
Kiongozi wa LRA Joseph Kony.
Katika kipindi cha miaka mitatu, vikosi vya Umoja wa Afrika vimekuwa
vikiwasaka waasi wa LRA katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, na ingawa
vikosi hivyo vimepata mafankio kadhaa, kundi hilo linaendelea kueneza
hofu.
Magari ya kijeshi yanayotimua vumbi kutoka barabara chafu karibu na
kijiji cha Nzako katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hayaonekani
kuwashangaza wenyeji walioko kandoni mwa barabara hiyo wakitafuta kivuli
cha miti. Vikosi vya wanajeshi wa Umoja wa Afrika viko katika eneo hilo
la kusini mwa nchi, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,
kuwalinda raia kutokana na mashambulizi ya kundi la Lord's Resistance
Army, LRA.
Wanajeshi hao - wengi wao kutoka Uganda, Jamhuri ya Congo na Sudan
Kusini - wakisaidiwa na Marekani wamekuwa wakijaribu kuwasaka masalia
wa LRA tangu mwaka 2012 katika eneo hilo lenye misitu mikubwa. Bado
kunaaminika kuwepo na mamia kadhaa ya wapiganaji wa kundi hilo,
lililoorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani, ingawa wanajeshi wa
Umoja wa Afrika wameripotiwa kupata mafanikio muhimu.
Kukamatwa kwa makamanda wake
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, vitendo vya utekaji
nyara katika vijiji vya eneo hilo vinavyofanywa na LRA vimepungua kwa
nusu katika miaka ya karibuni. zaidi ya hayo, makamanda sita wa LRA
wamekamatwa, wa karibuni zaidi akiwa Dominic Ongwen, moja wa makamanda
muhimu zaidi, ambaye atakabidhiwa kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu
ya ICC mjini The Hague, nchini Uholanzi.
Pamoja na hayo, bado hakuna dalili ya kukamatwa kwa kiongozi wa kundi
hilo Joseph Kony. Na wala haijulikani wazi amejificha katika nchi gani
pamoja na wafuasi wake waaminifu. Kilicho wazi ni kwamba waasi wa LRA
waliojihami kwa silaha nzito huibuka mara kwa mara kutoka msituni na
kufanya mashambulizi kawenye vijiji, hasa katika Jamhuri ya Afrika ya
Kati. Waasi hao wamekivamia kijiji cha Nzako mara tatu.
Mbinu za LRA zawachanganya AU
Kiongozi wa kijamii wa kijiji hicho Mahmad Ganda, anasema LRA walivamia
soko la kijiji, wakachukuwa kila kitu, wakauwa watu kadhaa wakiwemo
wanajeshi waliowekwa kutoa ulinzi. Msemaji wa vikosi vya Uganda katika
Jamhuri ya Afrika ya Kati Robert Kamara, anasema LRA inajaribu
kujinusuru kwa njia zozote zile, na bado wana uwezo wa kuendesha
operesheni zao katika mazingira magumu zaidi. LRA wana uwezo wa kuchuma
matunda, kulina asali, kuvua samaki na kupata nyama kutoka msituni.
Kamara anasema ni vigumu sana kwao kuwafuatilia. " Njia pekee ni
kutembea kwa miguu na kuishi msituni kama wanavyofanya kwa wiki kadhaa,
anasema huku akiangalia msitu mzito kutokea dirisha la helikopta ya
kijeshi. Mwaka 1987, LRA ilianza kufanya ukatili kaskazini mwa Uganda,
ikiwateka maelfu ya watoto kwa miaka kadhaa na kulwalazimisha kuwa
wanajeshi.
Hofu ndiyo zana yao kuu
Ongweni alikuwa moja wapo. Alitekwa na waasi akiwa na umri wa miaka 10
na kuingizwa jeshi, na kufanya juhudi hadi kufikia ngazi ya kamanda wa
juu katika kundi hilo. Mwaka 2005, kundi hilo liliondoka nchini Uganda,
na tangu wakati huo limekuwa likifanya utekaji nyara katika eneo la
mpakani mwa DRC, Sudan Kusini na Kongo. Karibu watu milioni mbili
wameyakimbia makaazi yao katika eneo hilo. Hofu ndiyo zana yenye nguvu zaidi inayotumiwa na waasi hao, ambao
wanahalalisha vita vyao kwa misingi ya dini. Katika eneo linalozunguka
Obo, mbali kabisaa kusini-mashariki na Jamhuri ya Afrika ya Kati, karibu
makaazi yote yameisha, na wakulima wanapanda mazao katika maeneo
yanayolindwa na Umoja wa Afrika tu.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment