine ni vema wote wakafishwa mahakamani. “Tumefurahishwa na hatua ya viongozi waliohusika na kashfa ya
Escrow kuwajibika, lakini haitoshi tu kujiuzulu pekee, bali pia
wanatakiwa wafikishwe mahakamani kama ambavyo bunge liliazimia kwamba
wawajibishwe kisiasa na kisheria,” alisema.
Aliongeza: “Kwa nini maofisa wadogo waliochukua fedha hizo
wamefikishwa mahakamani halafu hawa vigogo bado wanatesa mitaani,
hatukubali, tunataka sheria ichukue mkondo wake na wao wachukuliwe
hatua mara moja kama wenzao.” Aidha, Nyambabe alisema NCCR-Mageuzi kinaamini kwamba wakati
mchezo huo unachezwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kinafahamu.
Alisema wanaamini kwamba ipo hali ya kulindana ndani ya chama hicho
hata kama wanafahamu uozo unaofanywa na baadhi ya wanachama wao na
kwamba bila Wapinzani kufichua uozo huo wa kashfa ya Escrow suala hilo
lisingejulikana. “Kama wapinzani wasingeuanika bungeni usingesemwa wala kujulikana, wana-CCM waliamka baada ya wapinzani kupiga makelele,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment