
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, amesema nchi inapita katika kipindi cha majaribu na
mitihani mikubwa inayotokana na mmomonyoko wa maadili katika ngazi zote
kuanzia familia, shule, ofisi na serikalini.
Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya
Kanisa la Anglican, Dayosisi ya Dar es salaam yaliyofanyika katika
kanisa kuu la St. Albans jijini Dar es Salaam.
Membe alisema majaribu hayo ni pamoja na tatizo la ufisadi, ukatili
dhidi ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi,umaskini na kupotea
uvumilivu wa kidini na kisiasa.Alisema Watanzania wengi wamefika hatua ya kukata tamaa na kupoteza matumaini na kwamba changamoto hizo zinawasumbua pia viongozi wa dini zote. “Waumini wamekata tamaa na kupoteza hofu ya Mungu na wengi sasa wanaokimbilia kwenye nguvu za giza, uganga na unajimu.Tunahitaji kutoka hapa. Tunajiuliza wote, tunatokaje? Alihoji Membe.
Akizungumzia kuhusu ufisadi, alisema kamwe hatawaonea wivu wala rushwa na mafisadi wanaoihujumu nchi kwa fedha chafu. Alisema jukumu la kuzuia ufisadi ni la kila mtu katika kila eneo lake na kwa nafasi yake. Membe alisema anamshukuru Mungu kwa kuwa yeye si mpenda rushwa na kwamba mafisadi na wala rushwa wamekuwa wakimchukia kutokana na msimamo wake huo. "Mimi sipendi rushwa na ufisadi. Nashukuru Mungu kuwa rushwa, ufisadi na mafisadi hawanipendi zaidi." Alisema.
"Siyo jukumu la viongozi pekee au chama fulani pekee kupambana na rushwa maana mafisadi wako kote katika ngazi zote. Naamini, mwaka huu, wengi wetu tukisema hivyo, tukasimama katika mstari huo, na tukaenenda hivyo, ufisadi hauwezi kutushinda."alisema. Membe alilipongeza Kanisa la Anglican Tanzania kwa kusimama kidete kupinga ndoa za jinsia moja (ushoga) hata pale makanisa mengine ya Anglikana duniani yalipoamua kufanya hivyo. "Mlinipa faraja kubwa, maana kupitia kwenu ile sauti ya Serikali, na sauti ya Watanzania kukataa shinikizo kutoka nje ya nchi la kukubali ndoa za jinsia moja, " alisema Membe.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Anglican nchini, Dk. Valentino Mokiwa, aliwataka vijana kutokubali kutumika na mafisadi na wenye hela kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili ya kanisa. "Ni hi Vijana si mbwa ama punda kiasi Cha kukubali kutumika viably a na wenye fedha na mafisadi. Lazima kijana wa sasa ajitafakari na kuona wajibu wake katika jamii, " alisisitiza Askofu Mokiwa.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment