
Rais Jakaya Kikwete, ‘amewaangukia’ viongozi wa dini
nchini akiwaomba kusaidia kudhibiti makundi ya wagombea urais
yaliyoanza mbio za kujipitisha kwenye nyumba za ibada kunadi sera zao
ili kujisafishia njia ya kwenda Ikulu.
Amesema iwapo viongozi hao wa dini watakataa kuhadaiwa na wanasiasa
hao ili wawape nafasi ya kujitengenezea kete ya kisiasa ya kutekeleza
dhamira zao kupitia nyumba za ibada, watalisaidia taifa kupata kiongozi
mzalendo na mwadilifu.
Rais Kikwete aliyasema hayo kupitia hotuba yake iliyosomwa jana na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapteni mstaafu, George
Mkuchika, kwenye ibada maalum ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu
mpya wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo. Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaoatarajia
kufanyika Oktoba, mwaka huu, kuwaruhusu wanasiasa kunadi sera zao ndani
ya nyumba za ibada ni kuruhusu tatizo.
“Rai yangu kwenu viongozi wote wa dini, Mheshimiwa Baba Askofu,
Mkuu wa Kanisa la KKKT (Malasusa), msiwakaribishe tena wanasiasa kutumia
maeneo ya kanisa kwa shughuli za kisiasa. Na ninyi wanasiasa, acheni
kuchanganya dini na masuala ya kisiasa,” alisema.
Wakati Mkuchika akisoma hotuba hiyo ya Rais Kikwete, yalikuwapo
kanisani hapo makundi matatu ya wanasiasa wakongwe wanaotajwa kutaka
kuwania urais katika uchaguzi huo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Hao ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, aliyetangaza rasmi kugombea urais wiki chache zilizopita. Wengine wanaotajwa ambao hawakuwapo katika hafla hiyo, ni Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja. Mwingine aliyejitangaza ni Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamis
Kigwangalla na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba. Naye Naibu Waziri wa Fedha, Mwingulu Nchemba, alikaririwa na vyombo
vya habari wiki iliyopita akisema masheikh na maaskofu wamemuomba
awanie urais katika kinyanyangi'ro hicho.
KASHFA YA ESCROW
Kwa upande mwingine, Askofu Shoo alisema maaskofu wanahuzunishwa na
taarifa za kuenea kwa ufisadi mkubwa miongoni mwa viongozi na watumishi
wa serikali. Alisema kinachowasikitisha zaidi ni jeuri na ukakamavu wa hao waovu
wachache waliokosa uzalendo, akitolea mfano wa kashfa ya uchotwaji wa
zaidi ya Sh. bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kwa upande wake, Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa, alihitimisha
ibada hiyo kwa kumweleza mwakilishi wa Rais Kikwete (Mkuchika), kwamba
katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ni lazima serikali
ihakikishe daftari la kudumu la wapigakura linapatikana kwa wakati
stahiki.
“Tuna mambo mazito yanayolikabili taifa kwa sasa. Upo uchaguzi mkuu
mbele yetu na kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa, lakini hatuwezi
kuzungumza yote hayo kama ninyi mtabana kutoa nafasi ya kuboresha
daftari la kudumu la wapigakura. Siyo ufahari watu wachache kupewa
nafasi ya kupiga kura halafu ukawanyima fursa hiyo wengine kwa maana
amani ni chimbuko la haki, hakuna jinsi lileteni,” alisema Askofu Dk.
Malasusa.
Sherehe hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Chama
cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia. Wengine ni Gavana wa zamani wa BoT, Edwin Mtei, Mbunge wa Arusha
Mjini (Chadema), Godbless Lema, Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel
Natse, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa
Moshi Vijijini (CCM), Dk. Cyril Chami na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment