Social Icons

Pages

Wednesday, January 28, 2015

MITANDAO YA KIHALIFU HATARI KWA USALAMA, ASEMA CHIKAWE

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, ametahadharisha kuongezeka kwa mitandao ya uhalifu wa kimataifa na ugaidi, akisema kama haitadhibitiwa mapema na vyombo vya dola, inaweza kujipenyeza katika sekta mbalimbali ikiwamo kufadhili watafuta uongozi wa nchi.

Pia, amelitaka Jeshi la Polisi nchini kupanga mikakati thabiti ya kuhakikisha amani na utulivu uliopo nchini unaendelea kuimarishwa hasa wakati wa kampeni na upigaji kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa. Alitoa tahadhari hiyo jana mjini hapa alipokuwa akifungua mkutano Mkuu wa mwaka wa maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi nchini.
Alisema uhalifu wa kimataifa hutumia fedha chafu zinazopatikana kwa njia haramu na kuwa ni hatari kwa usalama wa taifa kutokana na kwamba kutokana na uwezo mkubwa wa kifedha wa mitandao hiyo, ni rahisi kujipenyeza hata katika uongozi. “Hawa watafuta uongozi kwa kutumia fedha zao ili kujiwekea kinga na kujenga misingi ya kuendeleza uhalifu wao, ni hali inayohatarisha utawala wa sheria, mfumo wa demokrasia na upatikanaji wa haki nchini,” alisema Chikawe.
Alilitaka Jeshi hilo kutovumilia watumishi wa aina hiyo na lisisite kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria mtumishi atakayejiingiza katika ushirikiano na mitandao hiyo hiyo ambayo inahatarisha amani na usalama wa nchi. Kuhusu kuibuka kwa makundi ya kihalifu kama vile ‘Panya road’, Chikawe alisema hali hiyo haikubaliki na kulitaka Jeshi hilo kutimiza wajibu badala ya kusubiri matukio yatokee. “Wananchi wa Dar es Salaam wanahoji inakuwaje baada ya taharuki ya ‘Panya road’ Jeshi la Polisi linakamata watu zaidi ya 1200?Je Jeshi la polisi lilikuwa linawafahamu kabla...Wananchi wanalituhumu Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuwa baada ya kuwakamata vijana wengi lilifanya mradi kwa kauli ya kuwa kuingia bure kutoka kwa pesa,” alisema bila kufafanua.
Alibainisha kama malalamiko hayo ni ya kweli baadhi ya askari wasiowaaminifu wametumia fursa hiyo kujinufaisha na kuwanyanyasa wananchi. Aliaagiza hatua stahiki zichukuliwe endapo  ikithibitika kuwa kuna ukiukwaji wa maadili mema ya Jeshi la polisi.
Kuhusu kuvamiwa kwa kituo cha Polisi Ikwiriri, mkoani Pwani, Chikawe alisema serikali imesikitishwa sana na tukio hilo na IGP amemhakikishia polisi hawatalala mpaka watuhumiwa wote waliofanya unyama huo wapatikane na kufikishwa katika mkono wa sheria.
Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu, alisema pamoja na mambo mengine Jeshi la Polisi inaweka mkakati kwa kushirikiana na vyama vya siasa, Msajili wa vyama na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kudhibiti matukio ya uvunjifu wa amani katika uchaguzi mkuu ujao na upigaji kura ya maoni ya Katiba.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: