Social Icons

Pages

Thursday, January 15, 2015

BURJ KHALIFA: JENGO REFU KULIKO YOTE DUNIANI


Kwa hesabu za haraka haraka, urefu wa mita 829.8 (sawa na futi 2,722) ni sawa sawa na viwanja vinane vya mpira wa miguu.
Uwanja wa mpira wa miguu uliotimia vizuri, una urefu wa mita 100, sasa vipangwe kwa mfuatano viwanja vinane halafu ongeza mita 29.8, ni kama mita 30 ndipo unapata urefu wa jengo la Burj Khalifa. Ni jengo refu kuliko yote duniani kwa sasa. Burj Khalifa lilijengwa katika eneo la ekari tatu kama kivutio cha mji wa Dubai, lakini ikiwa na matumizi mbalimbali ikiwamo makazi ya watu 30,000, hoteli kubwa tisa, maduka makubwa yanayojulikana kwa jina la Dubai Mall, pamoja na eneo la ekari 12 lililojengwa bwawa linaloitwa ziwa la Burj Khalifa. Balozi Mdogo wa Tanzania, Dubai, Omar Rajab Mjenga alisema katika mahojiano mafupi kuwa Dubai hawana mafuta wala mbuga za wanyama, kinachofanyika ni kuwekeza kwenye majengo yanayovutia. Anasema kuwa kinachofanyika Dubai ni amri, kwamba Mfalme wa Dubai akisema kitu kifanyike, kinafanyika na hakuna mjadala, lengo likiwa tayari limeshapangwa. Mtawala alisema mbadala wa mafuta Dubai ni kuwa na kivutio cha utalii. Balozi Mjenga anasema majengo marefu, mpangilio wa mji ni kivutio pekee cha utalii na sehemu kubwa ni fedha za wananchi zinazotoka mifukoni mwao. “Wamefanikiwa na watu wengi wanakuja kupumzika Dubai na kufanya ununuzi,” anasema. Naye dereva teksi, mkazi wa eneo hilo, Markiz Hamooud anasema kuwa imesaidia kuitambulisha Dubai kimataifa kuwa ni nchi pekee duniani yenye jengo refu. Anasema kuwa katika jengo hilo, haijawahi kutokea kukatika umeme na kwamba ikitokea watu wengi watakufa kwa kuwa sehemu kubwa wanategemea nishati hiyo.

Uamuzi wa kujenga Burj Khalifa
Uamuzi wa ujenzi wa jengo hilo refu ni wa serikali kwamba kwa kuwa Dubai haina mafuta, basi chanzo mbadala cha kuliingizia taifa mapato ni kutengeneza kitu cha tofauti ili kuwa kivutio cha watalii na ni jengo la Burj Khalifa. Inaelezwa kuwa Mtawala wa Dubai, Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum alitaka Dubai kuwa katika rekodi ya dunia kuwa ina kitu cha pekee na amefanikiwa. Kinachofurahisha katika jengo hilo ni kwamba, lina madirisha 24,348 ya vioo na vyuma na inachukua wiki nane kusafisha jengo zima.
Majengo marefu duniani
Kuna majengo mengi marefu duniani, katika nchi mbalimbali, lakini hakuna linalofikia Burj Khalifa. Jengo la Shanghai Tower lililopo China lina urefu wa mita 632 ambalo ni fupi kwa mita 200 za Burj Khalifa wakati jengo la tatu kwa urefu duniani ni Makkah Clock Royal Tower lililoko Saudi Arabia. Lina urefu wa mita 601.
World Trade Center lililoko kwenye mji wa New York Marekani lina urefu wa mita 541 ikiwa ni jengo jipya baada ya lile la awali lililoshambuliwa na magaidi Septemba 11, 2001. Jengo la tano kwa urefu duniani ni CTF Finance Centre, lililoko Guangzhou, ambalo linaendelea kujengwa na hadi litakapokamilika mwaka 2016, litakuwa na urefu wa mita 530.

Ujenzi wake Burj Khalifa
Kazi ya kuchimba msingi wa Burj Khalifa ulianzia Januari 2004 na kupitia changamoto nyingi hadi kuwa jengo linalovutia na alama ya Dubai. Ilichukua siku 1,325 na saa 22 milioni kukamilisha uchimbaji msingi na kufanyia vipimo hadi ghorofa ya mwisho. Msingi ulikuwa imara na ilichukua zaidi ya 330,000 m3 za ujazo wa zege la msingi na vyuma tani 39,000 (43,000 ST; 38,000 LT), ambavyo sasa vimebeba tani 110,000.
Msingi wenyewe umekwenda chini, urefu wa mita 50. Maboresho ya maeneo ya nje wakati ujenzi unaendelea, ulianza Mei 2007 na kukamilika Septemba 2009. Makandarasi wenye sifa za hali ya juu 380 walishiriki katika maeneo mbalimbali ya jengo. Jengo hilo, hadi kukamilika kwake, sehemu kubwa limeimarishwa kwa vyuma vya aluminiam na vioo kwa urefu wa mita 512. Jumla ya aluminium iliyotumika kujengea Burj Khalifa ni sawa na kujenga ndege tano aina ya A380 na urefu wa vyuma vilivyotumika kuimarishia jengo ni mara 293 ya urefu wa mnafa wa Eiffel ulioko Paris, Ufaransa.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: