Social Icons

Pages

Saturday, January 17, 2015

KILANGO, DC KADEGHE WAZOZA VITA YA UBUNGE

Vita ya ubunge baina  Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi (DC)   Dk. Michael Kadeghe, imezidi kufukuta Kilango akitishia kumshitaki DC huyo.
Akizungumza na wanahabari jana , Kilango anadai  kuwa atamfikisha kwenye  Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kwa madai ya kupeperusha bendera ya taifa kwenye gari lake akiwa  wilayani Same huku akijua ni kosa.
Mbunge huyo wa Same Mashariki alisema atamfikisha Dk Kadeghe kwa Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma Jaji mstaafu, Hamis Msumi. Kilango alidai  DC huyo  akiwa na gari lake lenye namba STK 3764 aina ya Land Cruiser, alifanya kosa hilo kwa minajili ya kuwatisha wananchi wa jimbo lake ili wamwamini anafaa kuwa mbunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao.
Kadeghe anadaiwa kuanza ‘kucheza rafu’ za uchaguzi mkuu ujao kwa kutishia harakati za Kilango kutetea kiti chake jimboni humo. Mkuu huyo wa Wilaya alidaiwa kuendesha vikao vya ndani vya siri vya Chama cha Mapinduzi (CCM) kabla ya wakati kwa nia ya kutaka kumng’oa ubunge Kilango.
“Nitakutana na Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma ili kutafuta haki. Haiwezekani wewe siyo DC wa Same upeperushe bendera kwenye eneo ambalo huliongozi?
Kilango alisema ingawa Kadeghe hana ubavu wa kumng’oa kwenye kiti chake,  hapaswi kumkejeli katika kipindi ambacho anatekeleza ilani ya uchaguzi ya chama chake kuelekea uchaguzi mkuu . Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Mbozi , alipoulizwa kuhusu madai hayo ya Kilango, alipinga kufanya vikao vya siri vya chama kwa ajili ya kuendesha kampeni ya kumng’oa kwenye ubunge. Pia bendera hiyo ilikuwa ikifanyiwa usafi na wala haikuwa inapepea kama ambavyo inadaiwa.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Kilango alimshinda Dk. Kadeghe kwa kura 389 dhidi ya kura 46 alizoambulia kwenye uchaguzi ndani wa CCM na mwaka 2010, Kilango pia  alimpiga mwereka mpinzani wake huyo kwenye kura za maoni kwa kupata kura 7,900 dhidi ya kura 2,200 alizoambulia Kadeghe.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Same, Herman Kapufi alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu mgogoro huo, alisema taratibu zipo wazi kwamba Mkuu wa Wilaya akishavuka nje  ya mipaka yake ya utawala haruhusiwi kupeperusha bendera.
Alinukuu vifungu vya madaraka ya Ukuu wa Wilaya na  Sheria ya Tawala za Mikoa namba 19 ya mwaka 1977 na Sheria ya Serikali za Mitaa namba 7 na 8 za mwaka 1982, vinamkataza Dk. Kadeghe kupeperusha bendera kwenye wilaya asiyoiongoza.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: