Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akifungua kikao cha Kamati Kuu ya
CCM, mjini Unguja, Zanzibar Kushoto ni Makamu wake (Zanzibar), Rais
wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein.
Wakati Kamati Kuu ya
CCM, ikieleza kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wake walio katika
dhamana ya kisiasa kukumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow,
adhabu kali zitachukuliwa dhidi ya wagombea urais sita walioadhibiwa
mwaka jana endapo walikiuka masharti ya adhabu zao.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema jana baada ya Kikao cha Kamati Kuu kilichokutana Ofisi Ndogo ya
CCM, Kisiwandui kuwa kamati hiyo imeagiza Kamati Ndogo ya Maadili
kushauri na kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi watakaokuwa
wamekiuka adhabu husika.
“Itakumbukwa kuwa kuna makada sita wa CCM
waliopewa adhabu kwa kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato
wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea urais, watamaliza muda wa adhabu zao
Februari mwaka huu. “Baada ya muda wa adhabu zao kuisha, itafanyika
tathimini kuona kama walizingatia masharti ya adhabu zao na kama kuna
ambao watakutwa hawakuzingatia mashariti ya adhabu zao, wataongezewa
adhabu,” alisema Nape.
Vigogo sita waliopewa adhabu ni; Waziri Mkuu
Mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira. Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Nape alisema kamati ndogo ya maadili inayoongozwa
na makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula itatoa ushauri kwa
ngazi za juu za CCM na ikibidi hatua nyingine za kinidhamu na kiatiba
zitafuata.
Makamba asema “Binafsi sina wasiwasi, kwanza mwanzoni sikustahili kuwemo na hata sasa sina shaka kama kuna lolote nililofanya kinyume.”
Alisema kuwa wanaopaswa kuwa na wasiwasi ni wale
wanaogawa pesa. “Sisi wengine hizo fedha hatuna...ninaamini wapo wengine
ambao hawapo kwenye orodha lakini wamekiuka maadili. Nilitarajia na wao
watahojiwa,” alisema Makamba.
Sumaye akumbushia rufani
Akizungumzia hatua hiyo ya Kamati Kuu, Sumaye
alisema: “Mimi siwezi kujitathmini mwenyewe, tusubiri hiyo kamati tuone,
sijui watasema nini na wala sielewi kosa langu na ndfiyo maana nilikata
rufani. “Labda watatumia muda huo kujibu pia rufani yangu. Sina mengine ya kusema.”
Sakata la Tegeta Escrow
Sakata la Tegeta Escrow
Akizungumzia kashfa ya uchotaji fedha katika
Akaunti ya Tegeta Escrow, Nape alisema: “CCM kimesikitishwa na sakata
hili. Baada ya kulijadili kwa muda mrefu na kwa kina Kamati Kuu imeamua
yafuatayo;-
“Pamoja na yale ambayo yameshatekelezwa na
serikali, Kamati Kuu imeitaka Serikali na vyombo vinavyohusika kuendelea
kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu suala hilo. “Kamati Kuu imewataka wote wanaopewa dhamana
wajenge utamaduni wa kuwajibika kwa dhamana zao, na wasipowajibika
waliowapa dhamana wachukue hatua za kuwawajibisha. “Pia, imeiagiza Kamati Ndogo ya Maadili kuchukua
hatua za kimaadili kwa wale wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili
kwenye sakata la Escrow na wako kwenye vikao vya uamuzi vya chama. Kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili kitafanyika Jumatatu ijayo, Januari 19 kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo,” alisema Nape.
Wanaotuhumiwa na uchotwaji wa fedha hizo ni pamoja
na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, Ngeleja na Waziri wa
zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka. Mwingine aliyeko katika tuhuma hizo ni Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Profesa Tibaijuka
ameshavuliwa wadhifa wake. Akizungumzia hatua ya Kamati Kuu, Profesa
Tibaijuka alisema: “Kama wameamua tufikishwe Kamati ya Maadili, basi
nitasubiri taarifa rasmi ili ajue kwa kina uamuzi huo. “Sikuhudhuria kikao, sina la kuchangia na kwa sasa nasubiri nipate taarifa” alisema Tibaijuka ambaye ni Mbunge wa Muleba Kusini.
Prof Tibaijuka ambaye hakuhudhuria mkutano huo,
alisema pia kuwa viongozi waliowekwa viporo sakata la Escrow, ni vyema
mamlaka ya husika ikashughulikia suala hilo. Alipotafutwa Ngeleja kuzungumzia suala hilo alisema, “Kwa sasa
sipo kuzungumzia suala hilo kwa sababu linashughulikiwa na vyombo
husika.” Kwa upande wake Chenge alisema kwa ufupi kuwa hapendi kulizungumzia suala hilo.
Kamati za Bunge
Sakata hilo la Akaunti ya Tegeta Escrow
lililodakwa na kamati hiyo ya CCM pia lilizusha mjadala mzito wakati wa
vikao vya Kamati za Bunge, Katiba na Sheria inayoongozwa na Ngeleja na
ile ya Bajeti chini ya Chenge. Wenyeviti hao wa kamati tatu za Bunge waliotajwa
kuhusika kwenye kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow na kutakiwa kuvuliwa
nyadhifa zao, wamezua mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wa kamati zao
kutokana na kuibuka kwa madai kuwa wamehukumiwa bila kuhojiwa.
Mvutano huo ulisababisha baadhi ya wajumbe wa
kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambayo inaongozwa na Ngeleja
kubishana kuhusu suala hilo wakati wakiwa ndani ya kikao. Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati hiyo
zilieleza kuwa watuhumiwa hao, kutoitwa na kuhojiwa na badala yake
kuhukumiwa moja kwa moja si jambo la kupongezwa, kwamba suala hilo
huenda likachelewesha utekelezaji wa kung’olewa kwa wenyeviti hao. Akizungumza na gazeti hili mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema: “Hatukuwahoji
wahusika kwa sababu kama tungefanya hivyo tungewapa hati ya
kutoshitakiwa na hivyo wasingeadhibiwa na kufikishwa mahakamani.” Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alipoulizwa
kuhusu suala hilo alisema kwa sasa hawezi kulitolea ufafanuzi, kwamba
anamsubiri Spika wa Bunge, Anne Makinda. Akifafanua Zitto alisema: “Kama kuna mtu
analalamika kuwa hakuhojiwa na PAC ajue kuwa tulikwepa ujanja wao wa
kutaka kupata kinga ya Bunge.”
Alisema Bunge liliazimia polisi na vyombo vingine
husika vya ulinzi na usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa
sheria za nchi dhidi ya watu wote waliotajwa na taarifa maalum ya kamati
kuhusika na vitendo vyote vya jinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya
Escrow na wengine watakaogundulika.
Juzi, baadhi yao, Ngeleja aliongoza Kamati ya
Nishati na Madini na kusema kuwa uchunguzi kuhusu tuhuma zinazowakabili
unaendelea na ikithibitika Bunge litachukua hatua.
CHANZO: MWANANCHI
Nape alisema Kamati Kuu imejadili na kufikia kuunda Kamati Ndogo
ya Maadili ili kufanya uchambuzi na tahmini za wagombea waliohusika na
adhabu waliopewa. Alisema Serikali imetakiwa kutekeleza kwa vitendo
maamizio yote ya Bunge kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow kabla
ya kikao cha Bunge Januari 27 na kutaka wahusika walioko kwenye dhamana
za uteuzi wachukuliwe hatua stahili na mamlaka zao kuwawajibisha mara
moja. Alisema Kamati Kuu imepitisha ratiba ya shughuli
za chama mwaka 2015 ikiwamo ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa
chama hicho kwenye uchaguzi ambao utapangwa na vikao husika.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment