
Meya wa Jiji, Dk Didas Masaburi
Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imebaini ufisadi wa zaidi ya Sh1.7
bilioni katika Jiji la Dar es Salaam, hivyo kuitaka Wizara ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kufuatilia kashfa hiyo na
kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote waliohusika.
Mbali na hilo, LAAC imeikataa taarifa ya
Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kabwe kuhusu makusanyo ya fedha za maegesho
ya magari kwa vile haiendani na uhalisia wa idadi ya magari yaliyopo
jijini. Mwenyekiti wa LAAC, Rajabu Mbarouk wakati
akikutana na watendaji wa jiji jana, alisema fedha hizo zimetumika
kuendesha mradi hewa wa kujenga machinjio ya kisasa yenye dalili za
kifisadi.
Mjumbe wa kamati hiyo, Dk Omary Nundu alisema:
“Inashangaza, mradi haujaanza lakini tayari meneja kapatikana na kalipwa
fedha zote.” Aliongeza: “Tunataka kujua mchakato ulifanyikaje
na nani aliyehusika, lakini kusema Sh1.7 bilioni mlichanga na zote
zimetumika halafu tunaambiwa hoja hii ifungwe, itakuwa ngumu.” Akizungumzia mradi huo, Meya wa Jiji, Dk Didas
Masaburi alisema: “Jambo hili tunalolizungumza lilitokea miaka 10
iliyopita, lakini kwa kuwa mmetuomba tukae basi tutazingatia maelekezo
yenu.”
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za
Jamii, Margreth Sitta alisema kamati hiyo imekutana na Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Stadi na kuhakikishiwa kuwa Serikali itaanzisha
Tume ya Ajira ya Walimu kuanzia Julai mwaka huu.
Alisema kwa muda mrefu walimu wamekuwa
wakilalamika kutokana na kusimamiwa na wizara zaidi ya moja, jambo
ambalo limekuwa likileta usumbufu. Wakati huohuo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk
Didas Masaburi amesema yuko tayari kuachia madaraka kama itabainika kuwa
asilimia 21 ya hisa za jiji hilo zilihamishwa kwenda Kampuni ya Simons
Group inayoendesha Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Alitoa kauli hiyo jana baada ya mjumbe wa Kamati
ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kangi Lugola kudai ana vielelezo
kamili vya mauziano hayo vilivyopo Mamlaka ya Usajili wa Biashara
(BRELA).
“Suala hili limenilazimu kwenda BRELA kujua
uhalali wake. Nimekuta taarifa zikionyesha hisa zimehamishwa kutoka jiji
kwenda Simons Group,” alisema. “Kama kuna ukweli kwenye madai hayo ya Kangi niko tayari kujiuzulu. Nitakuwa wa kwanza kuwajibika.” Awali, mjumbe wa kamati hiyo, Munde Tambwe alisema mikataba kati
ya kampuni hiyo na jiji una utata, huku akifafanua kuwa Simons Group
inaitumia Kampuni ya Uda bila kulipa chochote. Mjumbe wa kamati hiyo, Israel Natse alisema tangu LAAC ianze kufanya ziara Dar es Salaam, wamegundua kuwapo ujanja mwingi.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment